Polisi watumia nguvu kuzuia maiti kusafirishwa Geita

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Leonard Paulo alikuwapo wakati askari wake walipoingilia msafara huo na kusababisha vurumai kubwa.
Waombolezaji hao walikuwa wakiuhamisha mwili wa marehemu Fungungu kutoka Hospitali ya Runzewa kuupeleka katika Hospitali ya Geita.


Sakata hilo la ndugu na polisi lililotokea saa nane mchana juzi Jumamosi katika Pori la Samina, Geita na polisi wakiwa kwenye magari matatu wakiwa wamesheheni silaha mbalimbali walifika na kuzuia mwili wa marehemu kusafirishwa.


Baadhi ya ndugu wa marehemu akiwamo mkewe, wanadai kwamba Fungungu alifariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi wanaosemekana kwamba walimvamia nyumbani kwake usiku wa kuamkia Alhamisi iliyopita kisha kupora mamilioni ya fedha. Wanadai kwamba alipigwa risasi tumboni na kichwani katika Kijiji cha Runzewe, Wilaya ya Bukombe mkoani hapa.


Katika tukio hilo inadaiwa kuwa kiasi cha Sh360 milioni kiliporwa. Kati ya fedha hizo, Sh60 milioni zinadaiwa kwamba zilikuwa kwenye gari wakati Sh300 milioni zilikuwa kwenye masanduku mawili yaliyokuwa ndani ya nyumba.


Pia ndugu hao walidai kwamba Sh1.2 milioni zilichukuliwa na askari wawili wa kiume baada ya kumpekua mke wa marehemu kwenye nguo za ndani.


Pia askari hao wanadaiwa kupora mali mbalimbali za marehemu zikiwamo redio mbili, video kamera moja, nguo za marehemu ikiwamo kanzu, mashine ya printer, mashine ya inventor, karatasi za picha, deki mbili za kucheza CD, pamoja na nguo za mke wa marehemu.


Mapema Kamanda Paulo alikuwa ameeleza kuwa marehemu alijiua mwenyewe baada ya kumjeruhi Polisi, Fortunatus Beatus kwa risasi lakini taarifa hizo zimepingwa vikali na ndugu na jamaa wa marehemu ambao wanadai marehemu aliuawa na polisi akiwa nyumbani kwake.

Polisi kuzuia waombolezaji

Baada ya polisi kuyasimamisha magari manane yaliyokuwa katika msafara huo wa kupeleka mwili wa marehemu kwenda kuhifadhiwa katika chumba cha maiti Hospitali ya Geita, kulizuka mabishano makali kati ya Kamanda Paulo na ndugu wa marehemu.


Inadaiwa kwamba polisi walikuwa wakishinikiza mwili huo urejeshwe Runzewe, Bukombe kwa kuwa tayari ulikuwa umefanyiwa uchunguzi jambo ambalo liliwakera waombolezaji hao.


Kabla ya kamanda huyo kufika eneo hilo, msafara huo ulisimamishwa na Polisi wa Usalama Barabarani ambao walikuwa wamefuatana na wale wa Kutuliza Ghasia (FFU), wakiongozwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita, Leonard Makona.
Baada ya kuusimamisha msafara huo, Makona aliwataka ndugu wa marehemu kumsubiri Kamanda Paulo ambaye alifika baada ya takriban dakika 10.


Mwandishi wa habari hii ambaye alikuwa katika eneo la tukio, alishuhudia ndugu wa marehemu na Kamanda Paulo wakirushiana maneno.


“Mnapeleka wapi mwili wa marehemu, ina maana hamkuridhika na uchunguzi wa daktari wa Bukombe?” alihoji kwa ukali na kujibiwa pia kwa ukali na kaka wa marehemu, Mariatabu Fungungu: “Kwa nini mnatusimamisha? Tunaomba tuite waandishi wa habari hapa ili waje washuhudie tukio hili. Kwa nini msikae ofisini?”

 Baadaye, kamanda huyo aliwaamuru askari wake kuwaingiza katika gari la polisi ndugu watano wa marehemu wakiwamo mke wa marehemu, Lucia Kilaza (23) na Mariatabu. Walifanya hivyo kwa kutumia nguvu na kisha kuondoka nao hadi katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita.


Ndugu wa marehemu walilalamikia kitendo hicho wakisema kilikuwa na lengo la kuficha ukweli wa tukio hilo.

Mke wa marehemu

Kilaza alidai kuwa kifo cha mumewe kilitokea baada ya zaidi askari 20 kuvamia nyumbani kwake yapata saa tisa usiku na kumwamuru Fungungu kutoka nje na alipogoma, ndipo walipoanza kupiga risasi na kuvunja vioo vya madirisha na milango na risasi kumpata marehemu. Pia alidai kuwa walipiga mabomu ya machozi.


Alisema baada ya tukio hilo, walivunja mlango na kuingia ndani kisha kumchukua mumewe ambaye tayari alikuwa amefariki na kumtupa nje... “Mimi pia walinichukua wakanitupa nje ya uzio baadaye wakaanza kunipekua nguo za ndani na kuchukua Sh1.2 milioni ambazo nilikuwa nimezificha baada ya kuona wameanza kufyatua risasi.”


Wakizungumzia tukio hilo, Mbunge wa Bukombe, Profesa Kalikoyela Kahigi na Diwani wa Runzewe, Yusufu Fungameza walisema Serikali inatakiwa kuingilia kati suala hilo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika katika tukio.


Alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, Kamanda Paulo aliwaahidi waandishi wa habari kwamba angelitolea ufafanuzi jana Jumatatu. Hata hivyo, alishindwa kufanya hivyo kwa madai kwamba anapisha kwanza uchunguzi wa mwili wa marehemu kwenye Hospitali ya Geita.


Ndugu wa marehemu wamegoma kuuzika mwili wa marehemu wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike kwa kutumia jopo maalumu la madaktari huku wakiitaka Serikali kuunda tume kuchunguza tukio hilo.

Mtandao wa ujambazi Mbeya

Katika hatua nyingine; Watu wanaodaiwa kujihusisha na matukio ya uhalifu katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Morogoro na Dar es Salaam wamenaswa na polisi huko Mbeya.
Mtandao huo unadaiwa kuwahusisha askari mmoja wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) pamoja na wafanyabiashara maarufu wa Mbeya.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alisema jana kuwa watu 29 wanaodaiwa kujihusisha na mtandao huo wanashikiliwa na jeshi hilo.


“Askari hao mbali na kujihusisha na matukio ya ujambazi moja kwa moja, pia walikuwa na tabia ya kuwaazima majambazi sare za jeshi ambazo zilikuwa zikitumika kwenye matukio mbalimbali ya uhalifu,” alisema.


Alisema watuhumiwa wote hao wanakabiliwa na tuhuma za mauaji, ujambazi na kupokea mali za wizi na walikamatwa katika maeneo ya Mkwajuni, Chunya na Makambako na Mafinga, Iringa.


Kamanda Athumani alisema kuwa watuhumiwa 13 watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ujambazi, mauaji na kupokea mali za wizi, wengine saba watasafirishwa kwenda Iringa ambako ndiko watakakofikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.


Kamanda Athumani alisema uchunguzi wa watuhumiwa wengine 16 bado unaendelea na wataachiwa kwa dhamana na watatakiwa kuripoti vituo vya polisi watakavyopangiwa.

No comments:

Post a Comment