Nchimbi atimua mabosi sita polisi, makuruta 95

 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi amewafukuza kazi maofisa watano wa Polisi na kumsimamisha kazi kwa mwezi mmoja Kamishna msaidizi Mwandamizi wa jeshi hilo kutokana na makosa mbalimbali.

Pia, Dk Nchimbi amewafukuza makuruta 95 waliokuwa Chuo Cha Polisi (CCP), Moshi kutokana na kugundulika kutumia rushwa kupata ajira.

Kamishna msaidizi Mwandamizi wa Polisi aliyesimamishwa kwa mwezi mmoja ni Renatus Chalamila akihusishwa na rushwa katika kuajiri.

Alisema taarifa za uchunguzi za kamishna huyo, ambaye anashughulikia masuala ya ajira zimewasilishwa kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kumfukuza kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Nchimbi alisema maofisa watatu kati ya hao watano wamefukuzwa kutokana na kugundulika kuwa walikamata dawa za kulevya aina ya cocaine lakini zilipopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali alidai zilikuwa ni chumvi na sukari.

“Kama mtakumbuka mkoani Mbeya, Aprili mwaka jana zilikamatwa kilo 1.9 za dawa za kulevya na polisi walithibitisha hilo lakini zilipopelekwa kwa Mkemia Mkuu zikagundulika ni chumvi na sukari,” alisema na kuongeza:
“Niliunda timu kuchunguza kama ni kweli kwa kuwa askari walituthibitishia ni dawa za kulevya, timu ilichunguza na kugundua kilichokamatwa hakikuwa kilichopelekwa kwa Mkemia Mkuu.”

Dk Nchimbi alisema kutokana na hilo, amewafukuza kazi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Peter Elias ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya, Mrakibu wa Polisi, Jacob Kiango aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi mkoani humo na Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Charles Kinyongo aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia mkoani humo.

“Nimemwagiza kiongozi wa polisi awafungulie mashtaka ya kijeshi askari hawa kwani ajira zao zimesitishwa kuanzia jana (juzi Jumamosi),” alisema Dk Nchimbi.

Alisema ofisa mwingine aliyefukuzwa kazi kuanzia jana ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Peter Matagi aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kagera kwa kuwapiga na kuwabambikizia kesi zisizo na dhamana wananchi.

“Mwaka jana kulikuwa na mgogoro wa ardhi katika Kijiji cha Nyakasimbi huko Kagera kati ya wanakijiji na mmiliki mmoja wa shamba, wananchi waliona kuwa mmiliki wa shamba hilo ana eneo kubwa hivyo walikubaliana katika mkutano wa kijiji kuingia kwenye shamba hilo kwa nguvu,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:

“Waliingia na kuanza kuswaga ng’ombe kuelekea kwa Mkuu wa Wilaya, walikamatwa watu 12 lakini wawili walifanikiwa kutoroka na walisafiri hadi Dodoma kumwona mbunge wao, ambaye aliomba kuonana na mimi.”

Dk Nchimbi alisema licha ya kukubali kuonana nao,  ilishindikana baada ya watu hao kukamatwa wakidaiwa kuwa ni majambazi ambao walikuwa wakitafutwa huko Karagwe.
“Nilimpigia simu Kamanda wa Polisi Kagera nikitaka kuonana na hao majambazi katika Hoteli ya Dodoma na waliletwa na niliwasikiliza na kugundua kuna tatizo la wao kubambikiziwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha ambayo huwa haina dhamana,” alisema.

Alisema aliunda timu ambayo aliiongoza akiwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Aggrey Mwanri na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye na kusimamia uchunguzi na Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali iligundua hakuna mashtaka kama hayo na ndiyo maana Matagi anafukuzwa kazi na kushtakiwa kijeshi.

No comments:

Post a Comment