Wazanzibari waishio Tanganyika wapinga kugawanywa

Rais Jakaya Kikwete

Jumuiya ya Wazanzibari Waishio Tanganyika imekuja juu ikipinga vikali mikakati ya kuwabagua inayolenga kuwatisha ili kuwarudisha nyuma wasiendelee kudai mamlaka kamili ya Zanzibar pamoja na Muungano wa haki na wenye maslahi kwa pande zote mbili.

Mikakati hiyo inadaiwa kufanywa na watu wa kubuni wanaojiita Umoja wa Wapemba Waishio Tanzania Bara (Neppelta) kwa kutumia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba, Machi 21, mwaka huu.

Tamko la jumuiya hiyo lilitolewa na Mwenyekiti wake, Abdallah Mohammed Kassim, marufu kama “Dullah”, jijini Dar es Salaam juzi.

Alisema kauli ya watu hao, ambayo ilinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni, imeonyesha ubaguzi wa dhahiri dhidi ya Wazanzibari, ambao kiasili ni wamoja licha ya kutenganishwa na bahari.

Abdallah alisema hawakubaliani na kauli ya watu hao iliyosisitiza kuwa wao ni “Wapemba” kwa kuwa Zanzibar ni moja na maslahi yake ni ya wote.

“Kitendo cha kusisitiza kuwa Muungano ukivunjika watakaopata hasara ni Wapemba ni ubaguzi kwani Wapemba ni Wazanzibar hivyo kuwabagua ni kujenga chuki miongoni mwa raia wa visiwa hivyo viwili ambao ni wananchi wa nchi moja,” alisema Abdallah.

Alisema Muungano uliopo ni wa nchi mbili, ambazo ni Tanganyika na Zanzibar na kwamba, Zanzibar ni visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo kuendelea kuwabagua Wapemba kwa maneno na vitendo ni kutowatendea haki.

Abdallah alisema uamuzi wa Wazanzibari kuishi na kufanya kazi Tanganyika ni haki yao ya msingi, hivyo kuwajengea hofu ni kuwanyima haki hiyo na kuwafanya waishi kwa mashaka makubwa, kitu ambacho alisema siyo kizuri kwa raia.

“Jumuiya ya Wazanzibari tunaoishi Tanganyika tunauliza kauli iliyotolewa na bwana Shehe Haji Faki ambaye alijitambulisha kama Mwenyekiti wa Wapemba waishio Bara kwa kusema idadi ya Wapemba waishio Bara imeongezeka hadi kufikia zaidi ya watu 800,000 mwaka 2012 na mtaji wa trilioni 1.2, takwimu hizi amezipata wapi?” alihoji Abdallah.

Alisema uhusiano na mwingiliano baina ya Wazanzibari na Watanganyika vilikuwapo kabla ya Muungano wa mwaka 1964.

Hivyo, akasema kuishi katika nchi yoyote duniani hakutegemei Muungano, kwani wapo Watanzania wanaishi nchi mbalimbali duniani bila ubaguzi na hata Tanzania wapo raia wengi wa kigeni wanaoishi licha ya kuwa nchi hizo hawajaungana nazo.

“Wazanzibari waliopo Tanganyika na kumiliki ardhi na mali isiwe sababu ya kuwatisha na kuwajengea hofu ya kudai maslahi ya nchi yao, kwani utaifa wa mtu hauwezi kutupwa kwa sababu ya kumiliki ardhi, mali, kuoa au kuolewa,” alisema Abdallah.

Alisema umoja uliopo miongoni mwa Watanzania unakumbusha kuwa wanaofaidika na Muungano siyo Wazanzibari pekee, kwani faida hizo zipo kwa raia wa pande zote mbili za Muungano.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment