Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetangaza
matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Pili mwaka 2012, yanayoonyesha kuwa
wanafunzi 136,923 kati ya 386,271 waliofanya mtihani huo wamefeli.
Katika matokeo hayo shule kumi zilizofanya
vibaya zote ni za Serikali, zikitoka Mikoa ya Kusini. Wanafunzi kumi
bora wakitoka katika shule binafsi na taasisi za dini, ambapo Mkoa wa
Dar es Salaam ukiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliofeli.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam
jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo alisema
idadi ya waliofeli ni sawa na asilimia 35.5, wakiwamo wasichana 74,020
na wavulana 62,903, kwamba waliofaulu ni wanafunzi 245.9,32
Hata hivyo, alisema kuwa wanafunzi waliofeli
watarudia kidato cha pili na watapewa fursa nyingine ya kurudia mtihani
huo na iwapo watafeli tena watarejeshwa nyumbani.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Shule za St
Francis ya mkoani Mbeya na Kaizirege ya Bukoba, mkoani Kagera zimetoa
wanafunzi kumi bora, kati ya hao mwanafunzi wa tatu na nne pekee
wakitoka Sekondari ya Kaizirege na waliobaki ni St Francis.
“Wizara imeamua wanafunzi hawa warudie tena
kidato cha pili na watajiunga na wenzao wanaoingia kidato cha pili
mwaka huu kuendelea nao kidato cha tatu mwakani, hivyo basi nawaomba
wazazi wawape ushirikiano wa kutosha ili wajisijione wapweke hatimaye
wakakata tamaa ya kusoma,” alisema Mulugo.
Hata hivyo, alisema kuwa matokeo hayo
yanaonyesha kuwa katika mwaka huu, kiwango cha ufaulu kimepanda kutoka
asilimia 45.4 ya mwaka 2011 na kufikia asilimia 64.5 mwaka huu ambapo
watahiniwa 249,325 wataendelea na masomo ya kidato cha tatu.
“Wanafunzi waliofaulu ni sawa na asilimia
64.55 ambapo kati yao wasichana ni 133,213 na wavulana ni 136,122,”
alisema Mulugo na kuongeza:
“Waliopata alama A, B na C walikuwa 127,981 na
waliopata kiwango cha chini ya hapo ni 121,344, alama ya juu ya ufaulu
ni asilimia 92.”
Alisema wanafunzi wote waliofanya mtihani huo, wasichana ni 187,244 na wavulana ni 199,027.
Kusini hoi
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa
shule za Serikali zilizofanya vibaya na kushika nafasi 10 za mwisho
zinatoka Kanda ya Kusini. Alizitaja shule hizo kuwa ni ya Mihambwe,
Diduma, Kiromba, Marambo, Mbembaleo, Kinjumbi, Litupi, Luagala, Miguruwe
na Napacho.
Matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa shule zisizo
za Serikali zilizofanya vibaya mbili zinatoka Kanda ya Kusini, tano
kanda ya Mashariki na mbili Kanda ya Kati. Shule hizo ni Mfuru, Pwani,
Doreta, Kigurunyembe, Ruruma, At-taaun, Jabal Hira Seminari, Mkono wa
Mara, Kilepile na Kiuma. Alisema kutokana na shule nyingi za Kusini
kufanya vibaya, Serikali inaangalia uwezekano wa kupeleka walimu zaidi.
Kwa mujibu wa Mulugo, Mkoa wa Dar es Salaam
unaongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi waliofeli mtihani huo, licha ya
kuwa na walimu wa kutosha tofauti na mikoa ya Kusini.
Kumi bora za Serikali
Shule zilizofanya vizuri za Serikali ni
Mzumbe (Morogoro), Tabora, Ilboru (Arusha), Kibaha (Pwani), Iyunga
(Mbeya), Msalato (Dodoma), Malangali (Iringa), Ifunda Ufundi (Iringa),
Samora Michael (Iringa) na Kilakala (Morogoro).
Kwa Upande wa shule za binafsi zilizofanya
vizuri ni Kaizirege (Bukoba), Marian Wavulana (Pwani), St. Francis
(Mbeya), Don Bosco (Moshi), Bethel Sabs, Marian Wasichana (Pwani), Don
Bosco (Moshi), St Joseph Iterambogo Seminari, Canossa (Dar es Salaam) na
Carmel.
Wanafunzi bora
Wanafunzi kumi waliofanya
vizuri ni kutoka shule za binafsi na walioshika nafasi mbili za mwanzo
ni wasichana kutoka Shule ya St Francis (Mbeya), ambapo wa kwanza ni
Magreth Kakoko akifuatiwa na Queen Masiko.
Hata hivyo, baadaye taarifa kutoka Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi zilieleza kuwa majina hayo yana kasoro na
itatoa taarifa na orodha sahihi baadaye. Kabla ya taarifa hiyo, Mulugo
alibainisha kuwa wanafunzi wote kumi bora wanatoka katika shule mbili
tu, St Francis na Kaizirege (Bukoba) na kwamba nafasi ya tatu na ya nne
imeshikwa na wanafunzi kutoka Kaizirege ambao ni Lukundo Manase na Frank
Nyantarila.
Nafasi ya tano hadi ya nane imechukuliwa na
wanafunzi kutoka St Francis ambao ni Grace Msovella, Harieth Makirie,
Robinnancy Mtitu na Humrath Lusheke.
Nafasi ya tisa na kumi ikachukuliwa na wanafunzi kutoka Kaizirege ambao ni Mukhusin Hamza na Anastazia Kabelinde.
No comments:
Post a Comment