Mzimu wa Sharomilionea waanza kazi, wezi warudisha vifaa vyake

Gari aliyokuwa akiendesha Marehemu Sharomilionea baada ya

JESHI la Polisi mkoani Tanga limefanikiwa kukamata vitu mbalimbali vya marehemu Hussein Ramadhan, ‘Sharo Milionea’ vilivyoibwa na watu wasiojulikana, muda mfupi baada ya msanii huyo wa filamu na muziki nchini kupata ajali katika Kijiji cha Songa Kibaoni, wilayani Muheza na kufariki dunia papo hapo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Costantine Massawe alisema Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata begi la nguo, simu ya mkononi aina ya blackberry, betri ya gari, redio, tairi la gari na saa ya mkononi ya marehemu.

Alitaja vitu vingine vilivyopatikana kuwa ni nguo ambazo marehemu alivuliwa baada ya kupata ajali, ambazo ni fulana na suruali ya jeans.

Alisema kuwa,vitu hivyo vilipatikana baada ya wakazi wa kijiji ilipotokea ajali hiyo kuvisalimisha vitu hivyo kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Songa kibaoni, Abdi Zawadi .

“Vitu viliwasilishwa na wasamaria wema kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Songa Kibaoni, Abdi Zawadi ambaye alitoa taarifa polisi kwa ajili ya utambuzi na taratibu nyingine,” alisema Massawe.

Aliwataka wananchi wa Kibaoni kuendelea kutoa ushirikiano ili viweze kupatikana vitu vingine vya marehemu na kuongeza kuwa, jeshi hilo linaendelea na uchunguzi, ili kubaini pesa na vitu vingine vilivyokuwamo ndani ya gari hilo ambavyo havikupatikana.

“Hivi vitu mnavyoviona hapa vimesalimishwa na watu ambao huenda walishiriki katika wizi, au waliviona mahali na kwa mapenzi yao kwa marehemu wakaamua kuvirejesha,” alisema Massawe

Alisema baadhi ya vitu hivyo vilikamatwa nje ya wilaya ya Muheza katika gereji na kwenye nyumba za watu.

Kamanda alifahamisha zaidi kuwa, hadi sasa watu kadhaa wanashikiliwa na jeshi hilo kwa kuhusika na tukio hilo.

“Tunaamini kuna vitu vingi vya thamani havijapatikana, bado tunaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na wananchi na mtu atakayekutwa na kitu chochote cha marehemu atashtakiwa,” alisema Massawe.

Alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu kadhaa waliokutwa na vitu hivyo, lakini hakutaja idadi yao kwa kuwa vitu vingine havijapatikana.

“Pamoja na hayo, vitu vilikuwa vinasalimishwa usiku na wengine walivileta mchana kwa mwenyekiti wao. Hata hivyo, si kwamba mtu aliyeleta anakamatwa papo hapo, ila wale watakaokutwa navyo tutawakamata na kuwashtaki,” alisema Kamanda Massawe.

 DC atoa neno

Awali Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu aliliambia Mwananchi kuwa, licha ya kusalimisha vitu hivyo hakuna mtu aliyekamatwa kwa sababu washukiwa bado wako mafichoni.

“Kwa kweli hadi sasa aliyekamatwa kwa sababu washukiwa wote wamejificha,”alisema Mgalu.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kupatikana kwa vitu hivyo, kulitokana na amri aliyoitoa baada ya mazishi ya msanii huyo, kuwataka wakazi wa eneo ilipotokea ajali kuvirejesha vitu hivyo ifikapo Ijumaa saa 12.

“Nilikuwa kijijini Songa kibaoni hadi saa 5.30 usiku juzi (Jumatano) nikiwa sambamba na wakazi wa kijiji hicho ambao walipiga kura ya siri za kuwafichua waliohusika katika tukio hilo,” alisema Mgalu.

Aliwataka waliokimbilia mafichoni kurejea haraka watu wanaopatwa na ajali. Kwani lengo la Serikali ni kutaka wanaoishi kando ya barabara kuacha kuwafanyia unyama majeruhi na maiti mara zinapotokea ajali kwenye maeneo yao.

Jaji Mkuu: Siku ya kesi ya Lema nitakuwa nje ya nchi, sijajitoa


JAJI Mkuu, Mohamed Chande Othman, ambaye amefafanua suala la yeye kutoshiriki katika kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha



JAJI Mkuu, Mohamed Chande Othman ameeleza sababu za kutokuwa kwenye jopo la majaji waliopangwa kusikiliza kesi ya aliyekuwa mbunge wa Chadema mkoani Arusha, Godbless Lema.

Jaji mkuu, alitoa maelezo haya jana alipozungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu kwenye mahafali ya 12 ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

“Ngoja nitolee ufafanuzi suala hilo ili jamii itambue utaratibu wa uendeshaji wa Mahakama ya Rufani, ambayo ina majaji 16 nchini,” alisema Jaji Othman.

Jaji Othman alisema kimsingi hajajitoa kushughulikia kesi hiyo, ila siku ambayo kesi hiyo inatajwa, atakuwa nchini India kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 13 wa Majaji Wakuu Duniani.

Maelezo hayo ya Jaji Chande yamekuja siku tatu baada ya gazeti hili kuripoti kuwa, mkuu huyo wa mhimili wa Mahakama nchini amejitoa kusikiliza kesi hiyo na nafasi yake imechukuliwa na Jaji Bernard Luanda.

“Kwanza ifahamike kwamba, jaji wa Mahakama ya rufani hana ubia na kesi yoyote kwa mujibu wa utaratibu. Jaji yeyote kati ya majaji 16 wa mahakama ya rufani nchini ana mamlaka ya kusikiliza kesi yoyote ya rufani,” alieleza Jaji Othman.

Jaji Othman alifafanua kuwa, rufani ya Lema ni miongoni mwa kesi tatu za uchaguzi zilizobaki ambazo kwa mujibu wa taratibu za kisheria, huanza kusikilizwa baada ya muda wa mwaka mmoja na hukumu yake ni lazima itolewe ndani ya mwaka mmoja tangu kuanza kwake.

“Hivyo basi, kwa vile Jaji yeyote wa Mahakama ya Rufaa anaweza kuisikiliza kesi hiyo, hakukuwa na sababu inisubiri mimi,” alisema.

Jaji Othman alitaja kesi nyingine za uchaguzi zitakazoanza kufanyiwa vikao vya rufani na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufani kuwa, ni ile ya Jimbo la Ubungo kati ya Hawa Ng’umbi na John Mnyika ambayo itakuwa chini ya jopo la majaji watatu; Jaji Nathalia Kimaro, Jaji Salum, Salum Masati na Jaji Katherine Oriyo.

Nyingine ni ya Jimbo la Ilemela ya Yusuph Yussuph Masengela Lupilya na wenzake wawili dhidi ya Highness Kiwia na wenzake wawili, ambayo itakuwa chini ya jopo la Majaji Januari Msofe, Jaji Beard Luanda na Jaji Salum Massati.

Alisema rufani ya Lema haijaanza kusikilizwa kwa jaji yeyote, hivyo yeye asingeweza kujitoa kwa kuwa hajapangiwa.

“Kinachotatiza hapa ni kwamba, watu wanaifungamanisha rufani hii na ile ya Arusha ambayo mimi nilikuwa miongoni mwa jopo la majaji kama mwenyekiti.

“Ile ilikuwa ni pingamizi ya rufani, wakati hii ya Dar es salaam ni rufani ambayo lazima isikilizwe hadi kufikia hukumu,” alisema Jaji Chande.

Alisisitiza kuwa, hajajitoa wala hajaombwa kujitoa kwenye rufani kwa kuwa haifungamani na ile ya Arusha ambayo alikuwa mwenyekiti wa Jopo la Majaji, huku akifafanua kuwa kesi hiyo ya Arusha ilikuwa ya kupinga rufani na hii ya sasa inayosikilizwa Dar es salaam ni ya rufaa na inaanza upya kisheria.

Alieleza kuwa, Desemba 4, mwaka huu vitaanza vikao vya majaji wa mahakama ya rufaa vya kupitia kesi za rufani za uchaguzi zilizopangwa kufanyika Dar es Salaam, Zanzibar na Iringa wakati atakuwa kwenye mkutano mkuu wa majaji duniani utakaofanyika Lucknow, India.

Kuhusu kesi hiyo kuhamishiwa Dar es Salaam, Jaji Othman alisema wanasheria wa Godbles Lema ndiyo walioomba ihamishiwe huko.

“Suala la kuhamishiwa rufani hiyo Dar es Salaam si la Mahakama ya Rufani bali waaliomba wanasheria wa Lema na hii inakubalika kwa lengo la kukimbizana na muda kabla ya kufikia tamati, kwani mahakama imepewa muda wa kumaliza kesi zote za uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema Chande.

Mahakama hiyo ilikubali hoja ya wajibu rufaa kuwa, rufaa hiyo ilikuwa na dosari kutokana na tofauti ya vifungu vya sheria vilivyotumika katika hukumu iliyomvua ubunge Lema na vilivyotumika katika hati ya kukaza hukumu, iliyowasilishwa mahakamani sambamba na rufaa hiyo.

Hata hivyo, kilichomwokoa Lema ni kifungu cha 111 cha Kanuni za Mahakama, ambapo mahakama hiyo ilisema kuwa chini ya kanuni hiyo, dosari hizo zinaweza kurekebishwa.

Jaji Chande ndiye aliyekuwa kiongozi wa jopo la majaji watatu katika kesi hiyo akiwamo Salum Massati na Natalia Kimaro. Jaji Mkuu aliingia kwenye kesi hiyo akichukua nafasi ya Jaji Mbarouk Salim Mbarouk aliyekuwa amepangwa awali, ambaye sababu za kuondolewa hazikuwekwa wazi.

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI DESEMBA 1









Ushahidi mpya wa mauaji ya Mau Mau


Baadhi ya wapiganaji wa Mau Mau waliodhulumiwa na wakoloni wa Uingereza

Stakabadhi za Serikali zilizotolewa huko Uingereza zinaonyesha kwa ukamilifu namna wafungwa wengi waliuawa wakati wa uasi wa kundi la Mau Mau nchini Kenya.

Wakenya kumi na mmoja walipigwa na walinzi hadi kufa katika kambi walikozuiliwa ya Hola huku wengine wakijeruhiwa mwaka 1959.

Mzee moja manusura wa mauaji hayo kwa sasa ameshtaki serikali ya Uingereza akidai aliteswa.

Stakabadhi hizo zinaonyesha mkutano uliongozwa na aliyekuwa gavana wa Kenya na maafisa wakuu wa magereza kumbukumbu zinazoonyesha kuwa maafisa hao walikiuka haki za binadamu lakini hawakufunguliwa mashtaka.

Palestina yapandishwa hadhi na UN


Wapalestina walisherehekea sana kufuatia tangazo hilo

Baraza la umoja wa mataifa limepitisha kwa kauli moja kwa wingi wa kura kupandisha hadhi ya eneo la Palestina.

Nchi mia moja thelathini na nane ziliunga mkono hatua ya kuitambua Palestina kuwa nchi ambayo si mwanachama wa Umoja wa mataifa lakini itaruhusiwa kushiriki katika shughuli za umoja wa mataifa.

Mataifa tisa yakijumuisha Isarael na Marekani yalipiga kura ya kupinga mpango huo huku mataifa arobaini na moja yakisusia shughuli hiyo.

Kura hiyo yenye umuhimu mkubwa sasa inaiwezesha Palestina kuwa na ushirika na umoja wa mataifa na mashirika mengine kama vile mahakama ya ICC.

Mwandishi wa BBC amesema kuwa wapelestina wanaweza kutumia nafasi hayo kuishataki Israel kwa kusababisha visa vya dhulma dhidi ya ubinadamu katika ngome yake.

Mmiliki gari lililomuua Sharo Milionea

Hussein Ramadhani ‘Sharo Milionea’ (27) 

MMILIKI wa gari ambalo lilikuwa likiendeshwa na msanii maarufu nchini, Hussein Ramadhan ‘Sharo Milionea’ na kupata nalo ajali iliyosababisha kifo chake huko Muheza, Tanga, Mohammed Ismaili maarufu kwa jina la Mudi Suma, ameibuka na kueleza uhusiano wake na marehemu, huku akisema amekubali hasara.


Akizungumza kwa simu kutoka Muheza jana Suma alisema hana mpango wa kudai fidia au kupeleka malalamiko yoyote kwa ndugu wa marehemu kwa kuwa; “Kilichotokea ni kazi ya Mungu.” “Siwezi kudai hata kidogo hivyo ni vitu vya kupita tu. Marehemu alikuwa ni zaidi ya ndugu yangu, gari ni kitu kidogo sana katika uhusiano tuliokuwa nao,” alisema Suma na kuongeza kwamba hata Marehemu Sharo Milionea naye alikuwa amemwachia mali zake kadhaa ikiwamo gari.


“Siyo gari tu alilokuwa ameniachia. Kuna mikataba yake ya kazi, Bajaji yake na funguo za chumbani kwake. Nasubiri kukabidhi vitu hivyo baada ya kukaa na ndugu zake. Vitu viko kwenye mikono salama,” alisema.


Kuhusu gari lake lililopata ajali, Suma alisema lilikuwa na bima ndogo, lakini anapanga kwenda TRA atakaporejea Dar es Salaam kufuatilia baadhi ya mambo.
“Kabla ya kuondoka bima ile kubwa ilikuwa imekwisha kwa hiyo nikaamua kuikatia bima ndogo. Nitakapofika kesho (leo) Dar es Salaam, nategemea kwenda ofisi za bima kuzungumza nao,” alisema Suma.


Alipoulizwa kama kuna mtu mwingine atakayeathirika kutokana na gari hilo kuharibika katika ajali mbali na yeye, alijibu: “Hakuna tofauti na mimi mwenyewe na familia yangu.”


Kabla ya ajali
Suma alieleza kuwa kabla ya kuanza safiri yake, Sharo Milionea alifika nyumbani kwake mchana na kumweleza kuwa afya yake haikuwa nzuri.


“Kabla ya kuondoka aliniambia kuwa hajielewi elewi na kifua kilikuwa kinambana. Nikamshauri asiondoke peke yake, atafute mtu wa kuondoka naye ambaye atamsaidia kuendesha gari njiani,” alisema Suma na kuongeza:


“Tulianza kuwapigia simu jamaa zetu wanne wa kusafiri naye lakini kila tuliyemwambia hakuwa tayari. Ilikuwa ni changamoto mpaka ilipofika saa 10:45 hivi jioni, akaamua kuondoka peke yake. Wakati anatoa gari getini kwangu, nikamwambia, basi jaribu kuwa mwangalifu sana, maana alikuwa kweli anasumbuliwa na kifua. Tukakubaliana kwamba atakaporudi aende hospitali kucheki afya yake.”


Kuhusu uhusiano wake na marehemu, Suma alisema: “Mimi ni mfanyabiashara na yeye alikuwa msanii, lakini ilitokea tukawa marafiki sana mpaka ikafikia wakati nikaona kuwa ni ndugu yangu. Nilimwamini nikamtambua kama sehemu ya familia.”


Alisema marehemu alikuwa akitumia gari hilo kila alipolihitaji na safari ya kwenda nalo Tanga kwa wazazi wake ilikuwa ni ya tatu.“Siyo mara ya kwanza kuitumia gari lile, nilikuwa nimemwamini sana. Safari ya kwanza alichukua na kusafiri nalo mwenyewe, halafu safari ya pili ikafuata na hii ilikuwa safari ya tatu,” alisema Suma.


Eneo la ajali wakimbia makazi
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Songa Kibaoni mahala ambako Sharo Milionea alipatia ajali, wamezikimbia nyumba zao baada ya Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu kutoa siku moja kwa waliopora mali za marehemu huyo kuzisalimisha mara moja.


Mgalu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Muheza alisema jana kwamba usiku wa kuamkia jana, baadhi ya nyumba kijijini hapo zilikuwa tupu baada ya wakazi wake kuzikimbia.

Bakwata yamkana Sheikh Ponda mahakamani

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda 

Akitoa ushahidi wake jana huku akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, Lolila ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka alidai kuwa eneo hilo awali lilikuwa likimilikiwa kihalali na Bakwata.

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), limemkana Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake, baada ya kudai mahakamani kuwa eneo walilovamia wakidai ni mali ya Waislamu linamilikiwa kihalali na kampuni ya Agritanza.


Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman Lolila alisema hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi ya jinai inayomkabili Ponda na wenzake 49 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa pamoja na mambo mengine kuvamia na kupora ardhi na wizi wa vifaa vya ujenzi.


Akitoa ushahidi wake jana huku akiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, Lolila ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka alidai kuwa eneo hilo awali lilikuwa likimilikiwa kihalali na Bakwata.


Hata hivyo, alidai kuwa baadaye Bakwata walibadilishana na Kampuni ya Agritanza Limited baada ya kuona eneo lililobaki halifai kujengwa chuo kikuu kutokana na ufinyu wake.
Alidai kuwa awali eneo hilo lilikuwa kubwa lakini miaka ya 2000 lilianza kumegwa na kuzigawia baadhi ya taasisi na wafanyabiashara na kwamba tume iliundwa na kubaini kwamba hayo yalifanyika kinyume na utaratibu.


“Baada ya kumegwa eneo lililobakia ni finyu ambalo halitoshi kujengwa chuo kikuu. Mimi nilikuwapo wakati Baraza la Wadhamini wa Bakwata wakijadili jinsi ya kupata eneo kubwa na kuijadili Kampuni ya Agritanza iliyokuwa na eneo la ekari 40 Kisarawe ili tubadilishane,” alidai.


Shahidi huyo aliongeza kuwa Agritanza ilikubali kubadilishana maeneo na kwamba wao walichukua ekari nne zilizopo Markaz (Chang’ombe) na Bakwata ikachukua ekari 40 zilizopo Kisarawe.


“Hayo yalifanyika baada ya kupata baraka kutoka katika Baraza la Maulamaa lililokaa na kuamua hivyo Januari 22, 2011,” alisema shahidi huyo na kuongeza:
“Baada ya kufanyika mabadilishano, Agritanza walianza kushughulikia usajili wa kiwanja namba 311/3/4 na walipata. Hivyo kwa sasa ni wamiliki halali, tulishamalizana nao.”


Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa eneo hilo Serikali ililitoa kwa Wamisri kwa ajili ya kujenga chuo chini ya usimamizi wa Bakwata.
Alidai kuwa kwa mujibu wa mkataba huo uliosainiwa mwaka 2003, endapo Wamisri wataondoka Tanzania watarejesha eneo hilo katika umiliki wa Bakwata.
Shahidi huyo pia alitoa kielelezo cha makubaliano ya Baraza la Wadhamini wa Bakwata na Agritanza, kuhusu kubadilishana uwanja.


Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Juma Nassoro alipinga kwa madai kwamba kisheria walitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho mahakamani.


Akijibu hoja hizo, Wakili Kweka alidai kuwa barua halisi wanayo na kwamba ipo katika kumbukumbu za Bakwata, huku akisisitiza kuwa shahidi anastahili kutoa kielelezo hicho kwa sababu saini yake ipo.


Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo, alikikataa kielelezo hicho akisema Serikali ilitakiwa kutoa notisi kabla ya kuwasilisha kielelezo hicho.


Hakimu Nongwa alisema kwa kuwa barua halisi ipo wanatakiwa kuiwasilisha mahakamani, lakini akasema endapo barua halisi haipo, basi taarifa ya jana itatambulika kuwa notisi na wataruhusiwa kuiwasilisha.

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI NOVEMBA 30













Rufaa ya Jerry Muro Februari mwakani

 

Rufaa ya kupinga kuachiwa huru kwa aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro na wenzake wawili waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya rushwa ya Sh. milioni 10 imepigwa kalenda kusikilizwa hadi Februali 18 mwakani.


Jaji Dk. Fauz Twaibu wa Mahakama ya Kuu ya Kanda ya Dar es Salaam, alipiga kalenda rufaa  hiyo baada ya upande wa Jamhuri kuomba kuibadilisha.

Hata hivyo, ombi hilo halikuweza kupingwa na upande wowote wa mawakili kwani pande zote ziliridhika na ombi hilo na zote zimekubali tarehe hiyo iliyopangwa kwa ajili ya kusikilizwa tena rufaa hiyo.

Muro na wenzake waliachiwa huru na Hakimu Frank Moshi wa Mahakama ya Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Novemba 13 mwaka jana baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Mbali na Muro washtakiwa wengine walioachiwa huru ni Edmund Kapama maarufu kwa jina la Dokta na Deogratius Mgasa.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa Februali mwaka 2010 upande wa mastaka uliokuwa ukiongozwa na aliyekuwa wakili wa Serikali Boniface Stanslaus ambaye ni marehemu kwa sasa.

Kutokana na kifo cha wakili huyo ndipo wakili wa kujitegemea Richard Rwezengo alimwakilisha Muro na wakili Majura Magafu akamwakilisha mshtakiwa wa pili na wa tatu.

Awali ilidaiwa kuwa Januari 28 mwaka 2010 jijini Dar es Salaam washtakiwa wote na wengine ambao hawakuwepo Mahakamani walikula njama na kutenda kosa la kuomba rushwa.




Udom yachunguza wanafunzi wanaojiuza


Serikali  ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udoso), imeanza kuchunguza tuhuma za baadhi ya wanafunzi kujihusisha na biashara ya ukahaba ili kuwachukulia hatua za kinidhamu.


Udoso ilichukua hatua hiyo baada baadhi ya vyombo vya habari nchini kuripoti taarifa kuwa baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wanajihusisha na biashara hiyo ya ngono.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya wanafunzi hao, Rais wa Udoso, Yunge Paul, alisema kuwa tayari kazi hiyo imeanza na watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Alisema kuwa watu hao wanashusha heshima ya chuo hicho kikubwa na kama taasisi ambayo imebeba wasomi wengi na ni kioo cha jamii.

Aidha, alisema taarifa hiyo ya kashfa ya ngono iliyoripotiwa na vyombo vya habari imesononesha nchi nzima ukiwamo uongozi wa chuo.

“Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari kwa kweli imesononesha nchi nzima ikiwamo Udom yenyewe na wanafunzi na hivyo kuwajengea mashaka hata waajiri wao ambao wanatambua wapo hapo kwa ajili ya kusoma,” alisema.

Aliwaomba waandishi wa habari kushirikiana na taasisi hiyo katika kuhakikisha wale wote wanaojihusisha na biashara hiyo wanabainika.

Wiki iliyopita kituo kimoja na televisheni kilionyesha picha za baadhi ya wasichana wanaodaiwa kuwa ni wanafunzi wa chuo hicho wakifanya biashara hiyo katika moja ya mitaa ya mjini hapa.

Pia katika mahojiano hayo, baadhi ya wanafunzi walionyesha kusikitishwa na vitendo hivyo na kuongeza kuwa vinawadhalilisha.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idrissa Kikula, alikaririwa akisema ni vigumu kuwabaini wanafunzi wanaojihusisha na biashara.

Alisema watatumia Jeshi la Polisi kuwabaini wanafunzi hao ili wachukuliwe hatua.

Demokrasia yanawiri Somaliland


Kampeini za uchaguzi wa mitaa Somaliland

Uchaguzi wa mitaa unafanyika katika Jamhuri iliyojitangazia uhuru wake ya Somaliland , ambayo ilijitenga na Somalia zaidi ya mika ishirini iliyopi .

Uchaguzi huo haufanyiki katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo ambayo yana mzozo na jimbo jirani la Puntland.

Tangu ilipojitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991, Somaliland imekuwa ikipata mafanikio taratibu , lakini thabiti kuelekea demokrasia.

Hadi uchaguzi huu, ni vyama vitatu vilivyo ruhusiwa kuendesha shughuli zake . Sasa mfumo umewekwa na vyama saba vinachuana katika uchaguzi wa mitaa .

Vitatu vitakavyopata kura nyingi zaidi katika maeneo yote ya Somaliland vitaendelea kushindana katika uchaguzi wa bunge . Somaliland ni moja ya maeneo machache ya Somalia yaliyo na amani yanayoweza kuendesha uchaguzi .

Huenda maeneo mengine mengi ya Somalia yakasubiri kwa miaka kadhaa kabla ya kuweza kutekeleza haki yao ya kupiga kura.

Majaji wasusia kazi kumpinga rais Mursi


Rais Mursi wa Misri anapingwa kwa kujilimbikizia madaraka

Majaji wa mahaka ya rufaa nchini Misri wanajiandaa kususia kazi na kuunga mkono waandamanaji dhidi ya rais wa misri Mohammed Morsi kujipa mamlaka zaidi.

Sheria ya kumapaka mamlaka zaidi rais Mursi ilipitishwa siku ya Alhamisi wiki jana. Sheria hiyo inampa mamlaka rais kuchukua hatua zozote kulinda mapinduzi na kusema kuwa hakuna mahakama yoyote inaweza kuamua vinginevyo.

Polisi wamefyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliopiga kambi kwenye medani ya Tahrir kupinga uamuzi wa rais Morsi kujitangazia madaraka makubwa.

Picha za televisheni zimeonyesha waandamanaji walioficha nyuso wakiwarushia polisi mikebe ya mabomu hayo ya kutoa machozi.

Hapo jana waandamanaji hao walifanya maandamano na kuimba nyimbo za kumlaani Rais Morsi pamoja na vuguvugu lake la kiislamu la Muslim Brotherhood.

Walikesha usiku kucha katika medani ya Tahrir mjini Cairo kuelezea hasira zao dhidi ya tangazo la rais wao anayezingatia itikadi za kiislamu Mohammed Morsi kujipatia madaraka makubwa.

Walikesha wakiimba nyimbo za kumlaani rais pamoja na vuguvugu lake la kiislamu la Muslim Brotherhood.

Jana Jumanne, maelfu ya waandamanaji walifurika katika medani hiyo wakiandaa mandamano kadhaa huku wakisema watamkiuka rais Mursi huku wakipinga mamlaka aliyojilimbikizia.

Maandamano mengine ya kumpinga rais Morsi yamefanyika katika maeneo mbali mbali nchini humo.

Bwana Morsi amejaribu kumaliza mzozo huo kwa kuahidi kuwa madaraka yake yatakuwa na kikomo.

Vuguvugu la Muslim Brotherhood, ambalo bwana Mursi ni mwanachama, liliakhirisha mkutano wao siku ya Jumanne likisema linataka kuzuia taharuki kutanda miongoni mwa wanachi.

Waandamanaji wanasema Rais na chama chake cha Muslim Brotherhood wanajipatia mamlaka kinyume na sheria

Lakini lilisema linauwezo wa kukusanya mamilioni ya watu wanomuunga mkono rais wao.

Wanaomuunga mkono bwana Mursi wanasema kuwa sheria hiyo inahitajika ili kulinda mafanakio yaliyotokana na mapinduzi ya kiraia dhidi ya utawala wa Mubaraka na idara ya mahakama ambayo ilikuwa na watu wanaomuunga mkono rais aliyng'olewa mamlakani.

Waandamanaji wanasema kuwa vuguvugu la Muslim Brotherhood limeyateka nyara faida zilizotokana na mapinduzi ya kiraia

MTOTO AMUUA MAMA YAKE MZAZI KWA NGUMI


 Akina mama waombolezaji wakisawazisha kaburi la marehemu Sinjembele Julius(62) aliyeuawa kwa kupigwa na mwanae Ndele Julius(25)


 Baadhi ya waombolezaji wakishuhudia mazishi ya Sinjembele yaliyofanyika Nyumbani kwake katika kitongoji cha Igawilo kata ya Swaya Mbeya


 Kaburi baada ya kuzikwa marehemu

Mkazi wa  Swaya jijini Mbeya Ndugu Ndele  Julius amemuua mama yake mzazi kwa kumpiga mateke na ngumi kisha kutoroka pasipo julikana Novemba 25 mwaka huu.

Tukio hilo limetokea majira ya saa 10 jioni nyumbani kwa mama huyo mara baada ya kutokea kwa ugomvi kati ya mtoto wake na kijana  mwingine hali iliyopelekea mama huyo kuingilia ndipo alipo kutwa na mauti huo.


Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi  Mkoani humo Ndugu Diwani Athumani amesema kuwa Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliokuwepo kati ya mtoto wake na kijana  mwenzake kitendo ambacho kilipelekea mama huyo kuingilia ugomvi huo .


Amesema wakati  mama huyo akijaribu kuamulia ugomvu huo mtoto wake alicha kupigana na mwenzake na kuanza kumshambulia mama yake kwa kumpiga ngumi na mateke mwilini.


Amesema mama huyo alifariki muda mchache kutokana na kupigwa sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababishiwa majeraha makuibwa yaliyopeleka kupoteza uhai wake.

Awali akizungumzia tukio hilo Mtoto wa Kwanza wa mama huyo Ndugu Razaro Mbwiga amesema kuwa mdogo wake alikuwa na tabia ya kugombana na mama yake marakwamara .

Hata hivyo teyari mwili huo umekwisha chukuliwa hospitali na kuzikwa ambapo katika maziko hayo Chama cha Muungano wa kijamii (Mujata) umewataka vijana kujiepusha na vitendo viovu kama uvutaji bangi na pombe za kienyeji kwani ndio chanzo cha kutokea kwa vurugu nyingi.

Wakazi Wa Mheza -Tanga, Wamlilia Sharo Millionea

Gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR alilokuwa akiendesha msanii wa filamu na muziki Hussein Ramadhani Mkieti ‘Sharo Millionea’ kutoka jijini Dar es salaam kuelekea Kijijini kwao Lusanga Wilaya ya Muheza  mkoa wa Tanga. Sharo Millionea alikufa papo hapo na mwili wake kuhifadhiwa Hospitali ya Teule Muheza Tanga.

Baadhi ya watu wakiliangalia gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR alilokuwa akiendesha msanii wa filamu na muziki Hussein Ramadhani Mkieti ‘Sharo Millionea’ kutoka jijini Dar es salaam kuelekea Kijijini kwao Lusanga Wilaya ya Muheza  mkoa wa Tanga. Sharo Millionea alikufa papo hapo na mwili wake kuhifadhiwa Hospitali ya Teule Muheza Tanga.


Gari aina ya Toyota Harrier lenye namba za usajili T 478 BVR alilokuwa akiendesha msanii wa filamu na muziki Hussein Ramadhani Mkieti ‘Sharo Millionea’ kutoka jijini Dar es salaam kuelekea Kijijini kwao Lusanga Wilaya ya Muheza  mkoa wa Tanga. Sharo Millionea alikufa papo hapo na mwili wake kuhifadhiwa Hospitali ya Teule Muheza Tanga.

Mbunge wa Jimbo la Muheza Hebert Mtangi akiwasili nje ya jengo la Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Hospitali ya Teule Muheza kwa ajili ya kushuhudia mwili wa msaniii Sharo Millionea aliyekufa katika ajali ya gari wakati akitoka Dar es Salaam kwenda Lusanga, Muheza mkoani Tanga, ajali hiyo imetokea katika kijiji cha Kijiji cha Songa Kibaoni .

Wakazi wa wilaya ya Muheza na maeneo mengine wakiwa wamefurika nje ya Chumba cha Maiti cha Hospitali Teule Muheza, kusubiri kushuhudia mwili wa Sharo Millionea, aliyefariki kwa ajali ya gari.

Washukiwa wa ICC Kenya kuunda Muungano


Uhuru Kenyatta ni mmoja wa washukiwa wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007

Washukiwa wawili wakuu wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya, Uhuru Kenyatta na William Ruto wanajadiliana kwa lengo la kuunda muungano wa kisiasa watakaotumia kugombea uongozi wa nchi.

Taarifa za awali zilisema kuwa wawili hao tayari wameunda muungano huo ingawa baadaye afisa wa mawasiliano wa vigogo hao alikana kuwepo makubaliano yoyote.

Na hataua ya wawili hawa inakuja wakati mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu ikiwa wanaweza kugombea uongozi wakati wanakbiliwa na tuhuma za kuhusikana ghasia za baada ya uchaguzi ambapo mamia ya watu waliuawa.

Wanasema wameamua kuunda muungano watakaoutumia kuwania nafasi ya rais na makamu wake katika uchaguzi mkuu mwaka ujao kama ishara ya kuwapatanisha wakenya.

Wanatarajiwa kufika mbele ya mahakama ya ICC baada ya uchaguzi mwaka ujao kujibu mashtaka ya kuhusika na ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008

Kenyatta ambaye ni naibu waziri mkuu na Ruto ambaye ni mbunge , wanasema kuwa muungano wao utakuwa wenye kauli mbiu ya kupigia debe umoja wa kitaifa, ustawi na kupatanisha wakenya .

Katika uchaguzi uliopita, wawili hao walikuwa pande pinzani. Na ulikuwa uchaguzi ulioshuhudia upinzani mkali zaidi katika historia ya Kenya.

Ulifuatiwa na ghasia za kikabila ambapo mamia ya watu waliuawa na maelfu wengine kuachwa bila makao mwaka 2007.

Wawili hao wamekanusha madai ya kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi hasa kupanga makundi ya watu walioshambulia makundi hasimu.

JICHO LETU KATIKA MAGAZETI NOVEMBA 28