January Makamba, Zitto waungana urais

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (kulia) akimweleza jambo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe. Picha na Maktaba 
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi


Dar es Salaam. Uamuzi wa mwanasiasa kijana, January Makamba wa kutaka kuwania urais, umezidi kukoleza mijadala ya kisiasa katika mitandao ya kijamii na kuibua hoja zinazokinzana kuhusu ujana na uzoefu wa uongozi.

Makamba (40) ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na mbunge wa Bumbuli (CCM), ametangaza kuwa ameamua kwa asilimia 90 kujitokeza kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, akisema asilimia zilizobaki zitategemea mambo kadhaa.

Katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa facebook, Makamba alisema uongozi wa kizazi kipya upo tayari kushika hatamu za uongozi na kuijenga Tanzania mpya, fikra mpya na maarifa mapya.

Alisema mabadiliko yaliyotokea Tanzania, yalidaiwa na kuongozwa na vijana na kwamba vijana nchini wanaweza kushika usukani wa kuleta mabadiliko wanayoyataka.

“Ukiona kijana anamwambia kijana mwenzake hana uzoefu, basi kazi ya kuleta mabadiliko ni kubwa zaidi. Kutokuwa na uzoefu ni sifa ya kijana.”

Alisema kuwa tusi kubwa kwa Rais wa Marekani, Barack Obama mwaka 2008 lilikuwa ni kukosa uzoefu na kukosa rekodi, lakini tusi hilo liligeuka kuwa muziki kwa wapigakura wa nchi hiyo.

“Tanzania mpya inahitaji viongozi wapya, mazoea mapya, fikra mpya na maarifa mapya. Inahitaji kuthubutu mambo makubwa siyo kulinda uzoefu wa nyuma... tunaweza,” ameandika mwandishi huyo wa zamani wa hotuba za Rais Jakaya Kikwete.

Akichangia mada hiyo, mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema: “Ni kweli vijana hatuna uzoefu. Uzoefu wa kuiba. Tunataka namna mpya na bora ya kuongoza nchi. Nilipochaguliwa kuwa mbunge mwaka 2005 sikuwa na uzoefu. Kulikuwa na wengi wenye uzoefu, lakini uzoefu wa posho bila kazi.”

Naye William Sunday Sempoli alisema tatizo siyo umri wa mtu. Unaweza ukawa kijana mwenye mawazo ya kizee na unaweza ukawa mzee mwenye mawazo ya ujana. “Tanzania tunamhitaji mtu mwenye uwezo wa kututoa hapa tulipokwama na kutupeleka mbele.”

Kwa upande wake Cleophas Cyprian alisema kabla ya kuchagua vijana mwaka 2015, “Ninyi mliopo sasa ilitakiwa muonyeshe uwezo wenu katika kulipigania taifa kwa matendo na siyo maneno”.

Method Nyakunga akichangia mjadala huo alisema tatizo siyo tu kizazi kipya, alihoji kama mifumo nayo ni mipya? “Kama mifumo ni hii iliyopo basi labda kizazi kipya kitokane na vyama vya upinzani kwani ndani ya chama tawala, kwa namna kilivyo sasa, kimehodhiwa na watu wachafu wa kila aina wanaoangalia masilahi yao.”

Mzalendo Joseph Goliama alisema uko sawa kwa upande mmoja lakini kwa upande mwingine kauli hizo ni za ubaguzi wa rika. Nchi yetu na katiba ya nchi yetu inataka Rais atokane na Watanzania wenyewe.

No comments:

Post a Comment