Wazanzibari waishio Tanganyika wapinga kugawanywa

Rais Jakaya Kikwete

Jumuiya ya Wazanzibari Waishio Tanganyika imekuja juu ikipinga vikali mikakati ya kuwabagua inayolenga kuwatisha ili kuwarudisha nyuma wasiendelee kudai mamlaka kamili ya Zanzibar pamoja na Muungano wa haki na wenye maslahi kwa pande zote mbili.

Mikakati hiyo inadaiwa kufanywa na watu wa kubuni wanaojiita Umoja wa Wapemba Waishio Tanzania Bara (Neppelta) kwa kutumia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba, Machi 21, mwaka huu.

Tamko la jumuiya hiyo lilitolewa na Mwenyekiti wake, Abdallah Mohammed Kassim, marufu kama “Dullah”, jijini Dar es Salaam juzi.

Alisema kauli ya watu hao, ambayo ilinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni, imeonyesha ubaguzi wa dhahiri dhidi ya Wazanzibari, ambao kiasili ni wamoja licha ya kutenganishwa na bahari.

Abdallah alisema hawakubaliani na kauli ya watu hao iliyosisitiza kuwa wao ni “Wapemba” kwa kuwa Zanzibar ni moja na maslahi yake ni ya wote.

“Kitendo cha kusisitiza kuwa Muungano ukivunjika watakaopata hasara ni Wapemba ni ubaguzi kwani Wapemba ni Wazanzibar hivyo kuwabagua ni kujenga chuki miongoni mwa raia wa visiwa hivyo viwili ambao ni wananchi wa nchi moja,” alisema Abdallah.

Alisema Muungano uliopo ni wa nchi mbili, ambazo ni Tanganyika na Zanzibar na kwamba, Zanzibar ni visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo kuendelea kuwabagua Wapemba kwa maneno na vitendo ni kutowatendea haki.

Abdallah alisema uamuzi wa Wazanzibari kuishi na kufanya kazi Tanganyika ni haki yao ya msingi, hivyo kuwajengea hofu ni kuwanyima haki hiyo na kuwafanya waishi kwa mashaka makubwa, kitu ambacho alisema siyo kizuri kwa raia.

“Jumuiya ya Wazanzibari tunaoishi Tanganyika tunauliza kauli iliyotolewa na bwana Shehe Haji Faki ambaye alijitambulisha kama Mwenyekiti wa Wapemba waishio Bara kwa kusema idadi ya Wapemba waishio Bara imeongezeka hadi kufikia zaidi ya watu 800,000 mwaka 2012 na mtaji wa trilioni 1.2, takwimu hizi amezipata wapi?” alihoji Abdallah.

Alisema uhusiano na mwingiliano baina ya Wazanzibari na Watanganyika vilikuwapo kabla ya Muungano wa mwaka 1964.

Hivyo, akasema kuishi katika nchi yoyote duniani hakutegemei Muungano, kwani wapo Watanzania wanaishi nchi mbalimbali duniani bila ubaguzi na hata Tanzania wapo raia wengi wa kigeni wanaoishi licha ya kuwa nchi hizo hawajaungana nazo.

“Wazanzibari waliopo Tanganyika na kumiliki ardhi na mali isiwe sababu ya kuwatisha na kuwajengea hofu ya kudai maslahi ya nchi yao, kwani utaifa wa mtu hauwezi kutupwa kwa sababu ya kumiliki ardhi, mali, kuoa au kuolewa,” alisema Abdallah.

Alisema umoja uliopo miongoni mwa Watanzania unakumbusha kuwa wanaofaidika na Muungano siyo Wazanzibari pekee, kwani faida hizo zipo kwa raia wa pande zote mbili za Muungano.

CHANZO: NIPASHE

Dk. Slaa: Upinzani hatuna lengo la kuvunja Muungano

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia (Chadema),Dk. Willibroad Slaa.

Katibu  Mkuu wa Chama cha Demokrasia (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, amewataka Watanzania kutambua kuwa hakuna chama cha upinzani ambacho kina lengo la kuvunja Muungano bali yanayoelezwa ni njama ya kudhoofisha msimamo wa kuwapo kwa serikali tatu.

Alitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Tangamano, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa jiji la Tanga, baada ya kuongoza timu ya viongozi wa juu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mjini hapa na kuwataka wakazi wa jiji hilo kukataa hadaa zinazofanywa kwa lengo la kukanyaga rasimu ya katiba, ambayo waliitolea maoni yao.

Alisema kilichofanywa na Rais Jakaya Kikwete, wakati akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba kuiponda rasimu ya katiba ni kumdhalilisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambaye ni kiongozi mwenye heshima Tanzania na nje ya nchi na kwamba, Ukawa itazunguka nchini kote kumtetea.

Dk. Slaa ambaye ni Mwenyekiti wa Ukawa nje ya Bunge hilo, alisema Rais Kikwete anawahadaa wananchi anaposema wanaotaka serikali tatu wana lengo la kuvunja Muungano na kusisitiza kuwa hakuna chama chochote cha upinzania, ambacho kinataka Muungano uvunjike.

“Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na wananchi wote wa Tanzania Bara na hata visiwani, hakuna anayetaka Muungano uvunjike, bali kinachofanywa na CCM ni kuwachonganisha kwa wananchi ili waonekane ni maadui wa Muungano,” alisema Dk. Slaa.

Alisema inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar ndani ya Bunge hilo wakidanganywa kuahidiwa kupewa fedha za kuwasomesha ili waunge mkono msimamo wa kupiga kura ya serikali mbili jambo ambalo ni kinyume cha malengo ya uwakilishi wao kwa Watanzania.

“Chini ya Umoja wao wa Ukawa wanachofanya ni kutetea maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye Tume ya Katiba kwa kuwa Tanzania ni nchi ya wote na hakuna, ambaye akifa atazikwa nje ya nchi hii. Hivyo, ni lazima kutetea maslahi ya wananchi,” alisema Dk. Slaa.

KAIMU KATIBU MKUU WA CUF ANENA
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Shaweji Mketo, alisema Tume ya Maridhiano ya Zanzibar inayoundwa na viongozi kutoka CCM na CUF ikiongozwa na Nassoro Moyo, imetoa tamko la kumtaka Rais asidhani Watanzania ni watu wa kuhadaiwa, bali watatetea serikali tatu kwa kuwa ina lengo  la  kuimarisha  Muungano  uliopo.

CHANZO: NIPASHE

Diwani mbaroni kwa kufunga ofisi za serikali

Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanya, Benson Mpesya akitoa maelekezo kwa fundi ili kufungua mlango unaodaiwa kufungwa na diwani na watu wengine watatu. Picha: Mohab Dominick.

Watu  watatu  akiwamo  Diwani wa Kata ya Mwendakulima ya Halmashauri ya Wilaya ya  Kahama mkoani Shinyanga,  Ntabo Majhabi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufunga ofisi za serikali za mtendaji wa kata hiyo.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo wiki iliyopita  asubuhi baada ya mtendaji wa kata hiyo,  Cecilia Clement kupigiwa simu na mlinzi wa ofisi hizo, Joseph Katambi na kumpa taarifa za tukio hilo liliofanywa na wananchi 15 walioambatana na diwani huyo.

Kwa mujibu mtendaji huyo, waliamua kuibadilisha kamati ya sungusungu ya kata hiyo hali ambayo ilianza kuleta malalamiko na minong’ono na kwamba huenda ni chanzo cha watuhumiwa hao kufunga ofisi hizo.

Aliwataja wengine walikamatwa kuwa ni fundi selemala,Hamisi Abbas  na Makaka Benedictor,  wakazi wa kata hiyo.

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kahama,  Benson Mpesya akiongozana na kamati ya ulinzi ya kata na askari polisi, walifika katika ofisi hiyo  kushuhudia mlango huo ulivyofungwa kwa kuwekewa kipande cha bati na kupigiliwa misumari  na mawe.

Mpesya  alitoa amri ya kuvunjwa kwa bati hilo chini ya ulinzi wa polisi na kuamuru waliohusika akiwamo diwani huyo kukamatwa na kutiwa mbaroni.

Akizungumzia kitendo hicho Mpesya, alisema ni fedheha na kisichoweza kuvumilika .

CHANZO: NIPASHE

Msekwa: Sitta ana lake jambo

Aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa 


Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta kukiri kuchezewa kwa saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msekwa amesema, ‘mzungumzaji huyo ana lake jambo’.

Sitta akizungumza na gazeti hili juzi mjini Dodoma alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya 1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.

Alifafanua kuwa saini ya Nyerere imeongezwa herufi ‘us’ kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno ‘Msekwa’ kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini walifanya makosa.

Msekwa akizungumza na gazeti hili jana alisema: “Saini iliyo katika hati original (halisi) ni ya kwangu mimi, lakini huyo anayesema zimechezewa muulizeni atakuwa na lake jambo. Kama kompyuta imekosea ni leo kwa kuwa kipindi hicho kompyuta hazikuwapo.”

Aliongeza: “Ana lengo gani la kutilia shaka, ana lengo gani la kusema imechakachuliwa, kinachotakiwa ni hati original ambayo iko ofisi ya Katibu wa Bunge itolewe, kwanini tuendelee kuandikia mate wakati wino upo?”

Maoni mengine

Mjumbe wa Bodi ya Kituo cha Taarifa kwa Wananchi Umma (TCIB), Hebron Mwakagenda alisema yote hayo yanatokea ni kuvuruga hoja iliyopo mezani.

Alisema kitendo cha kupoteza muda kuzungumzia suala la kuchezewa kwa saini halitakiwi kwani kama maudhui yake hayakuchezewa basi hoja ya muundo wa Muungano uamuliwe na wananchi wenyewe.

“Tusianze kupoteza muda kwa mambo ambayo hayapo cha msingi wananchi wenyewe waulizwe wanaupenda Muungano au la lakini tusianze kumtafuta mchawi kuwa saini zimechezewa wananchi waamue wenyewe kuhusu Muungano,” alisema Mwakagenda.

Sakata lilivyoanza

Utata huo ulianza wiki hii baada ya kamati za Bunge Maalumu la Katiba kuanza vikao vyake vya kujadili sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba, zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wake.

Hali hiyo ilitokana na kutopatikana kwa hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ile ya Sheria ya Baraza la Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa Muungano.

Aprili 2 mwaka huu, Kamati namba 2 ilimwalika, Spika Mstaafu wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, lakini uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa aliitwa kutokana na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha, alithibitisha kutokea utata huo na kwamba walilazimika kumuita Msekwa ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa na Msekwa alisema saini zilizopo katika hati hiyo ni ya kwake.

Nahodha alisema kwa maelezo ya Msekwa, inaonekana hati ya Muungano ipo Umoja wa Mataifa (UN), kwani kabla ya Muungano, Tanganyika ilikuwa na kiti chake UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hali kadhalika.

Aliongeza kuwa baada ya UN kuomba uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi kurejeshwa.

Kwa upande wake Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo siyo rahisi kuipeleka bungeni Dodoma.

Kamati kumi zaitesa CCM

 
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba 


Dodoma. Kura za awali katika Kamati 10 kati ya 12 za Bunge Maalumu la Katiba, zinakipa wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi,(CCM) kutekeleza azma yake inayotajwa kuwa ni kufumua Rasimu ya Katiba, ili kuondoa mapendekezo ya Muundo wa serikali tatu, baada ya wajumbe wa Zanzibar kukwamisha upatikanaji theluthi mbili.

Kwa mujibu wa taarifa za kamati, ambazo tangu juzi zimeanza kutolewa katika sura ya kwanza na sita zinazungumzia Muundo wa Muungano, wajumbe kutoka Zanzibar kwa sasa ndiyo kikwazo kikubwa kwa CCM.

Hata hivyo, uamuzi ya mwisho kuhusu Muundo wa Serikali, kati ya mbili au tatu, unatarajiwa kujulikana Alhamisi wiki ijayo, wakati kamati zote zitakapowasilisha taarifa zao na kupigwa tena kura kwa wajumbe Tanzania Bara peke yao na Zanzibar peke yao.

Iwapo wajumbe wa Zanzibar wakiitetea kwa theluthi mbili kama sasa, mapendekezo ya muundo wa serikali tatu ndiyo yatakayopelekwa kwa wananchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wenyeviti wa kamati hizo, Stephen Wassira, Ummy Mwalimu, Anna Abdalah na Paul Kimili, walitaja moja ya vifungu ambavyo vimeshindwa kupata theluthi mbili kuwa ni ibara ya kwanza kifungu cha kwanza.

Akizungumza jana Wassira ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita alisema kwamba katika kamati yake ibara hiyo imeshindwa kupata theluthi mbili, ili kuweza kufanyiwa marekebisho.

“Lakini huu siyo mwisho kama nilivyosema awali, tukirudi bungeni tutapiga kura kwa wajumbe wote na ndiyo itakuwa na uamuzi wa mwisho kama muundo wa Muungano utakuwa na Serikali tatu ama mbili, ambao utapelekwa kwa wananchi,” alisema Wassira.

Jussa, Lissu- tumeibana CCM

Jussa alisema: “Kwa taarifa za matokeo tulizonazo katika Kamati Namba 1, 2, 3, 4, 6, 10, 11 na 12 mapendekezo ya kubadilisha Rasimu katika ibara hizo mbili yamekwama. Kama CCM wakichakachua sura ya kwanza na sita, maana yake ni kwamba hapa hakuna Katiba, hakuna kura ya maoni na hakuna mwafaka.”

Vifungu hivi pia kwa mujibu wa wenyeviti wa kamati nyingine, isipokuwa kamati ya Tano, ambayo inaongozwa na Hamad Rashid, havikupata kura theluthi mbili na hivyo kubaki kama vilivyo kwenye rasimu.

Naye Lissu alisema kwa sasa CCM ndiyo inaweza kuanza mkakati wa kuvuruga Bunge kwani tayari wamejua hawana theluthi mbili ya Zanzibar ili kubadili Rasimu kama wanavyotaka.

Matumaini ya kupatikana MH370 yakolea

Operesheni ya kuitafuta MH 370 inaendelea.

Kiongozi wa operesheni ya kuitafuta ndege ya Malaysia ya MH370 iliyotoweka mwezi mmoja uliopita, Angus Houston wa Australia, amesema kuwa ametambua mawimbi ya sauti inayoaminika kutoka kwa kinasa sauti cha ndege hiyo maarufu kama 'black box' ya ndege hiyo.

Houston alisema kuwa kifaa maalumu kinachokokotwa na meli moja ya kijeshi ya Australia, Ocean Shield, kilipata mawimbi kamili kwa muda wa kati ya dakika tano u nusu na saba.

Mawimbi sawa na hayo yaliopatikana mwishoni mwa wiki na hii ina maana kuwa wataweza kulenga eneo ambalo inaaminika zaidi kuwa ndege hiyo ilianguka na kwa hivyo kuimarisha utafutaji wake.

Kesi ya kusafirisha twiga hai kusikilizwa leo


Moshi. Kesi ya uhujumu uchumi ya kusafirisha wanyamapori hai wakiwamo twiga wanne kutoka Tanzania kwenda Jiji la Doha Qatar, itaendelea kusikilizwa leo kwa siku mbili mfululizo.

Twiga hao na wanyama wengine walitoroshwa kwenda Uarabuni Novemba 26, mwaka 2010 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) kwa kutumia ndege kubwa ya Jeshi la Qatar.

Washitakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni pamoja na raia wa Pakistan, Kamran Ahmed, Hawa Mang’unyuka, Martin Kimath na Michael Mrutu ambao wote wako nje kwa dhamana.

Wanyama waliotoroshwa kwenda Doha wenye thamani ya Dola 113,715 za Marekani sawa na Sh170.5 milioni za Tanzania, walisafirishwa kwa kutumia maboksi marefu huku wakitumia ndege hiyo. Ushahidi ambao tayari umeshatolewa mahakamani unaeleza kuwa wanyama hao walikamatwa katika maeneo ya Mto wa Mbu, Elboreti na Engaruka wilayani Monduli.

Lugola: JK amemziba mdomo Warioba

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Kangi Lugola.

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Kangi Lugola amesema hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete imemziba mdomo Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

“Tulitarajia itakuwa hivyo na ndiyo maana kulikuwa na ubishi kwa nini Rais Jakaya Kikwete asingetangulia kwa mujibu wa kanuni halafu ndiyo aje Mwenyekiti wa Tume wa Mabadiliko ya Katiba, Jaji  Warioba,” alisema.

Alisema hotuba  iliyotolewa na Rais Kikwete imekwenda mbali zaidi kwa sababu na yeye alikuwa anachangia katika utungaji wa katiba kutokana na kuchambua kifungu kwa kifungu.

“Nimemsikiliza...nimeyatafakari yale yote ambayo ameyatoa kwenye hutuba yake...kwa sababu alitoa msamiati kwamba tumia akili ya kuambia na uchanganye na ya kwako...basi ametuambia na sisi tutaenda kuchanganya na akili yetu katika kutunga katiba ya wananchi,” alisema.

Naye, Mjumbe wa Bunge hilo, Aden Rage alisema watahakikisha kwamba wanachukua ushauri wa Rais Kikwete ikiwa ni pamoja na kuweka maslahi ya taifa mbele.

“Tutaweka maslahi ya taifa mbele...interest (maslahi) ya nchi kwanza...tutashindana kwa hoja, na kuwahakikishia wananchi kupata katiba inayofaa,” alisema.

Bunge hatarini kuvunjika,adai mjumbe

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mustapha Akunaay.

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Mustapha Akunaay, amesema kuna hatari kubwa la Bunge hilo kuvunjika kutokana na kauli iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akihutubia wajumbe wa bunge hilo.

Akunaay ambaye pia ni Mbunge wa Mbulu (Chadema), alisema bila tahadhari, kuna hatari kubwa ya Bunge hilo kuvunjika.

Alitoa kauli hiyo, kufuatia Rais Kikwete kuzungumzia kwa undani na kusema muundo wa serikali tatu haufai na hauwezi kutekelezeka.

Alisema wao kama wajumbe na wabunge hawakutakiwa kulizungumzia suala la serikali mbili au tatu kwa sababu suala hilo lilishaamuriwa na wananchi.

“Rais Kikwete amezungumzia sana kuhusu serikali mbili kwa hiyo amewachanganya watu kuhusu muundo wa serikali mbili au tatu, sasa hali hii itakuwa ngumu zaidi kwenye kufanya uamuzi,” alisema.

“Maana dakika za mwisho kaja kusema kwamba msije mkaanza kung’ang’ania mambo ya kura, lazima mfanye mambo ya makubaliano...kwa hiyo mimi nimeachwa asilimia 30 kwa 70, alisema.

Mtendaji wa kijiji auawa kwa mapanga

Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Zelothe Steven.

Kundi la watu wasiofahamika, wamemuua kwa kumcharanga mapanga, Mtendaji wa kijiji cha Chakama kata ya Mwenge, Halmashauri ya mji wa Masasi mkoani Mtwara, Selemani Eckoni (32).

Mtendaji wa kijiji cha Mwenge, Mely Karim, alisema kuwa tukio hilo la kinyama lilitokea usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Mwenge wakati mtendaji huyo akiwa nyumbani kwake amejipumzisha.

Karim alisema taarifa za kuuawa kwa mtendaji huyo zilianza kuenea kijijini hapo jana asubuhi baada ya baadhi ya watu kusikia sauti ya mtoto wa marehemu, Makala Selemani (6), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mwenge akipiga mayowe kuomba msaada baada ya yeye kuona baba yake akiwa amelala nje ya nyumba yao akivuja damu kichwani huku pembeni yake kukiwa na kitanda cha kamba.

Alisema kufuatia mayowe ya mtoto huyo, wananchi walikusanyika katika nyumba ya marehemu na kukuta mtendaji huyo tayari amefariki dunia huku akiwa na majeraha makubwa kichwani.

Alisema baada ya watu hao kufanya mauaji hayo, waliingia ndani ya nyumba ya marehemu na kuchukua pikipiki moja aina ya Sanlg, deki moja ya televisheni na simu aina ya Nokia.

Kaka wa marehemu, Hassan Issa, alisema alipelekewa taarifa za kuuawa kwa ndugu yake akiwa nyumbani kwake.

Issa alisema alikwenda nyumbani kwa marehemu na kupiga simu polisi kuelezea taarifa za mauaji hayo.

Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Zelothe Steven, alithibisha kutokea kwa mauaji hayo.

Hata hivyo, Kamanda Steven alisema chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika na hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kuhusiana na mauaji hayo.

Baadhi ya ndugu wa marehemu wameliambia NIPASHE kuwa wakati wa uhai wake, mtendaji huyo aliyeacha watoto wanne, alikuwa akiishi peke yake.

Mbunge Kigwangalla mbaroni

Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kingwangalla (CCM).

Mbunge  wa Nzega, Dk. Khamis Kingwangalla (CCM), ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi katika tukio la vurugu kwenye machimbo ya dhahabu.

Vurugu hizo ziliibuka jana katika machimbo ya dhahabu ya Mwashina yaliyopo wilayani Nzega, Tabora na Jeshi la Polisi kulazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya wachimbaji wadogo waliokuwa wakiandamana wakiongozwa na mbunge huyo.

Wananchi hao walikuwa wakiandamana jana kuanzia eneo la Isunga Ngwanda kuelekea katika machimbo hayo kupinga kitendo cha serikali kufunga machimbo hayo ambayo wamekuwa wakichimba dhahabu kwa muda mrefu na kuwasaidia kupata riziki.

Vurugu hizo ambazo zilianza majira ya mchana, zilisababisha watu wengine kadhaa kutiwa mbaroni sambamba na Dk. Kigwangalla.

Dk. Kigwangalla akizungumza na NIPASHE kwa simu muda mfupi baada ya kutiwa mbaroni, alisema wakiwa katika maandamano hayo polisi walianza kuwatawanya waandamanaji kwa mabomu ya machozi na yeye alifanikiwa kutoroka.

Hata hivyo, baadaye polisi walifanikiwa kumkamata na kumuweka ndani na hadi jana saa 10:45 jioni, mbunge huyo alikuwa bado chini ya ulinzi wa polisi huku waandamanaji wakiwa wametawanyika.

“Soma facebook yangu, nimenusurika kufa na sasa nimekamatwa na polisi na kuwekwa ndani…baada ya askari kuwatawanya wananchi kwa risasi za moto. Nitatoka kwenye mawasiliano sasa hivi,” alisema Dk. Kigwangala wakati akizungumza na NIPASHE.

Dk. Kigwangalla katika mtando wake wa facebook alisema katika vurugu hizo kijana mmoja aliyekuwa karibu naye alipigwa risasi baada ya riasi hiyo kumkosa yeye.

“Nimenusurika kuuawa muda si mrefu. Mungu mkubwa. Askari kwenye gari ananiambia na bahati yako nimekukosa, nililengwa kichwa....kijana mmoja aliyekaa mbele yangu amepigwa risasi kwenye paji la uso, sijui kama amenusurika,” alisema na kuongeza:

 “Vijana wamenilinda kwa ujasiri bila hofu. Leo askari wamenikamata kwa staha. Siwezi kukubali kamwe dhuluma ya mabepari dhidi ya wanyonge. Niliwaahidi na niliapa kuwatetea.”

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Bituni Msangi, alisema alijulishwa kuwapo kwa vurugu hizo na Mkuu wa Polisi wa wilaya (OCD).

“Nipo nje ya wilaya, lakini nimepata taarifa kutoka kwa OCD kwamba kumetokea vurugu ila sijafahamu vurugu hizo zimesababishwa na nini,” alisema Msangi.

Hata hivyo, taarifa ambazo zililifikia gazeti hili jana  jioni, zilieleza kuwa wachimbaji  watano akiwamo mbunge huyo waliokamatwa sambamba na mbunge huyo wamewekwa katika kituo kikuu cha polisi wilayani humo.
 

Boti la wakimbizi lazama Ziwa Albert


Mili 25 imepatikana Ziwa Albert baada ya boti iliyokuwa imebeba wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuzama.

Wakimbizi wa mapigano mashariki mwa Congo

Wakimbizi hao walikua wakitoroka kutoka kambi ya wakimbizi ya Kyangwali wilayani Hoima magharibi mwa Uganda, wakirejea kwao.

Kwa sasa Jeshi la polisi linaendelea na jitihada za kutafuta miili zaidi. Kamanda wa polisi wa eneo hilo John Ojukuna amesema watu 43 wameokolewa. Boti iliyozama inadhaniwa kuwa ilikua imebeba zaidi ya wakimbizi 100.

Wengi wa wakimbizi hao ni wale waliokimbia mapigano mashariki mwa Congo mwaka jana.

Mwendeshaji wa boti hiyo amekamatwa na jeshi la polisi na inadaiwa kuwa alikua amelewa. Wakimbizi waliookolewa wameambia polisi kuwa alikuwa mlevi na alikua akiendesha boti hiyo kwa kasi sana.

Hii sio mara ya kwanza ajali ya boti kuua watu katika Ziwa Albert kutokana na kujaza abiria na mizogo kupita kiasi.Miaka minne iliyopia boto nyingine ilizama na kusababisha vifo vya watu 70.

Waponea kifo mikononi mwa Boko Haram


Jeshi linaendelea kuwasaka wapiganaji wa Boko Haram

Wasichana waliotekwa nyara na kundi lenye itikadi kali za kidini, Boko Haram nchini Nigeria, wameielezea BBC ukatili walio upitia mikononi mwa kundi hilo.

Wakati wakizuiwa, wasichana hao walishuhudia watu kadhaa wakiwemo baadhi wanaotoka kijiji kimoja na wapiganaji wa kundi hilo, wakikatwa shingo.

Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 23, ameiambia BBC kwamba ameona kiasi ya raia hamsini wakiuawa mbele yake na Boko Haram.

Hili limefanyika miezi kadhaa iliyopita katika kambi moja katika eneo la mashambani, la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Wakati huo huo msichana mwingine alieleza jinsi wapiganaji hao walivyo mlazimisha kumuua mwenziwe ambaye pia alitekwa nyara.

Wote walifanikiwa kutoweka kutoka kambi hizo na sasa wanaishi mafichoni.

Jeshi la Nigeria linasema linaendelea kuwasaka wapiganaji wa kundi la Boko Haram katika eneo hilo lililo mashinani.

Wapiganaji hao wanaendelea kuyashambulia miji na vijiji katika kiwango cha kushtusha ambapo zaidi ya raia mia tano wameuawa katika wiki za kwanza za mwaka huu.

Simu yawa mkombozi wa wajawazito Kilindi


Afya ya Mama na mtoto ni muhimu katika maendeleo ya kila Taifa. Ni vyema afya za kundi hili zizingatiwe kwa kiasi kikubwa ili kuepusha vifo hivyo.

Kilindi. Wengi kati yetu wanaifahamu simu kwa matumizi yao ya mawasiliano ambayo huitumia kuzungumza kirafiki au kutumiana ujumbe.

Kwingineko, simu inatumika kwa majukumu mengine yakiwamo ya tiba na imeonyesha mafanikio na kuwa mkombozi.

Wilayani Kilindi mkoani Tanga, imebainika kuwa teknolojia ya kisasa  inayoitwa Simu ya Teknolojia ya Utoaji wa Huduma ya Afya Ngazi ya Jamii  kwa Kutumia Data (MHEALTH) imefanya maajabu.

Huduma hiyo iliyoanzishwa na Mradi wa Afya Mama na Mtoto Kupitia Shirika la World Vision imewezesha wahudumu wa afya ya jamii kuwasaidia kinamama na watoto wanaozaliwa.

Mhudumu wa afya, Pili Juma anaeleza kuwa walipewa simu hizo mahususi kwa utoaji wa huduma kwa mama na mtoto chini ya umri wa miaka mitano na kwamba  zina uwezo mkubwa wa kutoa mwongozo kwao (wahudumu).

Anasema kuwa badala ya kutumia vitabu, sasa wanao mfumo rahisi wa kutumia simu unaomwezesha mhudumu kutoa huduma kwa mjamzito na kubaini matatizo yake.

Anaongeza kuwa simu hiyo inamwongoza mtumiaji wake kubaini tatizo alilonalo mjamzito na kama anatakiwa apelekwe kwenye kituo cha afya au hospitali ili kuokoa maisha yake, hufanyika hivyo haraka.

“Simu hizi zimerahisisha  utoaji huduma, hatuendi tena kupeleka taarifa kwenye vituo vya afya kwa kutumia mafaili au karatasi, hivyo taarifa za wajamzito na watoto zinapaikana kupitia teknolojia hii,” anasema.

Anaongeza kuwa teknolojia hiyo inawawezesha kuchukua maelezo ya mjamzito moja kwa moja kwenda kwa ofisa mradi huo, vituo vya afya au hospitali ya wilaya.

Simu inavyofanya kazi

Mtaalamu huyo anaeleza kuwa simu hiyo inamwonyesha mtoa huduma anapomtembelea mjamzito nyumbani anapokuwa na mimba chini ya miezi minne kwa mara ya kwanza anatakiwa apewe elimu ya kuhudhuria kliniki, kujua dalili za hatari wakati wa ujauzito na ushiriki wa wenza wao.

Pia, inamwonyesha mtoa huduma  akitoa elimu ya lishe bora wakati wa ujauzito na anaponyonyesha, wakati anapotaka kujifungua na kutoa ushauri wa kupima Ukimwi na kuzuia maambukizo yake kwenda kwa mtoto atakayejifungua.

Huduma nyingine itamwezesha mhudumu kutoa elimu kwa mama mjamzito kupima malaria na kumpima mtoto wake aliye na umri chini ya miaka mitano na kutoa ushauri kwa waume zao wahudhurie kliniki.

Aidha, mtoa huduma anapomtembelea mama huyo kwa mara ya pili atatoa elimu kwa kuyarudia yote aliyomweleza wakati alipomtembelea kwa mara ya kwanza.

Kwa mara ya tatu,  mtoa huduma atatoa elimu kwa mama huyo jinsi ya kumhudumia mtoto atakayezaliwa, dalili za hatari baada ya kujifungua ili akiziona aende kituo cha afya.

Pia, simu hiyo itamwonyesha mtoa elimu kwa mama mwenye Virusi vya Ukimwi (VVU) kuhusu  namna ya kumnyonyesha mtoto wake na kutumia uzazi wa mpango na kuzuia maambukizi katika jamii.

Ofisa Mradi wa Afya wa Afya Mama na Mtoto Wilaya ya Kilindi, Jacqueline Kawiche anaeleza kuwa mradi huo kwa kushirikiana na Shirika  la D-Tree wametoa simu hizo kwa wahudumu wa afya ya jamii ambazo zina programu inayoitwa Com- Care.

Kawiche anasema mhudumu wa afya anapokwenda kumtembelea mjamzito hataenda na makaratasi, hivyo atatumia simu hiyo ambayo ina mwongozo wa Wizara ya Afya wa kutumia Bango Kitita.

“Mwongozo ule wa Wizara ya Afya ambao kwa sasa unatolewa kwenye kaya kupitia makaratasi, sasa unatolewa kwa njia ya simu,” anaeleza.

Faida ya teknolojia hiyo ya simu inamrahisishia  mhudumu wa afya kufanya kazi  na  hivyo anapomhoji mjamzito ambaye ana matatizo hatarishi simu yake hutoa ishara  kuwa mama huyo apelekwe kituo cha afya.

Teknolojia hiyo ya simu inasaidia ukusanyaji wa taarifa kwa wakati, mfano mjamzito anapotembelewa kwenye kaya yake, taarifa hizo zinafika kwa ofisa afya, zinafika kituo cha afya au zahanati husika na baadaye zinatunzwa  kwenye mfumo wa taarifa kwenye hospitali ya wilaya.

Taarifa hizi za mama mjamzito zinakwenda kwa wakati na humsaidia mhudumu wa afya kutoa rufaa ya kumpeleka kituo cha afya kama atagundulika ana dalili hatarishi.

Usiyoyajua kuhusu uchunguzi wa miili ya maiti nchini Tanzania

Selemani Uliza akionyesha kitanda cha kusafishia na kuchunguza miili ya marehemu.

Maiti ya Adrian Louis iliokotwa kando ya barabara kuu ya kwenda Lukuledi wilayani Masasi katika Mkoa wa Mtwara.

Haikuwa na jeraha lolote. Ndugu zake walipopata taarifa za msiba, waliuchukua mwili na kuusitiri harakaharaka.

Hawakuwa na wasiwasi wowote wa kutaka kujua chanzo cha kifo cha ndugu yao kwani waliamini kuwa amefariki dunia kwa sababu ya kuzidiwa na ulevi, kwa kuwa siku zote alikuwa mlevi kupindukia. Kumbe, walikuwa wamekosea, kwani siku hiyo Louis hakuwa amelewa, bali kifo chake kilisababishwa na majambazi waliompora fedha kabla ya kumnyonga  hadi kufa.

Yapo matukio mengi ya namna hiyo katika sehemu mbalimbali nchini, lakini mengi kati ya hayo hayafanyiwi uchunguzi wa kujua chanzo.

Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa na Kiongozi wa Idara ya Uchunguzi wa Vifo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Innocent Mosha anasema ni muhimu kufanya uchunguzi wa sababu za kifo ili kujiondolea shaka au wasiwasi wa kipi kilisababisha kifo hicho.

Dk. Mosha anaelezea maana ya uchunguzi wa kifo na kusema kuwa ni  kitendo cha madaktari kutafuta chanzo kilichosababisha kifo cha mtu na kujiridhisha au ndugu kuridhika pasipo shaka.

“Watanzania walio wengi bado hawafahamu umuhimu wa kufanya uchunguzi wa vifo vya ndugu zao, jambo ambalo linasababisha wakati mwingine kupoteza ushahidi au kukosa  cheti cha kifo ambacho kina umuhimu mkubwa katika masuala ya mirathi,” anasema Dk Mosha

Anasema uchunguzi wa kifo si kwa ajili ya polisi wa upelelezi tu, bali ni mchakato unaotakiwa kufanywa  na ndugu wa marehemu ili kujiridhisha na sababu ya kifo cha ndugu yao.

Anaongeza kuwa tatizo kubwa hapa nchini ni kuwa watu wengi hawaelewi maana na umuhimu wa kuchunguza miili ya ndugu zao ili kujua chanzo au sababu za vifo vyao.

Mchakato wa Uchunguzi

 Kwanza, Dk. Mosha anasema uchunguzi wa kifo kwa matukio yanayohusisha polisi, huhitaji taarifa ya utangulizi ambapo polisi hutakiwa kutoa maelezo ya awali kuhusu marehemu.

Anasema pia kuwa katika matukio hayo, ndugu zaidi ya mmoja  huhitajika kwa ajili ya kumtambua marehemu,  sanjari  na kujaza fomu ya maelezo mafupi. “Baada ya polisi kutoa maelezo yao ambayo kwa kawaida huwa ni mafupi, daktari huendelea na uchunguzi wake kulingana na ujuzi wake,” anasema.

 Anaeleza kuwa zipo hatua kadhaa za kufanya uchunguzi wa kifo ambazo  hazina budi kufuatwa. Anazitaja kuwa marehemu huchunguzwa  sehemu za nje za mwili akiwa na nguo zake.

“Hapo daktari huangalia mazingira ya nje, kwa mfano nguo alizovaa; iwapo zina damu; damu imeingiaje, kama zimechanika  na zilikuwa katika mazingira gani. Utambuzi huu wa awali wakati marehemu amevaa nguo zake, huweza kutuonyesha mazingira ya nje iwapo kulikuwa na purukushani kabla ya kifo au la,” anasema.

Baada ya hapo, Dk. Mosha anasema daktari hutakiwa kwenda hatua ya pili ya kuchunguza ndani ya mwili ambapo mwili wa marehemu huchunguzwa kwa umakini mkubwa kama kuna chochote kitakachoashiria sababu ya kifo chake.

 Kwa mfano, Dk. Mosha anasema majeraha ya mwili huangaliwa, pia mazingira ya majeraha hayo.

Anaongeza kuwa hapo daktari anaweza kujua iwapo marehemu alipigwa alizama majini, alikunywa maji mengi au  kuzamishwa majini.

“Kama mtu amezama majini ni rahisi kujua kwani macho yake huwa na mshipa midogo midogo iliyovilia damu. Mwingine huwa na kitu kinachoitwa ‘Perypheral discoloration’ ambapo  kisigino cha marehemu huwa na rangi ya bluu kwa sababu ya kukosa hewa ya oksijeni.” Mtaalamu huyo anasema wakati mwingine uchunguzi wa vifo hivi ni  muhimu kwani husaidia kujua iwapo mtu amefia majini au aliuawa, kisha akatupwa kwenye maji.

Uchunguzi wa mwingine wa vifo vya marehemu huweza kuhusisha kumpasua mwili na kisha kuangalia ogani kama ini, figo, mishipa ya damu, utumbo na kifua.

 Pia, mwili wa marehemu huangaliwa kama kuna uvimbe usoni, mapafu kujaa maji na wakati mwingine mapafu hutolewa na kupimwa kama yameingia maji na maji hayo ni ya aina gani.

 Kuna watu wanaofariki wanaodhaniwa kuwa wamejinyonga kuna utaalamu wa kuangalia kama kweli wamejinyonga au walinyongwa na kutundikwa.

Anasema uchunguzi wa kifo cha marehemu si lazima kuukatakata mwili,  bali wakati mwingine  wataalamu wanaweza kuchukua maelezo au kukata  sehemu ndogo tu ya mwili huo.

“Wakati mwingine iwapo mgonjwa amefariki dunia kwa kuugua malaria au aliletwa hospitali akiwa anaumwa ugonjwa huo na kama amekufa, basi ili kuthibitisha sababu ya kifo hicho, tunaweza kukata tishu kuangalia dalili za malaria katika mwili, kuangalia rangi ya manjano katika macho au wakati mwingine kipande cha ini kinachunguzwa,” anasema.

Gharama za uchunguzi

Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Muhimbili, Dk.  Praxeda Ogweyo anasema  gharama za uchunguzi kwa watu wa kawaida ni  Sh200,000, lakini kwa raia wa kigeni ni 800,000. Anasema kwa madaktari wanaotaka kufanya uchunguzi wa vifo kwa sababu za kitaaluma hawatozwi gharama zozote na kwa polisi gharama zao hulipwa na serikali.

Dk. Ogweyo anasema ni wakati kwa Watanzania kujifunza na kuujua umuhimu wa uchunguzi wa vifo vya ndugu zao kwa kuwa husaidia kusuluhisha migogoro ndani ya familia.

“Kama ndugu wanahisi  kuwa kifo cha ndugu yao kina utata basi uchunguzi unasaidia. Mara nyingi mtu anapofariki ghafla huleta utata kwa jamii,” anasema

Dhana au mazoea

Dk. Mosha anasema kuna dhana zilizozoeleka kuwa  kama mtu ameuawa, basi sura ya muuaji huonekana kwenye macho ya marehemu, lakini anasema  hilo halina ukweli kwani kinachoonekana machoni ni kuvilia kwa damu au kuvimba kwa macho kwa sababu kama za kunyongwa.

Takwimu za uchunguzi

Kuhusu hilo, Dk. Mosha anasema  Watanzania wengi hawafanyi uchunguzi wa vifo vya marehemu ndugu zao kwa sababu ya dhana potofu kuwa ndugu zao hukatwakatwa au kuibiwa baadhi ya viungo. “Wengi wanaochunguza vifo vya marehemu ni polisi kwa sababu za kipolisi na madaktari kwa sababu za kitaaluma. Lakini watu wa kawaida bado hawana uelewa kuhusu uchunguzi wa vifo.”  Kwa mfano, takwimu za  hapa Muhimbili zinaonyesha kuwa uchunguzi wa vifo vya marehemu unaofanywa kwa maombi ya ndugu ni watu wawili hadi wa tatu kwa mwezi wakati uchunguzi unaofanywa kwa maombi ya polisi ni matukio sita hadi saba kwa wiki.

Sababu za kuchunguza miili

 Dk. Mosha anasema, uchunguzi wa miili ya marehemu una umuhimu mkubwa katika kufahamu sababu za kifo na kujiridhisha.

Lakini pia, uchunguzi huu huwasaidia madaktari kujifunza kutorudia makosa ya kitabibu au kujua kifo kilisababishwa na nini wakati wa matibabu. “Kwa mfano mtu aliyepata ajali akaumia kichwa, madaktari huangalia jeraha la kichwani  pekee. Hata hivyo, baadaye uchunguzi wa kifo huonyesha kuwa  utumbo wa marehemu ulipasuka na ndicho chanzo cha kifo, tunajiridhisha,” anasema.

Sheria na uchunguzi wa kifo

Kisheria, uchunguzi wa kifo cha marehemu unatakiwa kufanyika ndani ya saa 24 iwapo mgonjwa alikuwa akiugua maradhi kama malaria.

 “Iwapo mtu amefariki dunia halafu kuna daktari alikuwa akimwangalia, basi uchunguzi wake unatakiwa kufanyika ndani ya siku 14 na hapa si lazima kumpasua marehemu.

Kisheria, wiki mbili zikipita hata daktari aliyekuwa akimtibu hawezi kumfanyia ‘post- mortem’ kwani hana nguvu za kisheria kufanya hivyo,” anasema.

Wakili wa Kujitegemea wa Kampuni ya Kakamba and Partners, Mathew Kakamba anasema kisheria uchunguzi wa kifo husaidia kupata uthibitisho wa kina kuhusu chanzo au sababu ya kifo.

“Kama watu wanadai marehemu alinyweshwa sumu, basi ripoti ya post-mortem (uchunguzi baada ya kifo) huleta kithibitisho kama ni kweli ni sumu na ni sumu ya aina gani na imesababisha vipi kifo,” anasema

Anasema  ripoti hii huondoa utata.   Huweza kubadili mwelekeo  wa kesi.