Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce
Ndalichako akionyesha karatasi ya majibu ya mmoja wa watahiniwa wa
mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2012, Dar es Salaam jana.
WIZARA ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi inaweza kukumbwa na kashfa kubwa kutokana na matokeo
mabaya ya kidato cha nne ya 2012 yaliyotangazwa juzi na Waziri wake, Dk
Shukuru Kawambwa.
Kashfa hiyo inatokana na aina ya majibu
yaliyoandikwa na baadhi ya watahiniwa katika mitihani hiyo, huku wengine
wakikusanya vitabu vya majibu bila kujibu chochote, hali inayohusishwa
na uhaba mkubwa wa walimu katika baadhi ya shule za sekondari nchini.
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Mitihani (Necta), Dk Joyce Ndalichako alisema
wasahihishaji walikutana na mambo ya ajabu yakiwamo matusi, michoro ya
vitu visivyoeleweka, mashairi na nyimbo za muziki wa kizazi kipya (bongo
fleva).
“Mwaka jana tulikutana na ‘single’ yaani
waliandika mashairi kwa uchache, lakini mwaka huu tumepata albamu nzima…
ni vituko vitupu, wengine wanaandika mapenzi, mwanafunzi anatumia
ukurasa mzima kumlalamikia mpenzi wake. Miongoni mwa yaliyoandikwa ni
mpenzi, umeniacha, natamani kunywa sumu, usiku silali nakuwaza wewe…”
alisema Dk Ndalichako.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili ofisini kwake Dar es Salaam jana, Dk Ndalichako alisema wanafunzi
wengine waliandika malalamiko dhidi ya wabunge na uendeshaji wa Bunge.
“Unakuta mwanafunzi anaeleza anavyolishangaa
Bunge… mtu anaandika… nawashangaa wabunge, wamekaa kama wapo kijiweni,
wabunge wamekosa ustaarabu, badala kujadili kero za wananchi
waliowachagua, wanapokea timu zilizoshinda makombe… timu ikishinda Kombe
la Kagame inapokelewa bungeni. Bunge limekuwa kama kijiwe, bungeni siyo
ukumbi wa starehe kama mnataka kupokea timu hizo nendeni katika ofisi
zao au viwanjani…” alisema.
Alisema wanafunzi walioandika vitu visivyoeleweka walikuwa ni wengi na walichangia kwa kiasi kikubwa matokeo kuwa mabaya.
Dk Ndalichako alionyesha baadhi ya michoro
hiyo ambayo inaonyesha vikaragosi ambavyo wanafunzi hao waliviita Messi
(Lionel, mchezaji wa Barcelona) na zombi (ni picha za kutisha) ambazo
huonyeshwa kwenye televisheni.
Sababu za kufeli
Dk Ndalichako alisema
hawezi kuwa na jibu la moja kwa moja juu ya kwa nini matokeo ya mwaka
huu yamekuwa mabaya, lakini akadokeza kuwa huenda yametokana na
wanafunzi wengi kukosa maarifa.
Anasema mbali na waliojaza matusi na michoro,
wanafunzi wengine waliofanya vibaya ni wale ambao hawakujaza chochote
kwenye karatasi zao za majibu.
“Kuna baadhi ya shule unakuta darasa zima
watoto hawajajibu somo fulani kwa mfano Biolojia, wanaingia tu na
kuandika namba. Tuliamua kuwapigia simu walimu wao, majibu waliyokuwa
wakitupa ni kuwa hawajawahi kuwa na walimu wa somo husika kwa hiyo
watoto hawakuwa na cha kujaza.”
Dk Ndalichako alisema kwa ku mbukumbu zake, hakuna matokeo mabaya kama ilivyo kwa mwaka huu yaliyowahi kutokea.
“Tukiangalia tu kuanzia 2000, hakujawahi
kutokea matokeo mabaya kama haya, kwa kweli hali haipendezi. Hata kabla
ya kuyatangaza nilikuwa nayaangalia mara tatu tatu, sikuyapenda na
inasikitisha kwa kweli,” alisema Dk Ndalichako.
Udanganyifu
Dk Ndalichako alisema hakukuwa na uvujaji wa mitihani wala udanganyifu wa ndani kwani vitendo hivyo vilidhibitiwa.
Alisema
baadhi ya wanafunzi wamefutiwa mitihani yao kutokana na majibu yao
kukutwa na mfanano usiokuwa wa kawaida na kutoa mfano wa wanafunzi tisa
katika shule ambayo hakuitaja kwamba majibu yao yalifanana katika somo
la Kiswahili.
Alisema katika somo hilo, kulikuwa na swali
lililotaka wanafunzi waandike shairi la kuonyesha umuhimu wa mwalimu na
kwamba wanafunzi hao waliandika shairi moja la majigambo lililofanana
kwa kila kitu.
“Ni vigumu wanafunzi wote tisa kuwaza na
kuandika kitu kimoja, shairi hilo lilifanana kila kitu na kwenye
kiitikio wote walikosea kwa kuandika neno ‘hacheni’ niitwe mwalimu
badala ya ‘acheni’ niitwe mwalimu,” alisema.
Dk Ndalichako alisema udanganyifu mwingine
ulionekana katika somo la hisabati, hali iliyothibitisha kuwapo kwa
maandalizi ya pamoja ya majibu. Katika shule moja wanafunzi 90 walifanya
kosa linalofanana.
Awasifu wasimamizi
Dk Ndalichako aliwamwagia sifa wasimamizi wa mitihani hiyo akisema walitimiza wajibu wao kikamilifu.
Alisema kutokana na umakini wa wasimamizi hao wanafunzi waliokuwa wameficha madaftari sehemu za siri walibainika.
“Kuna mmoja wa kike alikuwa ameficha daftari
kwenye sehemu za siri, msimamizi akamwona anahangaika kweli hata
kutembea hawezi, akatuma walinzi wa kike kumkagua akakutwa ameficha
daftari sehemu za siri,” alisema Ndalichako:
“Kwa hiyo wasimamizi walifanya kazi ya ziada,
kumfutia matokeo lazima kuwe na ushahidi wa kutosha. Mfano wanakuta mtu
amejiandika kwenye kiganja cha mkono ama kanyagio la mguu, huwezi kukata
na kuleta kama ushahidi lakini walitafuta mpigapicha wakapata picha
wakaleta kama ushahidi.”
Alisema mitihani yote iliyotungwa ilikuwa
ndani ya mihutasari na ilitokana na mambo ambayo wanafunzi hao
wangetakiwa wayasome ndani ya miaka minne.
CWT: Mgomo hauhusiki
Rais wa Chama cha
Walimu Tanzania(CWT), Gratian Mukoba alisema matokeo hayo ni kitu
ambacho kimekuwa kikikua kila siku na kwamba kufeli huko hakuhusiani na
mgomo wa walimu wa mwaka jana.
“Matokeo haya ni ‘trend’ ya miaka mingi ila
watu walikuwa hawajajipanga kuyapokea kama ya sasa. Ni tatizo
lililojitokeza kidogo kidogo hadi lilipofikia sasa,”alisema Mukoba na
kuongeza:
“Suala hili lisipotafutiwa ufumbuzi, tutazalisha kizazi kitakachokuja kutulaumu kwa sababu hatukukiandalia mazingira mazuri.”
Mukoba alisema matokeo hayo yasihusishwe na mgogoro wa walimu
kwani wakati mgomo ulipoanza tayari walimu walikuwa wameshafundisha
zaidi ya nusu mwaka na wanafunzi wangeweza kufanya mtihani.
“Matokeo mabaya hayahusiani na mgogoro, kwa
sababu ulidumu kwa muda mfupi. Hata hivyo, wakati wa mgogoro ilikuwa
nusu ya mwaka imeshafundishwa,” alisema Mukoba.
No comments:
Post a Comment