Usiyoyajua kuhusu uchunguzi wa miili ya maiti nchini Tanzania

Selemani Uliza akionyesha kitanda cha kusafishia na kuchunguza miili ya marehemu.

Maiti ya Adrian Louis iliokotwa kando ya barabara kuu ya kwenda Lukuledi wilayani Masasi katika Mkoa wa Mtwara.

Haikuwa na jeraha lolote. Ndugu zake walipopata taarifa za msiba, waliuchukua mwili na kuusitiri harakaharaka.

Hawakuwa na wasiwasi wowote wa kutaka kujua chanzo cha kifo cha ndugu yao kwani waliamini kuwa amefariki dunia kwa sababu ya kuzidiwa na ulevi, kwa kuwa siku zote alikuwa mlevi kupindukia. Kumbe, walikuwa wamekosea, kwani siku hiyo Louis hakuwa amelewa, bali kifo chake kilisababishwa na majambazi waliompora fedha kabla ya kumnyonga  hadi kufa.

Yapo matukio mengi ya namna hiyo katika sehemu mbalimbali nchini, lakini mengi kati ya hayo hayafanyiwi uchunguzi wa kujua chanzo.

Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa Magonjwa na Kiongozi wa Idara ya Uchunguzi wa Vifo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Innocent Mosha anasema ni muhimu kufanya uchunguzi wa sababu za kifo ili kujiondolea shaka au wasiwasi wa kipi kilisababisha kifo hicho.

Dk. Mosha anaelezea maana ya uchunguzi wa kifo na kusema kuwa ni  kitendo cha madaktari kutafuta chanzo kilichosababisha kifo cha mtu na kujiridhisha au ndugu kuridhika pasipo shaka.

“Watanzania walio wengi bado hawafahamu umuhimu wa kufanya uchunguzi wa vifo vya ndugu zao, jambo ambalo linasababisha wakati mwingine kupoteza ushahidi au kukosa  cheti cha kifo ambacho kina umuhimu mkubwa katika masuala ya mirathi,” anasema Dk Mosha

Anasema uchunguzi wa kifo si kwa ajili ya polisi wa upelelezi tu, bali ni mchakato unaotakiwa kufanywa  na ndugu wa marehemu ili kujiridhisha na sababu ya kifo cha ndugu yao.

Anaongeza kuwa tatizo kubwa hapa nchini ni kuwa watu wengi hawaelewi maana na umuhimu wa kuchunguza miili ya ndugu zao ili kujua chanzo au sababu za vifo vyao.

Mchakato wa Uchunguzi

 Kwanza, Dk. Mosha anasema uchunguzi wa kifo kwa matukio yanayohusisha polisi, huhitaji taarifa ya utangulizi ambapo polisi hutakiwa kutoa maelezo ya awali kuhusu marehemu.

Anasema pia kuwa katika matukio hayo, ndugu zaidi ya mmoja  huhitajika kwa ajili ya kumtambua marehemu,  sanjari  na kujaza fomu ya maelezo mafupi. “Baada ya polisi kutoa maelezo yao ambayo kwa kawaida huwa ni mafupi, daktari huendelea na uchunguzi wake kulingana na ujuzi wake,” anasema.

 Anaeleza kuwa zipo hatua kadhaa za kufanya uchunguzi wa kifo ambazo  hazina budi kufuatwa. Anazitaja kuwa marehemu huchunguzwa  sehemu za nje za mwili akiwa na nguo zake.

“Hapo daktari huangalia mazingira ya nje, kwa mfano nguo alizovaa; iwapo zina damu; damu imeingiaje, kama zimechanika  na zilikuwa katika mazingira gani. Utambuzi huu wa awali wakati marehemu amevaa nguo zake, huweza kutuonyesha mazingira ya nje iwapo kulikuwa na purukushani kabla ya kifo au la,” anasema.

Baada ya hapo, Dk. Mosha anasema daktari hutakiwa kwenda hatua ya pili ya kuchunguza ndani ya mwili ambapo mwili wa marehemu huchunguzwa kwa umakini mkubwa kama kuna chochote kitakachoashiria sababu ya kifo chake.

 Kwa mfano, Dk. Mosha anasema majeraha ya mwili huangaliwa, pia mazingira ya majeraha hayo.

Anaongeza kuwa hapo daktari anaweza kujua iwapo marehemu alipigwa alizama majini, alikunywa maji mengi au  kuzamishwa majini.

“Kama mtu amezama majini ni rahisi kujua kwani macho yake huwa na mshipa midogo midogo iliyovilia damu. Mwingine huwa na kitu kinachoitwa ‘Perypheral discoloration’ ambapo  kisigino cha marehemu huwa na rangi ya bluu kwa sababu ya kukosa hewa ya oksijeni.” Mtaalamu huyo anasema wakati mwingine uchunguzi wa vifo hivi ni  muhimu kwani husaidia kujua iwapo mtu amefia majini au aliuawa, kisha akatupwa kwenye maji.

Uchunguzi wa mwingine wa vifo vya marehemu huweza kuhusisha kumpasua mwili na kisha kuangalia ogani kama ini, figo, mishipa ya damu, utumbo na kifua.

 Pia, mwili wa marehemu huangaliwa kama kuna uvimbe usoni, mapafu kujaa maji na wakati mwingine mapafu hutolewa na kupimwa kama yameingia maji na maji hayo ni ya aina gani.

 Kuna watu wanaofariki wanaodhaniwa kuwa wamejinyonga kuna utaalamu wa kuangalia kama kweli wamejinyonga au walinyongwa na kutundikwa.

Anasema uchunguzi wa kifo cha marehemu si lazima kuukatakata mwili,  bali wakati mwingine  wataalamu wanaweza kuchukua maelezo au kukata  sehemu ndogo tu ya mwili huo.

“Wakati mwingine iwapo mgonjwa amefariki dunia kwa kuugua malaria au aliletwa hospitali akiwa anaumwa ugonjwa huo na kama amekufa, basi ili kuthibitisha sababu ya kifo hicho, tunaweza kukata tishu kuangalia dalili za malaria katika mwili, kuangalia rangi ya manjano katika macho au wakati mwingine kipande cha ini kinachunguzwa,” anasema.

Gharama za uchunguzi

Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi wa Muhimbili, Dk.  Praxeda Ogweyo anasema  gharama za uchunguzi kwa watu wa kawaida ni  Sh200,000, lakini kwa raia wa kigeni ni 800,000. Anasema kwa madaktari wanaotaka kufanya uchunguzi wa vifo kwa sababu za kitaaluma hawatozwi gharama zozote na kwa polisi gharama zao hulipwa na serikali.

Dk. Ogweyo anasema ni wakati kwa Watanzania kujifunza na kuujua umuhimu wa uchunguzi wa vifo vya ndugu zao kwa kuwa husaidia kusuluhisha migogoro ndani ya familia.

“Kama ndugu wanahisi  kuwa kifo cha ndugu yao kina utata basi uchunguzi unasaidia. Mara nyingi mtu anapofariki ghafla huleta utata kwa jamii,” anasema

Dhana au mazoea

Dk. Mosha anasema kuna dhana zilizozoeleka kuwa  kama mtu ameuawa, basi sura ya muuaji huonekana kwenye macho ya marehemu, lakini anasema  hilo halina ukweli kwani kinachoonekana machoni ni kuvilia kwa damu au kuvimba kwa macho kwa sababu kama za kunyongwa.

Takwimu za uchunguzi

Kuhusu hilo, Dk. Mosha anasema  Watanzania wengi hawafanyi uchunguzi wa vifo vya marehemu ndugu zao kwa sababu ya dhana potofu kuwa ndugu zao hukatwakatwa au kuibiwa baadhi ya viungo. “Wengi wanaochunguza vifo vya marehemu ni polisi kwa sababu za kipolisi na madaktari kwa sababu za kitaaluma. Lakini watu wa kawaida bado hawana uelewa kuhusu uchunguzi wa vifo.”  Kwa mfano, takwimu za  hapa Muhimbili zinaonyesha kuwa uchunguzi wa vifo vya marehemu unaofanywa kwa maombi ya ndugu ni watu wawili hadi wa tatu kwa mwezi wakati uchunguzi unaofanywa kwa maombi ya polisi ni matukio sita hadi saba kwa wiki.

Sababu za kuchunguza miili

 Dk. Mosha anasema, uchunguzi wa miili ya marehemu una umuhimu mkubwa katika kufahamu sababu za kifo na kujiridhisha.

Lakini pia, uchunguzi huu huwasaidia madaktari kujifunza kutorudia makosa ya kitabibu au kujua kifo kilisababishwa na nini wakati wa matibabu. “Kwa mfano mtu aliyepata ajali akaumia kichwa, madaktari huangalia jeraha la kichwani  pekee. Hata hivyo, baadaye uchunguzi wa kifo huonyesha kuwa  utumbo wa marehemu ulipasuka na ndicho chanzo cha kifo, tunajiridhisha,” anasema.

Sheria na uchunguzi wa kifo

Kisheria, uchunguzi wa kifo cha marehemu unatakiwa kufanyika ndani ya saa 24 iwapo mgonjwa alikuwa akiugua maradhi kama malaria.

 “Iwapo mtu amefariki dunia halafu kuna daktari alikuwa akimwangalia, basi uchunguzi wake unatakiwa kufanyika ndani ya siku 14 na hapa si lazima kumpasua marehemu.

Kisheria, wiki mbili zikipita hata daktari aliyekuwa akimtibu hawezi kumfanyia ‘post- mortem’ kwani hana nguvu za kisheria kufanya hivyo,” anasema.

Wakili wa Kujitegemea wa Kampuni ya Kakamba and Partners, Mathew Kakamba anasema kisheria uchunguzi wa kifo husaidia kupata uthibitisho wa kina kuhusu chanzo au sababu ya kifo.

“Kama watu wanadai marehemu alinyweshwa sumu, basi ripoti ya post-mortem (uchunguzi baada ya kifo) huleta kithibitisho kama ni kweli ni sumu na ni sumu ya aina gani na imesababisha vipi kifo,” anasema

Anasema  ripoti hii huondoa utata.   Huweza kubadili mwelekeo  wa kesi.

No comments:

Post a Comment