Leo tuzungumzie watoto. Tuangalie afya, mapenzi
na usalama wao. Hakuna kipindi cha historia yetu wanadamu ambapo watoto
wanafanyiwa unyama duniani kama sasa.
Machi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto
(UNICEF) lilisema tangu vita vianze vita Syria, watoto 10,000, wameuawa
makusudi. Wengine milioni tano hawana makazi maalumu. Mauaji haya
yanafanywa majumbani, mashuleni, mitaani na kambi za wakimbizi. Watoto
wanapigwa risasi makusudi na magaidi wa Boko Haram, Nigeria. Miezi
miwili sasa wasichana 200 waliotekwa na hawa (wanaotumia dini kama ngao
ya uyahawani wao) hawajapatikana. Kila kukicha watoto vijijini na
shuleni Nigeria wanauliwa bila hatia yoyote.
Wiki iliyopita mtoto wa Kipalestina, Tarik Abu
Khdeir, mwenye miaka 15 alipigwa na askari wa Kiyahudi Jimbo la West
Bank nusura afe. Alipokuwa akiongea na wanahabari uso mzima ulikuwa
umemvimba utadhani kaota vichuguu vya mchwa. Kipigo kilifuatilia mgogoro
kati ya Wapalestina na Wayahudi. Watoto watatu wa Kiyahudi walikokotwa
njiani wakakutwa wamekufa kitongoji cha Wapalestina. Serikali ya Israel
ilidai Hamas iliwaua. Ili kulipiza kisasi mtoto wa miaka 16 wa
Kipalestina, Mohammed Abu Khdeir, naye aliburutwa barabarani, akapigwa
kikatili na kutupwa msituni kama fuko.
Ingawa waliohusika wameshakamatwa na askari wa Israel, haisaidii kurudisha maisha ya watoto.
Barani Afrika, nchi zenye vita mathalan, Jamhuri
ya Afrika ya Kati, Sudan na Kongo, unyanyasaji wa watoto ni jambo la
kawaida. Umoja wa Mataifa umekadiria asilimia 65 ya ubakaji uliofanywa
Kongo kipindi cha miaka 15 iliyopita uliwaathiri watoto. Asilimia kumi
ya watoto waliobakwa Kongo wana umri chini ya miaka kumi! Mbali ya
kubakwa, kupigwa au kulawitiwa watoto hulazimishwa kubeba mizigo na kuwa
askari.
Kwetu Tanzania mateso ya watoto- kwa njia
mbalimbali- yamefikia daraja la kishetani kwa taifa hili lenye utamaduni
mahususi wa amani. Juma lililopita msichana wa kazi za nyumbani, ambaye
jina lake halikutajwa (aliitwa tu ‘hausigeli’ utadhani kijiti au kifuu
cha nazi) aliteswa miaka miwili na tajiri wake, Boko, Kinondoni. Mateso
ya watoto wanaofanya kazi majumbani hayasemeki. Kwa kuwa hawana midomo,
haki au cha kuwatetea, hali zao hazifahamiki.
Baadhi ya maoni ya wasomaji kwenye mitandao
yanasomeka: “Huwezi kumtesa binadamu mwenzio kiasi hiki hata kama
amefanya nini, unampiga kama mwizi, lahaulaa. Ilhali yeye ndiye
anayeangalia nyumba yako?”
Au “Yaani ukatili mwanamke unamfanyia mtoto wa
mwenzio hivyo au hujawahi kuzaa hujui uchungu? Huyu ni sawa na muuaji
hukumu yake ni kifo tu. Je, kama ni mtoto wake alifanyiwa hivyo
angejisikiaje?”
Hali inadhirisha ukosefu wa utu na ubinafsi ulioenea leo.
Labda tutasema unyanyasaji huu ni wa waovu
wachache tu. Lakini je, watu wazima wenye nafasi zao wanaolala na
kuwalawiti watoto kisirisiri?
Hapa Uingereza mwaka mzima sasa ‘tetemeko la
habari’ linaendelea kufichua visa vya watu mashuhuri waliowalawiti au
kuwabaka watoto.
Mosi alikuwa Jimmy Saville. Mstahiwa alikuwa
mtangazaji mashuhuri wa BBC aliyependwa na mamilioni kiasi ambacho
hakuna hata mtu mmoja aliyemkisia mabaya. Jimmy Saville na sigara lake
kubwa, nywele nyeupe zilizofanana na katani, miwani mekundu juu ya pua
nene iliyompa sura ya majigambo na vichekesho alifariki dunia mwaka 2011
akiwa na miaka 84. Baada tu ya mazishi malalamishi na mashtaka zaidi ya
200 yalifanywa na wanawake na wanaume waliodai aliwafanyia uanaharamu
wakiwa watoto lakini enzi hizo sheria iliziba masikio. Hawakusadikiwa.
Wengine wanne walidai aliwachezea wakiwa na miaka kumi. Kutokana na
umaarufu wake alipewa ufunguo akaruhusiwa kuingia hospitalini kutumbuiza
wagonjwa ambao aliwanajisi na kuwafanyia uchafu. Aliingia vyumba vya
vilema na maiti. Karibuni madai yameongeza kusema Bwana Saville
alihusudu kulala pia na maiti. Alifanya vituko hivi tangu mwaka 1964.
Baada ya habari za Jimmy Saville kuzagaa, watu wengine maarufu
wanaendelea kushtakiwa. Wiki jana mwanamuziki na mchoraji aliyetunukiwa
taji la heshima na Malkia na kuitwa Sir Rolf Harris, alihukumiwa kifungo
cha miaka mitano baada ya kupatikana na hatia 12 za kulala na watoto.
Madai yanasema Bwana Harris mwenye umri wa miaka 84 alianza ufuska wake
miaka 40 iliyopita. Tarakilishi au kompyuta zake zilikutwa na picha
zaidi ya 200 za watoto wadogo wakiwa uchi.
Wakati mashtaka yakiendelea Serikali imetangaza
mabomu mawili. La kwanza lahusu viongozi serikalini. Mwaka 1983 enzi za
uongozi wa marehemu Margaret Thatcher uchunguzi uliofichua ulawiti na
ubakaji wa watoto ndani ya mashirika makubwa ya hospitali, BBC na
serikalini ulizimwa. Aliyepewa mafaili ya uchunguzi Bwana Leon Brittan,
tajiri- mbunge na Waziri enzi hizo-inadaiwa aliyaharibu mafaili ya
mashtaka. Wiki jana Serikali iliamuru uchuguzi ufanywe na maofisa saba
wa polisi wameteuliwa kuusimamia.
Bomu la pili ni ukeketaji. Alhamisi Julai 3,
Serikali ya Uingereza iliwaamuru waganga, walimu na wafanyakazi wa
taasisi za umma kutotetereka kuzuia ukeketaji eti kwa sababu za
kitamaduni. Tangu sheria ilipopitishwa kutokomeza desturi hii mwaka 1985
hakuna aliyeshtakiwa hadi mwaka huu.
“Ukeketaji ni uhalifu. Siyo suala la kikabila bali
utesaji. Siyo jando unyago bali unyanyasaji.” Kamati husika ya Wizara
ya Uhamiaji ilitamka. Baraza la Waislamu Uingereza nalo lilitoa taarifa
iliyopinga vikali ukeketaji na kusema Uislamu hauafiki kitendo hicho.
Wenzetu wameamua vita kutetea watoto.
Je, sisi Afrika?Ukeketaji, ubakaji na kulawiti
watoto vinaendelea kisirisiri (na wazi) mijini na vijijini Tanzania.
Sababu kuu ni umaskini na watoto wengi kutokwenda shule. Watoto
kulazimika kulala nje au kuishi maisha ya dhiki. Pili, woga umeenea.
Wahusika hawasemwi. Vyombo husika huficha au kutumia mabavu kuuzima
moto.
No comments:
Post a Comment