Mfungwa akamatwa na SMG uraiani

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Philip Mangula

Jeshi la Polisi mkoani Simiyu, linamshikilia mkazi wa kijiji cha Ng’wang’wali, Wilaya ya Itilima, aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 15 gerezani akiwa na silaha ya kivita.

 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Salum Msangi, alimtaja mfungwa huyo aliyekamatwa juzi na silaha hiyo kuwa ni Masanja Maguzu (42).

Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, Maguzu alikamatwa na bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) ikiwa na risasi 31 nyumbani kwake.

Kamanda Msangi alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu jana kutoka wilayani Bariadi.

Alisema kwa mara ya kwanza Maguzu alikamatwa na bunduki aina ya SMG na risasi 622 mwaka 2010 na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Shinyanga na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 15 gerezani baada ya kupatikana na hatia.

Hata hivyo, alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida, jeshi hilo tena limemkamata mfungwa huyo akiwa uraiani.

Kamanda Msangi alisema mbali na bunduki, pia alikamatwa na magazini tatu na risasi 31 za SMG kinyume cha sheria.

Alisema bunduki hiyo anatuhumiwa kuifanyia vitendo vya kihalifu na ujangili katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la Akiba la Maswa.

Kamanda Msangi alisema jeshi lake linaendesha uchunguzi wa kina ili kufahamu mazingira yaliyosababisha mfungwa huyo kuwa nje ya gereza baada ya kuhukumiwa adhabu hiyo.

Alisema Novemba 6, mwaka huu, polisi walimkamata mke wa mfungwa huyo aliyetambuliwa kwa jina la Holo Mabuga (30), akiwa na silaha nyingine ya kivita aina ya G3.

Kamanda Msangi alisema silaha hiyo ilikamatwa ikiwa na risasi zake 36 pamoja na risasi nyingine zinazotumika katika bunduki aina ya SMG.

Siku 10 baada ya kukamatwa kwa mwanamke huyo, polisi walifanikiwa kumnasa mumewe, ambaye ni mfungwa aliyeaminika yumo gerezani akitumikia adhabu yake ya kifungo cha miaka 15 akiwa na silaha hiyo ya SMG na risasi 31 na magazini tatu; moja hutumika katika bunduki aina ya Uzi gun ya Kiisraeli.

“Jamani, tukio hili limetushitua na kutusikitisha sana. Maana wakati tukipambana na kukabiliana na vitendo vya uhalifu na wahalifu, bado kuna watu wengine wanakwamisha juhudi zetu sisi polisi. Mfungwa huyu kila mmoja hapa mkoani anaelewa kuwa yuko gerezani anatumikia adhabu yake.  Ajabu leo amekutwa tena uraiani akiendelea na vitendo vyake vile vile. Je, tutashindwa kulaumiwa kuwa tunakula na wahalifu?” Alihoji Kamanda Msangi na kuongeza:

“Haiwezekani mfungwa aliyehukumiwa kutumikia jela miaka 15 kwa muda mfupi hivi akawa nje hata kama ni kwa msamaha. Ni muda mfupi sana na hasa ikilinganishwa na kosa lenyewe. Maana ni la kupatikana na silaha tena ya kivita. Na iliyokuwa ikitumika kwa vitendo vya kijambazi na ujangili ndani ya hifadhi, hii inaonyesha kuna namna imefanyika. Na sisi tunaendelea kuchunguza kujua ukweli wa jambo hili.”

Alisema inawezekana mfungwa huyo alitoka gerezani katika mazingira ya kutatanisha, lakini bado aliendelea kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwa kutumia silaha za kivita, kinyume cha sheria na mitego ya polisi ilifanikiwa kumnasa baada ya kumkamata mkewe, ambaye pia alikutwa akiwa na silaha nzito za kivita.

Alisema uchunguzi wa awali wa polisi ulibaini kuwa mke wa mfungwa huyo, Holo Mabuga, pamoja na kupatikana akiwa na silaha hizo za kivita kinyume cha sheria, hakuwa peke yake katika matumizi ya silaha hizo, bali nyuma yake kulikuwa na kundi la watu aliokuwa akishirikiana nao.

Kamanda Msangi alisema kupatikana kwa magazini ya Uzi gun, kunathibitisha kwamba, bunduki yake, ambayo matumizi yake ni sawa ya SMG, bado iko mikononi mwa mtandao wa wahalifu na watu wabaya.

Alisema kama haitapatikana haraka itaendelea kusumbua wananchi na kuhatarisha usalama wa maisha na mali zao na hata wanyama katika hifadhi za wanyamapori.

NIPASHE iliwasiliana kwa njia ya simu jana na Msemaji wa Jeshi la Magereza nchini, Omary Mtiga, kutaka aeleze mfungwa huyo aliondokaje gerezani na kurudi uraiani lakini alisema hakuwa na taarifa hizo.

“Mimi sina taarifa. Niandikie meseji (ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) ili nifuatilie huko Simiyu kujua ni gereza gani alilokuwa akitumikia kifungo hicho,” alisema Mtiga.

Naye Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, aliomba apewe kufuatilia suala hilo.

 “Nami nitafuatilia kesho (leo) kujua kulikoni,” alisema Nantanga.

No comments:

Post a Comment