Busara ya Ukawa sasa inahitajika

Rasimu ya Katiba imesheheni mambo mengi muhimu, yanayohitajika kwa wakati tulionao. Ikiwa yatakosekana kupatikana mwakani, anaweza akatokea rais mkorofi, asiyeambilika wala kushaurika akasema hana mpango wa kuunda katiba mpya hadi miaka 50 mingine ipite na kuiona iliopo inafaa na kukidhi haja.PICHA|MAKTABA 
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi


Sauti za viongozi wa kisiasa, kiserikali na madhehebu ya dini kuwaasa na kuwasihi Ukawa warejee bungeni zimesikika, kazi sasa ni kwa wajumbe wa kundi hilo kuitikia wito huo au kuziba masikio.

Matamshi ya viongozi hao kwa nyakati tofauti, yameeleza wazi na kuwataka wabunge hao kutengua misimamo yao na kurejea bungeni ili kuchuana, kushindana kwa hoja na kukosoana wakiwa ndani ya Bunge, si nje ya chombo hicho cha kikatiba na kisheria au kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima.

Viongozi hao kwa nyakati tofauti, wameeleza kuwa itakuwa busara ikiwa upande wa wabunge waliobaki ndani ya Bunge na wale waliotoka nje, wakakaa pamoja kwa kuzitumia kamati ya mashauriano, iliyopo.

Miongoni mwa viongozi waliotoa wito wa kuwataka Ukawa warejee bungeni ni Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk Hussein Mwinyi.

Wengine ni Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, Askofu wa Kanisa la Katoliki Jimbo Iringa Tarcius Ngalalekumwa na Mufti Mkuu wa Bakwata Sheikh Shaaban Bin Simba.

Hata hivyo Ukawa wameeleza kuwa wamelisusa Bunge la Katiba, baada ya kujitokeza matusi, kejeli na maneno ya ubaguzi kutoka kwa wajumbe wa CCM, ambao wanadaiwa kuwa waliacha kujadili hoja za msingi na kuanza malumbano kinyume na dhamira ya kuundwa Bunge maalumu la Katiba.

Pia wanaeleza na kutoa masharti kuwa Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ijadiliwe kama ilivyo, isipunguzwe kipengele wala kifungu chochote na kwamba ushauri au maoni ya Tume yabaki vilevile kama yalivyo bila ya kutiwa mikono au kuchakachuliwa.

Madai haya ya Ukawa kwa upande mmoja yanaleta mkanganyiko na kutia hofu. Kazi ya Bunge maalumu la Katiba ni kuipitia rasimu, kuijadili, kuongeza au kupunguza yaliyomo kwa masilahi ya taifa pale inapobidi, si kuwa muhuri wa kuidhinisha matakwa ya tume yatokanayo na makamishna wao kwa kulitumia Bunge, kabla ya kuitishwa kura ya maoni.

Pia Ukawa wanamtupia lawama Rais Kikwete na kumtaja kuwa ndiye chimbuko la kuvurugika kwa mchakato huo, baada ya kutoa maoni yake kama Mkuu wa Nchi.

Dai hili kwa maoni yangu naona kama limekosa nguvu ya hoja kutokana na Rais kuwa na haki ya kutoa maoni kama ambavyo makamishna wa Tume na Mwenyekiti wao walivyotoa.

Rais pia ana haki ya kutoa maoni yake kwa niaba ya chombo anachokiongoza ambacho ni serikali na kwa niaba ya taifa akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Anapotakiwa anyamaze, afumbe mdomo au aache mambo yaende kama yanavyotakiwa na wengine, hapo atakuwa anapoteza sifa ya kuitwa Rais wa Nchi na kiongozi wa Serikali.

Kama alivyosimama Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Jopseph Warioba, Makamu Mwenyekiti wake Jaji Augustino Ramadhan na makamishna wa tume hiyo na kushiriki makongamano, semina na warsha nyingine kutetea msimamo wao, rais pia ana haki na wajibu wa kusimamia lile analoliamini kwa niaba ya Serikali.

Madai kwamba Rais amevuruga mchakato wa katiba hayana mashiko na yamekosa uzani wa kusimamia ukweli katika lengo la kumlisha maneno au kumwambia amevuruga zoezi zima la kupatikana Katiba Mpya kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa, wanataaluma na makala za waandishi wa habari.

Sote tumeshuhudia jinsi Rais Kikwete alivyoichambua Rasimu ya Katiba kitakwimu, hoja alizoziainisha, hofu yake kuhusu vipengele alivyovitaja pia wasiwasi wake kama Mkuu wa Nchi kuhusu suala la mabadiliko ya muundo wa Muungano na mabadiliko yake kama inavyotarajiwa iwe kulingana na maoni ya Tume ya Katiba.

Kadhalika wakati mjadala ukianza na wabunge kujadili sura ya kwanza hadi ya sita, pande zote mbili zilikuwa zikitupiana vijembe, mipasho na wakati mwingine kutupiana maneno mazito kinyume na uungwana wa demokrasia.

Madai ya kupatikana Katiba Mpya yamekuwa yakidaiwa na kambi ya upinzani na baadhi ya wadau tangu mwaka 1992 kwa kuelezwa kuwa Katiba ya mwaka 1977 haikidhi haja, imepitwa na wakati, ina upungufu wa msingi na si ya kidemokrasia.

Malalamiko hayo yakazingatiwa na utawala wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete. Yamefanyika kwa weledi na utashi, mambo yamewiva, yameonyesha njia na mwelekeo wa kutosha badala yake, Wajumbe wa Ukawa wanatoka na kususia vikao.

Katika rasimu hiyo ya Katiba ukiangalia kwa kina na undani, utajua na kubaini pande zote zinatakiwa kuacha kejeli na mipasho, zijadili hoja, wanachokikataa au kukiafiki waonyeshe kama ni kweli hawakitaki kwa sababu zipi na kuafiki kwa minajili gani badala ya kuweka mbele itikadi na sera za vyama.

Kwa mfano, kabla ya kutoka kwao nje kumekuwa na matamshi kuwa Wajumbe wa CCM madai waliokuwa wakiyatoa Zanzibar kabla ya kufika Dodoma wamefyata na kushangaa hulishwa kitu gani wanapovuka bahari kuja Dar es Salaam hadi Dodoma.

Wengine wakasoma Hansard kuhusu michango ya wajumbe ili kuwasuta na kuelezwa huo ndiyo unafiki na uzandiki.

Upande wa upinzani nao ukatupiwa maneno ya usaliti wa Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar, wakaitwa vibaraka na mawakala wa utawala ulioangushwa mwaka 1964 huku wengine wakiambiwa Zanzibar si kwao na hata rangi zao hazifanani na Afrika,

Wakati akitoka bungeni Profesa Ibrahim Lipumba aliliita Bunge hilo ni la Interahamwe. Tafsiri yake ni mbya sana, haifai kuelezwa au kutamkwa na kiongozi anayeaminika katika jamii mwenye kaliba yake kama msomi na mweledi kitaaluma.

Haya yote hayakustahili kutamkwa ndani ya Bunge la Katiba. Madhali viongozi wa juu wakiwamo wanasiasa na viongozi wa madhehebu ya dini kuwataka Ukawa warejee bungeni, nafikiri ni wakati wao mwafaka Ukawa kukaa na kutafakari ushauri uliotolewa ili warejee bungeni.

Rasimu ya Katiba imesheheni mambo mengi muhimu, yanayohitajika kwa wakati tulionao. Ikiwa yatakosekana kupatikana mwakani, anaweza akatokea rais mkorofi, asiyeambilika wala kushaurika akasema hana mpango wa kuunda katiba mpya hadi miaka 50 mingine ipite na kuiona iliopo inafaa na kukidhi haja.

Ikiwa hilo litatokea,kundi la Ukawa halitaachwa kubebeshwa lawama na viongozi wake wataingia katika kurasa za lawama ya kihistoria kwa kutopima wakati na kusoma kuvuma kwa pepo ili kushika turufu na piku mkononi mwao.

No comments:

Post a Comment