Ajali yaua wanane, yajeruhi 47

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma

Watu wanane wamekufa na wengine zaidi ya 47 kujeruhiwa vibaya baada ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso katika barabara kuu ya Mwanza-Musoma, Wilaya Bunda mkoani Mara.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alithibisha kutokea kwa ajali hiyo juzi saa 11.00 jioni katika kijiji cha Nyatwali, karibu na mpaka wa Wilaya ya Bunda na mji mdogo wa Lamadi wilaya ya Busega, mkoani Simiyu.


Kamanda Mwakyoma alisema kuwa mabasi hayo ya Mwanza Coach lenye namba za usajili T. 736 AWJ na Best Line lenye namba za usajili 535 AJR yaligongana kutokana na kuendeshwa kwa mwendo kasi.


Alisema kuwa basi la Mwanza Coach lilikuwa linatokea mjini Musoma mkoani

Mara, likielekea jijini Mwanza wakati Best Line lilikuwa linatokea jijini Mwanza likielekea Sirari, wilayani Tarime, mkoani Mara.


Kamanda Mwakyoma alisema kuwa watu sita walikufa papo hapo na wengine wawili baada ya kufikishwa katika hospitali ya DDH-Bunda kwa matibabu. Madereva wa mabasi hayo ambao bado majina yao hayajafahamika walitoroka baada ya ajali hiyo kutokea.


“Chanzo cha ajali hii ni uzembe wa madereva wote wawili, maana tunaambiwa na majeruhi pamoja na abiria ambao walinusurika kuwa walikuwa katika mwendo kasi…nitumie fursa hii kuwaambia madereva kwamba wajali roho za watu wanaowabeba, hatutasita kuwachukulia hatua madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani,” alisema.


Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tuppa, alifika katika eneo la tukio kisha kuwasalimia majeruhi katika hospitali ya DDH-Bunda na kuagiza vifaa vya tiba viongezwe hospitalini hapo kutoka Hospitali ya Mkoa wa Mara mjini Musoma. Tuppa pia aliagiza majeruhi wote wenye hali mbaya wapelekwe kwenye hosptali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, aliyefika mapema katika eneo la tukio, alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni madereva wa mabasi hayo kutokuwa makini kutokana na barabara hiyo ambayo inakarabatiwa na kampuni ya Kichina kuwa na vumbi jingi.


Mirumbe alisema kuwa magari ya watu binafsi na magari ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, yalifika katika eneo la tukio na kubeba majeruhi na kuwapeleka hospitani na kwamba mizigo yao iliyokuwa kwenye mabasi hayo imehifadhiwa kituo cha Polisi Bunda.


Aidha, Mirumbe akiwa katika Hospitali ya DDH-Bunda aliambiwa na Daktari Kiongozi wa hospitali hiyo, Dk. Christian Kudilli, kwamba wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya tiba pamoja na damu, na aliwataka wanachi kujitokeza kuchangia ili kuokoa maisha ya majeruhi hao.


Baadhi ya abiria walionusurika, Joseph Mnyaga, mkazi wa Musoma pamoja na mwanakwaya wa Kanisa la African Inland Church  (AIC), Yombe  Mitron, waliokuwa wanatoka Mwanza kurekodi nyimbo, walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi.


Aidha, majeruhi wa ajali hizo walisema kabla magari yao kupata ajali waliwaambia madereva kupunguza mwendo kutokana na vumbi kuwa jingi katika barabara hiyo, lakini madereva hao walikaidi.


 “Kabla ya ajali kutokea, sisi tulimwambia dereva wa basi letu la Mwanza Coach kwamba punguza mwendo, lakini hakusikia, vumbi lilikuwa jingi na tulikuwa hatuoni mbele,” alisema abiria mmoja, ambaye alijeruhiwa kichwani.


Idadi ya vifo hivyo ilitolewa na jeshi la polisi imetofautiana nay a Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Rainer Kapinga, akisema waliokufa ni saba.


Dk. Kapinga  alisema kuwa walipokea miili ya watu sita waliokufa katika eneo la tukio wakiwamo wanawake watatu na wanaume watatu na kwamba majeruhi wengine wawili.


Alisema majeruhi mwingine ambaye ni mwanaume alikufa baada ya kufikishwa hospitalini hapo.

Dk. Kapinga alisema majeruhi waliopokelewa hospitalini hapo ni 47 na kwamba wanane kati yao wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, kutokana na hali zao kuwa mbaya na kuongeza kuwa hali za majeruhi walioko katika Hospitali ya DDH-Bunda zinaendelea vizuri.


Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya DDH-Bunda na kuongeza kuwa miili minne tayari imetambuliwa na ndugu zao. Aliwataja marehemu waliotambuliwa kuwa ni Amina Juma (35), mkazi wa jijini Mwanza; Grace Mlimwa (50), mkazi wa Bunda na Magori Ibrahimu (23), mkazi wa kijiji cha Bitaraguru wilayani Bunda.


Hata hivyo, Dk. Kapinga alisema kuwa hospitali hiyo inakabiliwa na vifaa tiba pamoja na upungufu mkubwa wa damu, hali ambayo ilisababisha baadhi ya wananchi kuanza zoezi la kuchangia damu baada ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mirumbe, kuwaomba kufanya hivyo.


Ajali hiyo imetokea zikiwa ni siku chache baada ya ajali nyingine kutokea wilayani Magu mkoani Mwanza, ambayo ililihusisha basi la kampuni ya Bunda Express, ambalo wiki iliyopita liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine 22.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment