Mgeja, Guninita wajiengua CCM, wajiunga Chadema

Kutoka kushoto  ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM
Kutoka kushoto  ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa    Dar es Salaam John Guninita na aliyekuwa mwenyekiti Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja ambao leo wamehamia Chadema. 
By Louis Kolumbia, Mwananchi Digital

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na aliyekuwa mwenyekiti mkoa wa Dar es Salaam John Guninita wametangaza leo kuachana na CCM na kujiunga Chadema.

Makada hao wa CCM wametangaza kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam leo.

Wakizungumza katika mkutano huo, makada hao wamesema wamechukua uamuzi huo baada ya kubaini CCM imepoteza mwelekeo na kwamba kinaendeshwa kibabe tofauti na misingi ya kuasisiwa kwake.

Wametolea mfano wa kukiukwa kwa demokrasia kulikofanywa wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais wa chama hicho ambapo Dr John Magufuli aliteuliwa kupeperusha bendera ya CCM.

Hatua ya makada hao imekuja ikiwa ni siku moja tu tangu aliyekuwa mbunge wa chama hicho jimbo la Sikonge, Said Nkumba atangaze kuachana na chama hicho na kujiunga na Chadema.

Huo ni mwendelezo wa matukio ya makada na wabunge chama hicho kuhamia upinzani hasa Chadema kwani awali aliyekuwa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa aliachana na CCM baada ya jina lake kukatwa na kamati ya maadili ya chama hicho.

Wengine waliohama CCM ni aliyekuwa mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, aliyekuwa mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga ambaye pia ni naibu waziri Kazi na Ajira, aliyekuwa mbunge wa Kahama, James Lembeli, aliyekuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai na mbunge wa viti maalumu anayemaliza muda wake Esther Bulaya.

No comments:

Post a Comment