‘Presha’ ya uchaguzi, ahadi zawatorosha wabunge Dodoma

 

 Bunge likiendelea katika Kikao cha tisa cha mkutano wa 11wa Bunge mjini  Dodoma jana.
 Picha na Edwin Mjwahuzi 
Na Sharon Sauwa


Dodoma. Baadhi ya wabunge wamesema kukosekana bungeni kwa wenzao wanaofikia 200 hata kuhesabiwa ni watoro, kumetokana na wengi wao kutokamilisha ahadi kwa wapigakura wao walizotoa mwaka 2010, hivyo kulazimika kukimbilia majimboni ili kujaribu kuzikamilisha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti bungeni hivi karibuni, walisema wengi wao bado hawajakamilisha ahadi walizoahidi walipoomba kura na sasa umefika mwaka wa uchaguzi.

“Wengine wamesafiri nje ya nchi kikazi. Si unajua hiki ni kipindi kigumu kwa sababu tunaingia kwenye uchaguzi. Wamekwenda majimboni kufanya maandalizi ya uchaguzi,” alisema Mbunge wa Mufindi Kusini (CCM), Mendard Kigora.

Alisema yeye yupo bungeni tangu Mkutano wa 19 ulipoanza kwa sababu ameshakamilisha ahadi zake kwa asilimia 90.

“Sina wasiwasi, nimekuja bungeni kuhakikisha nashiriki kutunga sheria zote, ili ‘next year’ (mwaka ujao) tuzisimamie vizuri. Sitaki muswada hata mmoja unipite,” alisema Kigora.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Christowaja Mtinda alisema wabunge wengi wako majimboni kwa sababu huu ni wakati wa lala salama na hawajakamilisha ahadi walizoahidi.

“Wapo majimboni kuwaweka sawa wananchi wao kabla ya uchaguzi hasa kwa upande CCM, wengine wako huko kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanapigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa,” alisema.

Alisema wabunge walio chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wana ratiba kila wanapokamilisha mikutano ya Bunge hurudi majimboni kwao kwa ajili ya kutekeleza ahadi zao.

“Sisi hatuko kama upande wa pili (CCM), hatusubiri hadi uchaguzi ukaribie. Tuna ratiba, tukitoka hapa tunakwenda moja kwa moja majimboni kukamilisha ahadi zetu,” alisema.

Mbunge wa Karagwe (CCM), Godbless Blandes alisema kuwa wabunge wengine wako katika kamati mbalimbali za Bunge wakijadili miswada itakayowasilishwa katika vikao vinavyoendelea.

“Miswada ni mingi inayoingia katika Bunge hili, kwa hiyo wakati mwingine unakuta wabunge wako katika kamati zao wakijadili miswada yao,” alisema.

Alisema wabunge wengine wana dharura za kuugua au majimboni mwao kuna kero hali inayowalazimu kwenda huko kuzitatua kabla ya kurejea tena kwenye vikao vya Bunge.

Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR Mageuzi), Moses Machali alisema wabunge wengi wana wasiwasi na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, hivyo wako majimboni.

“Presha imepanda, wako majimboni wanajitahidi kuweka mambo sawa kabla ya uchaguzi,” alisema.

Hata hivyo, alisema yeye hana wasiwasi kwani anajua wenye haki ya kumpa kura katika uchaguzi ni wananchi.

“Hakimu wa ubunge wangu ni mwananchi. Kama wanaona nilifanya vyema basi watanichagua tena, wao ndiyo wenye ‘kisu’ bwana wanaamua, nipite, nisipite ni sawa tu kwa kuwa mimi sina uamuzi wa mwisho,” alisema Machali.

Kukithiri kwa utoro kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano vinavyoendelea ilibainika hivi karibuni baada ya ofisi ya chombo hicho cha kutunga sheria kusema kuwa kina taarifa za wabunge 15 pekee walioomba ruhusa kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

Bunge hilo, linalotakiwa kuwa na wabunge 357, lilishindwa kupitisha miswada mitatu iliyohitaji theluthi mbili ya wabunge wa kila upande wa Muungano.

Wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa uliowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama wiki iliyopita kulikuwa na wabunge 81 ndani ya Ukumbi wa Bunge, jambo linalomaanisha kuwa takriban wabunge 250 hawakuwamo.

Hali ilikuwa mbaya zaidi wakati kikao cha Bunge hilo kilipoanza kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Silaha na Risasi kwani kulikuwa na wabunge 29 tu ukumbini.

Hali hiyo ilimaanisha kwamba zaidi ya wabunge 320 hawakuwamo ndani kujadili suala hilo nyeti kwa mustakabali wa Taifa.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema : “Wabunge 15 tu ndiyo wenye ruhusa, wengine wapo lakini wanaingia na kutoka bungeni. Kutokuwapo kwao kunaathiri sana wakati wa kupitisha miswada kutokana na kutotimia kwa akidi.”

Idadi ya wabunge walio na ruhusa ni ndogo ikilinganishwa na viti vingi vinavyokuwa vitupu wakati wa mijadala mbalimbali kwenye vikao vya Mkutano wa 19 vinavyoendelea mjini Dodoma.

Ofisi ya Bunge imeeleza kuwa jambo hilo linathiri shughuli mbalimbali za Bunge zinazotakiwa kufanyika.

Kaimu kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu anasema utoro wa wabunge unakwamisha mambo mengi ya msingi bungeni, huku akibainisha kuwa miswada haiwezi kupitishwa huku kukiwa na idadi ndogo ya wabunge na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka kanuni.

“Ukiingia bungeni unakuta ukumbi mtupu kabisa, lakini ukitoka nje unakutana na wabunge wengi wakizurura. Kanuni zinasema kuwa ili muswada upitishwe inatakiwa kuwe na wabunge walau nusu,” alisema Lissu.

Lissu alisema huenda kukosekana kwa wabunge hao kukawa kunachangiwa na Uchaguzi Mkuu, kwani wengi wamejikita majimboni.

“Pia wapo ambao wamekwenda safari za kibunge, lakini si wengi kufanya Bunge liwe tupu.”

Wabunge wengi hawaonekani bungeni, lakini wamekuwa vinara wa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii katika majimbo yao hasa kipindi hiki, kitu kinachoonekana kuwa ni kujiweka karibu na wananchi.

Wengi wanajishughulisha na kuchangia masuala ya maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu katika majimbo yao.

Mbali na kutoonekana bungeni kutokana na kujikita kuweka mikakati ya ushindi majimboni, baadhi ya wabunge pia wamekuwa watoro wa kuhudhuria vikao vya Bunge, kama wakionekana asubuhi, jioni ni nadra kuwaona.

Baada ya kujadili muswada wa Uhamiaji wiki iliyopita, Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohamed Habib Mnyaa aliomba mwongozo wa Spika kuhusu idadi ya wabunge kuwa ndogo.

Mbunge huyo alisema kwa idadi hiyo itakuwa kinyume na kanuni kama Bunge litapitisha muswada. “Ninavyofahamu ili tuweze kupitisha muswada huu wabunge tunaotakiwa kuwemo humu ndani ni kuanzia 176, lakini nikitizama idadi yetu hata 100 hatufiki, kutokana na suala hili naomba mwongozo wako,” alisema Mnyaa.

Akijibu suala hilo, Spika Makinda alisema: “Naona kuna watu wapo kwa ajili ya kukwamisha vitu tu. Haya tuendelee.”

Baada ya majibu ya Spika, idadi ya wabunge iliongezeka kidogo na kufikia 139.

Akizungumzia muswada huo, Lissu alisema itakuwa vigumu kupitishwa kwa sababu unatakiwa kupigiwa kura na theluthi mbili ya wabunge wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar.

“Sijui kama muswada huu utaweza kupita maana ukitizama idadi ya wabunge si rahisi kupata theluthi mbili kutoka Zanzibar na Tanzania Bara,” alisema Lissu. Licha ya idadi kuwa ndogo, mjadala uliendelea na hatimaye muswada huo ukapitishwa.

Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan alisema utoro huo hautoi picha nzuri kwa wananchi kwani wabunge ni wawakilishi wa wananchi na wanatakiwa kuhudhuria vikao vya Bunge.

Mbunge wa Songwe (CCM), Philipo Mulugo alisema: “Kukosekana kwa mbunge kuna sababu nyingi, wapo walioomba ruhusa kutokana na kuwa na sababu maalumu na pia wapo waliopo majimboni. Ila binafsi naona ushiriki wetu bungeni ni jambo muhimu.”

Tangu kuanza kwa vikao vya Mkutano wa 19 wa Bunge Machi 17 mwaka huu, idadi ya wabunge imekuwa ndogo ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge uliokuwa na mahudhurio makubwa kutokana na kujadili sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.

Katika mkutano wa 18 ulioisha Februari mwaka huu, wabunge wengi waliokuwa wakichangia hoja, walijikita katika kuzungumzia matatizo ya majimbo yao na kuacha mjadala uliokuwa mezani.

Jambo hilo lilimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwataka wajikite kwenye hoja za msingi na si kuzungumzia masuala ya majimbo

Mwendesha mashitaka auawa Uganda







  Askari akikagua gari ambalo lilikuwa likiendeshwa na Joan Kagezi

Watu wenye silaha wamemuua mwendesha mashitaka mkuu katika kesi ya watuhumiwa wa Kiislam wanaotuhumiwa kuua watu kadha katika mashambulio ya bomu mwaka 2010.

Mwendesha mashitaka huyo Joan Kagezi ambaye alikuwa kaimu mkurugenzi mwendesha mashitaka msaidizi nchini Uganda ameuawa kwa kupigwa risasi na watu waliokuwa katika pikipiki wakati akiendesha gari kurudi nyumbani mjini Kampala.

Kesi inayoendelea inawahusu watu kumi na watatu wanaotuhumiwa kuwa wapiganaji wa kikundi cha al-Shabaab.

Wanatuhumiwa kuua watu zaidi ya sabini wakati wakiangalia Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2010 katika mgahawa mmoja na katika uwanja wa klabu ya rugby.

Wiki iliyopita Marekani ilisema ilipata "habari za kuwepo uwezekano wa shambulio" katika maeneo ya mji ambayo raia wa mataifa ya magharibi wanakutana.

Serikali ya Uganda imesema Marekani ilionya juu ya uwezekano wa kuwepo kwa mtu anayejitoa mhanga akijaribu kuingia nchini humo.

Wagombea urais Nigeria mchuano ni mkali


Huku nusu ya matokeo katika uchaguzi wa rais nchini Nigeria yakiwa yametangazwa, mgombea kutoka chama kikuu cha upinzani, Muhammadu Buhari, anaongoza dhidi ya rais aliye madarakani, Goodluck Jonathan.

Lakini majimbo ya kusini yenye idadi kubwa ya watu kama vile Lagos na Rivers bado hayajatangaza matokeo na mwandishi wa BBC mjini Abuja amesema mchuano bado ni mkali.

Gwajima ajisalimisha polisi, atakiwa kwa DC

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima (katikati) akimsikiliza wakili wake, John Mallya (kulia) walipokuwa wakielekea Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam jana alikoitwa kwa mahojiano. Kushoto ni Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo, Yekonia Bihagaza. Picha na Venance Nestory 


Dar es Salaam. Wakati  Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akijisalimisha kwa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amemtaka aripoti ofisini kwake keshokutwa kutoa maelezo kuhusiana na tuhuma za kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini.

Juzi, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ilitoa amri kwa askofu huyo kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kutoa maelezo kuhusu tuhuma za kashfa na matusi dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Askofu Gwajima alitii amri hiyo na jana alifika kituoni hapo saa 8.15 mchana kwa ajili ya kutoa maelezo.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kwenda kutoa maelezo, Askofu Gwajima alisema Baraza la Maaskofu Tanzania, lilikubaliana kupinga Mahakama ya Kadhi lakini Askofu Pengo akawageuka..

“Tulikubaliana kwa pamoja kwamba hatutaki na viongozi wote tulisaini makubaliano hayo akiwamo Kardinali Pengo lakini tunashangaa alitugeuka,” alisema na kuongeza:

“Mimi kama kiongozi wa kiroho nilimkemea kiongozi mwenzangu wa kiroho.”

Alisema katika maneno aliyotoa hakuna neno lolote ambalo ni la kashfa...“yale yote ambayo nimeongea ni maneno kutoka kwenye Biblia. Kwa hiyo leo (jana) nimeshangaa kuitwa na polisi. Nilitarajia kama kuitwa angeitwa yeye (Kardinali Pengo),” alisema Askofu Gwajima na kuongeza kuwa, aliitikia wito huo ili kufahamu ni kwa nini ameitwa. Mapema wiki hii, mitandao mbalimbali ya kijamii, ilisambaza sauti ya Askofu Gwajima akitoa maneno makali ya kumkashifu Kardinali Pengo.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema: “Taratibu za mahojiano zimeanza kwa mujibu wa sheria na mtuhumiwa  atapewa haki zote anazostahili kama vile kuwa na ndugu na rafiki yake wa karibu anayemwamini au wakili wake.”

Akizungumzia kuhusiana na tuhuma zinazomkabili Askofu Gwajima, Kova alisema ni pamoja na kumkashifu na kumtukana hadharani Kardinali Pengo.

Kuitwa kwa DC Kinondoni

Katika hatua nyingine, Makonda amemwandikia barua Askofu Gwajima akimtaka kufikia ofisini kwake kutoa ufafanuzi juu ya maneno makali dhidi ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki.

Katika barua yake, Makonda alisema ofisi yake inataka kufahamu kama uhuru wa kuabudu kikatiba ni kutokuheshimu watu wengine. “Hatuamini kama imefika wakati kwenye nyumba za ibada kumegeuka sehemu ya kutukana na kuwasema watu badala ya kuhubiri habari njema. Tunataka kujidhihirisha malengo hasa ya kutumia maneno hayo ni nini.”

Hesabu za uandikishaji BVR zinagoma

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge, mjini Dodoma jana. 
Picha na Anthony Siame. 


Dar/Dodoma. Licha ya Serikali kusisitiza kuwa uandikishaji wa wapigakura nchi nzima kwa mfumo wa BVR utakamilika Aprili 28 na Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa, hesabu zilizopigwa na Mwananchi zinakataa kuwianisha siku zilizosalia na idadi ya mashine za BVR zilizopo na zinazotarajiwa kuwasili. Hali hiyo imejitokeza zikiwa zimebaki siku 36 kabla ya Kura ya Maoni kufanyika, huku kukiwapo wasiwasi miongoni mwa wadau kuhusu uwezekano wa kufanikisha matukio hayo bila manung’uniko.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa uandikishaji nchi nzima utaanza siku sita kuanzia leo na kusisitiza kuwa Kura ya Maoni kuridhia au kukaa Katiba Inayopendekezwa itafanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa.

Wasiwasi wa kutofanyika kwa kura hiyo katika tarehe iliyopangwa unatokana na uandikishaji wa wapigakura kwa BVR unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ulioanza Februari 23, mwaka huu kutokamilika hata katika mkoa mmoja wa Njombe, wenye wapigakura 392,634 kati ya milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa nchini kote.

Hesabu zinavyokataa

Kulingana na takwimu za NEC, BVR moja inaandikisha kati ya wapigakura 80 hadi 100 kwa siku endapo hakuna tatizo lolote, hivyo kwa kadirio la chini, iwapo BVR 7,750 zilizoagizwa na NEC zitawasili nchini kwa mafungu, zitahitajika siku 38 kuandikisha wapigakura milioni 24 wanaokusudiwa kama kazi hiyo itaanza leo.

Hata hivyo, katika uandikishaji wa majaribio na baadaye katika Mkoa wa Njombe mashine hizo zimeripotiwa kukabiliwa na changamoto mbalimbali ama za kukwama, weledi mdogo wa watumiaji na hali ya hewa, hivyo kufanya idadi iliyokusudiwa kutokamilika.

Mwandishi wa Mwananchi, Kizzito Noya aliyekuwa Makambako, Njombe wakati wa uandikishaji hivi karibuni amesema kwa wastani alishuhudia mashine moja ya BVR ikiandikisha wapigakura 60 kwa siku, idadi hiyo ikilinganishwa na watu 24,000,000 wanaokusudiwa kuandikishwa kwa BVR 7,750 nchi nzima, shughuli hiyo itachukua siku 52, wakati siku zilizosalia hadi Kura ya Maoni ni 36.

Jambo jingine linalofanya hesabu hizo kukataa ni kitendo cha mashine hizo 7,750 za BVR zilizokusudiwa, kutokuwapo zote nchini hadi sasa, licha ya NEC kusema mara kwa mara kwamba zitawasili wakati wowote.

Jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hata awamu ya kwanza ya mashine 3,100 za BVR bado ziko njiani.

Iwapo mashine hizo pekee zitafika na kutumika kuandikisha wapigakura hao milioni 24 zitahitajika siku 97 kukamilisha shughuli hiyo.

Mchakato huo ulianza kusuasua tangu wakati majaribio yaliyotumia BVR 250 katika majimbo ya Kilombero, Morogoro; Kawe, Dar es Salaam na Milele mkoani Katavi na baadaye katika Mji wa Makambako na mkoa mzima wa Njombe.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa mashine hizo 250 zimekuwa hazitumiki zote kwa kuwa baadhi zinatumika kutoa mafunzo kwa waandikishaji watakaofanya kazi hiyo nchi nzima.

Changamoto nyingine inayokwamisha shughuli hiyo ni ukata, kwa kuwa Serikali haijatoa fedha za kutosha kufanikisha shughuli hiyo, jambo ambalo limethibitishwa na Pinda kuwa fedha zilizotolewa hadi sasa ni asilimia 70 ya kiwango kilichotarajiwa.

Kauli ya Lubuva

Jaji Lubuva alisema: “Tuliamua kuanza na Njombe kutokana na BVR 250 tulizonazo kutosha katika mkoa huo wenye kata 99. Tunasubiri nyingine 7,750 kuwasili wiki ya kwanza hadi ya pili ya mwezi ujao zikitokea China.”

Alisema uandikishaji Njombe unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika Aprili 12, kama ilivyopangwa.

Kuhusu uwezekano wa kura ya maoni kufanyika Aprili 30, alisema: “Kazi ya msingi kabla ya shughuli yoyote ni kuandikisha daftari la wapigakura, hivyo kama tarehe itafika bado hatujamaliza nitawaeleza, lakini mpaka sasa bado tarehe ya Aprili 30 haijabadilishwa.

“Vifaa 3,100 kati ya 7,750 viko njiani na vitakapowasili tutatangaza ratiba, tutaanza na mikoa gani na Njombe kweli wamehamasika kwani wamejitokeza kwa wingi na sisi kama tunaona hatujamaliza licha ya ratiba kututaka kuhama tunaongeza siku ili kuhakikisha kila mmoja anaandikishwa sasa mimi sielewi hao wanaosema kwamba uandikishaji unakwenda sivyo hata huko bungeni sielewi wana maanisha nini.”

 Oktoba 22 mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete alipokutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika Jamhuri ya Watu wa China, aliwaeleza kwamba kura hiyo itafanyika Aprili mwaka huu.

Matumaini ya Pinda

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge jana, Pinda alisema uandikishaji utaanza siku sita kuanzia leo na Kura ya Maoni kuridhia au kukaa Katiba Inayopendekezwa itafanyika Aprili 30, mwaka huu.

Alisema utoaji wa elimu kwa umma sambamba na kampeni za kuiridhia au kuikataa Katiba hiyo, vinaweza kufanyika wakati uandikishaji ukiendelea. Waziri Mkuu alisema Serikali imeshalipa asilimia 70 ya fedha kwa kampuni inayosambaza mashine hizo.

“Tukianza uandikishaji nchi nzima ndiyo tutaona changamoto zaidi zipo wapi na zinaweza kutupeleka katika uamuzi wa aina gani. Ila hilo litakuwa jukumu la Tume (NEC), sisi kazi yetu ni kuhangaika ili BVR zinazotakiwa ziwe zimepatikana kwa wakati,” alisema Pinda.

Akizungumzia muda wa kampeni wa siku 30 kabla ya Kura ya Maoni Pinda alisema: “Tume ndiyo inaweza kulizungumzia suala hilo kiundani. Unajua inatakiwa mpaka kufikia Aprili 28 mambo yote yawe yamekamilika na siku mbili baadaye (Aprili 30) ndiyo siku ya kura. Kama wanasema mwezi mmoja ni sawa, tunaweza kuendelea na mambo mengine huku elimu ikitolewa kwa wananchi.”

Alipoulizwa juu ya changamoto zilizojitokeza mkoani Njombe alisema Serikali iliamua kuanza uandikishaji mkoani humo ili kupata uzoefu kutokana na hali ya jiografia ya mkoa huo.

“Tulichojifunza ni kwamba katika maeneo ya mijini,  tukianza uandikishaji nchi nzima ni lazima maeneo kama hayo tuyape nafasi kubwa zaidi tofauti na vijijini,” alisema.

Alisema maeneo ya mijini lazima mashine za BVR ziwe nyingi zaidi kuliko maeneo ya vijijini kwa sababu ya idadi ya watu.

Alisema katika Mkoa wa Njombe zilipelekwa mashine za BVR 250 lakini hazikutumika zote.

“Tumetenga siku saba kwa kila kata kwa ajili ya uandikishaji nadhani zinatosha na kila kata tutaweka mashine za BVR mbili hadi tatu,” alisema Waziri Mkuu.

Aliongeza: “Mashine hizo zinatosha kabisa. Kwa uzoefu tulioupata pale Njombe hatuoni tatizo hata kidogo kwamba tunaweza kushindwa kuandikisha wananchi na kutofikia malengo tuliyoweka. Zinatosha kwa sababu leo wanaweza kuandikishia kituo kimoja na watu wakiisha wanahamia kituo kingine. Kata ina vijiji vinne hadi vitano na kila kijiji kina kitongoji kati ya vinne hadi vitano, hivyo muda wa siku saba unatosha kabisa.”

Juzi, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba mwongozo bungeni akiitaka Serikali itoe majibu ya kueleweka juu ya hatima ya uandikishaji wa wananchi katika daftari la Wapigakura ulioanzia Mkoa wa Njombe na iwapo Kura ya Maoni itafanyika Aprili 30.

Alisema kuwa muda uliobaki ni ndoto kwa Serikali kukamilisha uandikishaji huo nchini nzima, akitoa mfano kwamba ili wananchi wa Mkoa wa Njombe waweze kuandikishwa wote, uandikishaji unatakiwa kuongezwa muda hadi Aprili 28 na Spika alimjibu kuwa Serikali ingetoa maelezo.

Warioba: Tunahitaji rais mzalendo


Jaji Joseph Warioba 


Aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Jaji Joseph Warioba, ametaja sifa za rais ajaye kuwa ni uzalendo, uadilifu na dira katika kuliongoza taifa.

Jaji Warioba alisema hayo juzi, katika Kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa hewani na ITV.

“Rais anapaswa pia kujua matatizo ya Watanzania, awe mzalendo, mwadilifu na aone mbali. Anapaswa pia kujua  atafanya nini kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta za afya na uchumi,” alisema.

Kwa kauli hiyo, Jaji Warioba anaungana na viongozi wengine kadhaa waliowahi kuzungumzia sifa za rais ajaye, akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Hassy Kitine; Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye; Mwanasiasa mkongwe, Cleopa Msuya; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba;  na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao walitaja sifa hizo za rais ajaye kuwa ni uadilifu, busara, uzalendo, uwezo wa kufanya uamuzi na kuyasimamia, weledi wa masuala ya maendeleo, kutokuwa na makundi, kuwa na nguvu ya mwili na akili na uwezo wa kusimamia Katiba na sheria za nchi.

Walisema yeyote asiyekuwa na sifa hizo, hafai kuwa rais na kuwaongoza Watanzania.

Dk Kitine: Urais siyo lelemama

“Mtu anayetangaza (mwenyewe) kuwa anataka kuwa rais anakuwa hajui anachokisema..., anakuwa hajui matatizo ya urais. Mtu asiyejua matatizo ya urais anaweza kujisemea tu kwa sababu haelewi urais maana yake ni nini,” alisema aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa na Waziri wa kwanza wa Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Dk Hassy Kitine.

Kitine alisema hayo Septemba 9 mwaka jana. Alisisitiza, “Mtu anayejua maana na changamoto za urais hawezi kutangaza anautaka urais. Ataogopa kwa sababu ya changamoto (nyingi) za urais…, kwa hiyo hawezi kujitangazia ovyo kuutaka.”

 Kwa mujibu wa Dk Kitine anayetaka kuwa rais lazima awe mwadilifu wa asili na siyo wa kujifanya. Awe pia mzalendo na mwenye uwezo wa kufanya uamuzi.

“Rais awe amesoma na asiwe na kundi, pia ajue misingi ya utawala bora, utawala wa sheria na aonekane kuwa anachukia rushwa kwa vitendo. 

Kauli ya Msuya

 Mwezi huohuo wa Septemba mwaka jana, mwanasiasa mkongwe nchini, Cleopa Msuya, alitaja sifa 16 za rais ambazo ni pamoja na uadilifu, uzalendo, mpambanaji dhidi ya rushwa na ufisadi na mwelewa na msimamizi wa uchumi.

Sifa nyingine kuwa na shauku ya ustawishaji wa uchumi na uelewa wa kujua umuhimu wa kujenga na kusambaza huduma za miundombinu ya kiuchumi na kijamii. Pia rais anapaswa awe ni mtu mwenye kujua umuhimu wa watu kufanya kazi, uwezo wa kuwatetea na kukomesha unyanyasaji wa wananchi ndani ya nchi yao, uwezo wa kuelewa misingi ya uchumi wa taifa na uwezo wa kufumua maovu yanayofanyika.

Awe pia mnyenyekevu na mapenzi kwa taifa na wananchi,  awe na uwezo kuongoza na kuona mbele, awe na uwezo wa kutofautisha mambo ya nchi na binafsi, aweze kutofautisha mambo ya biashara na mali za umma, kutofautisha mambo ya ofisi na nyumbani na pia awe na uwezo wa kusimamia na kuwezesha wananchi katika uchumi.

Lowassa: Siwezi kuzuia mafuriko kwa mikono


 

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuwazuia wananchi kwenda nyumbani kwake kumshawishi agombee urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mkono.

Lowassa alitoa kauli hiyo nyumbani kwake mjini Dodoma jana wakati alipotembelewa na kundi jipya kutoka Mbarali mkoani Mbeya waliokwenda kumshawishi atangaze nia kugombea urais.

Lowassa ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kusema kuwa kwa kuandaa makundi ya kumshawishi, mbunge huyo wa Monduli anajua adhabu yake na anaweza kupoteza sifa za kuwa mgombea urais kupitia CCM.

“Sasa mmekuja siku mbaya kwa sababu jana kuna watu wamesema maneno mengi mabaya ambayo kwa malezi yangu mimi mambo ya chama humalizwa kwenye vikao vya chama na siyo kwenye vyombo vya habari. Mnazungumza, mnaelewana mnatoka pale,” alisema.

“Na utaratibu huu ulioanzishwa na watu, mimi ni vigumu kuuzuia, utazuiaje mafuriko kwa mikono? Mafuriko yanakuja halafu nazuia kwa mikono nitaweza kweli? Hawa watu sina hoja nao, sina cha kuwaambia,” alisema.

Mambo ya chama

Lowassa ambaye hivi karibuni aliweka bayana kuwa ameshawishika kuwania nafasi hiyo, alisema, “Lakini mambo ya chama hayawezi kuwa kwenye ma-TV, magazeti na maredio, mara huyu hivi, mara huyu vipi. Mkiona chama kinakwenda kwa utaratibu huo, ni hatari sana, CCM ninayoijua mimi ni ya vikao.”

Alisema hakusudii kujibu hizo hoja (za Nape) bali rafiki yake Hussein Bashe amezielezea vizuri.

“Niseme mawili tu yanayonisikitisha wanasema eti nawaiteni, nakupeni fedha, mimi hela natoa wapi? Lakini kibaya zaidi nikiweka maturubai hapa ni kosa, mkiwa na viti hapa ni makosa? Na wanasema nawapeni chakula mambo ya ajabu sana na yanasemwa na watu wazima wenye heshima

zao,” alisema Lowassa na kuongeza:

“Juzi walikuwapo vijana 300 hapa, nitawapikia chakula nitawaweza? Nyie kwa wingi huu mtaenea hapa? Lakini ni vibaya unamdhalilisha binadamu mwenzako kuwa maisha yake yote ni kufikiria tumbo. Hamna cha kufikiri isipokuwa tumbo, kwa hiyo mnakuja hapa kwa sababu mnataka Lowassa awapeni chakula, ni kudhalilisha watu.”

Alisema watu wanaofika nyumbani kwake wanafanya hivyo kwa utashi, hiari na gharama zao wenyewe na wengine yeye hawafahamu kabisa.

Lowassa alisema hajawahi kuwaona, wala kuwatuma kufanya hivyo au kuwaomba kufika nyumbani kwake watu ambao wanamshawishi kutangaza nia ya kugombea urais.

Ushauri wa Kikwete

Aliwashauri wengine ambao hawajafika wasubiri chama kiseme nini kifanyike kwa watu wanaotaka kuja kunishawishi.

“Kwa sababu Rais (Jakaya Kikwete), alivyokuwa Songea kule na mimi nilikuwapo kule akasema mkiona hawa hawatoshi muda upo bado washawishini wengine waingie, sasa mkifanya hivi ni kosa, ni kampeni.

Ipi si kampeni sasa? “alihoji Lowassa na kuongeza:

“Nawashauri tusiingize mgogoro kwenye chama tungoje tupate maelekezo, mimi nina uhakika kuwa tutapata nafasi. Hakika ipo siku Watanzania watapata uhuru wa kusema juu ya mtu mimi. Watapiga kura zao kusema naam ama hapana. Kwa hiyo tungojee siku. Nami nina hakika wako Watanzania wengi wanaonipenda.”

Lowassa alisema, “Kwa hiyo huyo anayepiga kelele nyingi sijui tutoke chama, sijui tufanye nini? Angojee wanachama wa CCM na wananchi waamue. Mimi ni mwanademokrasia, ninaamini kwenye demokrasia lakini pia kwenye utendaji bora.”

Lowassa, ambaye bado anatumikia kifungo cha mwaka mmoja kutoka chama chake aliwataka watu hao kujiandikisha kwa wingi na kupiga kura kwa mtu ambaye wanaamini ataweza kuwaongoza kwa kutoa maamuzi magumu na makubwa kwa faida ya nchi.

Juzi, Nape alisema kitendo cha makundi ya watu kwenda kumshawishi Lowassa atangaze nia ya kuwania urais ni kinyume cha Katiba ya CCM.

Alisema kitendo hicho ni kampeni ya wazi ya urais anazoendelea nazo kabla ya muda kufika na kuonya kama ataendelea atapoteza sifa za

kugombea nafasi ya urais.

Katika kipindi cha wiki mbili sasa kwenye makazi yake Monduli mkoani Arusha na Area C mjini Dodoma makundi ya watu mbalimbali yamekuwa yakifika kumshawishi agombee urais baadaye mwaka huu.

Askari wawili mbaroni kwa fedha bandia

 
 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo akionyesha sare za jeshi la wananchi zilizokamatwa kutoka kwa askari polisi baada ya kupekuliwa nyumbani kwake. 
Picha na Faustine Fabian 

Jeshi la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia askari wawili wa magereza na polisi kwa kukutwa na noti bandia ikiwa pamoja na sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Charles Mkumbo alisema askari hao walikamatwa juzi saa tisa mchana katika Mtaa wa Old Maswa, Kata ya Nyakabindi, wilayani Bariadi.

Alisema askari hao walifika kwenye kibanda cha Mpesa kinachomilikiwa na Mwalimu wa Shule ya Sekondari Old Maswa, Kassian Luhende (29) wakiwa na pikipiki aina ya Sunlg kwa lengo la kuweka fedha hizo katika simu.

Alisema baada ya mwalimu huyo kupokea noti 10 zenye thamani ya Sh100,000 alizitilia shaka na kuamua kuzikagua zaidi ndipo alipogundua kuwa siyo fedha halali.

Mkumbo alisema mwalimu huyo baada ya kugundua hilo aliomba msaada wa kukamatwa kwa askari hao. Alisema majirani walipofika walihoji, ndipo mmoja wao alipotoa kitambulisho kuwa yeye ni askari na mwingine kujitambulisha kuwa ni dereva bodaboda.

Alibainisha kuwa baada ya wananchi kuambiwa hivyo waliwatilia shaka zaidi na kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Bariadi na kisha kukamatwa.

Mkumbo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni askari mwenye namba H 2420 PC Seleman Juma (25) ambaye ni wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Simiyu, na mwenye namba B.6499 WDR Edmund Masaga (28) wa Magereza wilayani Bariadi.

Kamanda Mkumbo alieleza kuwa, baada ya askari hao kukamatwa mmoja wao PC Selemani alipopekuliwa katika mfuko wa suruali yake, alikutwa na noti nyingine za bandia za Sh100,000.

Mbali na hilo Mkumbo alisema askari huyo alipopekuliwa nyumbani kwake alikutwa na sare za JWTZ ambazo ni kaptula nne, fulana mbili, kombati moja pamoja na kitambaa.

Alisema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa usambazaji wa noti bandia ndani ya mkoa na kwamba baada ya uchunguzi kukamilika askari hao watachuliwa hatua za kinidhamu pamoja na kisheria.

Baba mbaroni kwa kuwabaka watoto wake

 

Rahma Mashamu ambaye ni mama mzazi wa watoto wawili mmoja wa miaka 11 na mwingine 15 wanaodaiwa kubakwa na baba wa watoto hao akilia kwa uchungu wakati akihojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo, wilayani Kibaha mkoani Pwani. Picha na Julieth Ngarabali 


Mkazi mmoja wa Miembe Saba wilayani Kibaha mkoani Pwani amekamatwa na polisi akituhumiwa kuwabaka watoto wake wawili wadogo kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Habari zilizolifikia gazeti hili, zilisema kuwa katika tukio hilo ambalo limethibitishwa na polisi na watoto wenyewe, baba huyo alianza kuwafanyia binti zake vitendo hivyo mwaka 2013 kwa siku ambazo mkewe ambaye nimama wa wasichana hao hakuwapo hadi usiku wa Machi 19, mwaka huu. Kwa sasa tunayahifadhi majina ya familia hiyo.

Watoto hao mmoja mwenye umri wa miaka 15 anayesoma darasa la saba na mdogo wake mwenye umri wa miaka 11 aliyeanza kubakwa akiwa darasa la tatu.

Kwa mujibu wa watoto hao, baba huyo alikuwa anamuita mmoja wa watoto wake chumbani kwake na kumtaka alale na mdogo wao wa kiume wakati huo akiwa na mwaka mmoja na binti akipitiwa na usingizi humvua nguo za ndani na kumwingilia huku akimtaka kukaa kimya na kuvumilia maumivu.

Mke wa mtuhumiwa huyo, ambaye amekuwa akizimia mara kwa mara kutokana na kulia baada ya kubaini mchezo huo, alisema aligundua watoto wake wanabakwa Ijumaa iliyopita baada ya mmoja wa mabinti zake hao kumweleza kuwa baba yake alikuwa amembaka Machi 19, mwaka huu.

Alisema kabla ya binti huyo kumweleza hivyo, alimwomba asimpige kwani kuna kitu anataka amweleze, japo ni kibaya lakini yeye amechoshwa na kimekuwa kikimuumiza kichwa.

“Alisema kila ninapokwenda katika biashara zangu, anatamani nisiwe ninawaacha hapo, nikamwahidi sitamfanya kitu ili mradi aseme ukweli tu,” alisema mama huyo.

Baada ya kuhakikishiwa kulindwa, ndipo binti huyo aliposimulia jinsi ambavyo baba yake amekuwa akiwafanyia na kuwatishia wakipiga kelele atawaua.

“Niliposikia mwili ulisisimka na ghafla binti yangu mwingine naye akatokea akilia na kuniambia, ‘hata mimi baba ananifanyiaga hivyohivyo kila siku unapokuwa umepeleka mboga sokoni Kariakoo,” alisema mama huyo.

Mwanamke huyo ameomba sheria ichukue nafasi yake katika tukio hilo kwa kuwa ni la kinyama na pia wataalamu wa saikolojia wamsaidie binti yake mdogo wa darasa la tano kwani yeye ameathirika zaidi.

Daktari aliyewapima watoto hao, ameshauri binti huyo mdogo apate ushauri zaidi ili kurudisha akili yake katika hali ya kawaida.

 Simulizi za watoto

Wakizungumza nyumbani kwao jana watoto hao, walisema baba yao alikuwa akiwatishia kuwakatakata kwa panga au kuwakaba koo humohumo chumbani endapo wangethubutu kumweleza mtu yeyote kitendo wanachokifanya.

“Tulikuwa tumeingia kwetu kulala na wadogo zangu, nikasikia ananiita nikambembeleze mtoto eti anamsumbua, nilikwenda nikambembeleza  akalala, wakati nashuka kitandani kurudi chumbani kwetu baba akanivuta kwake akanivua, akasema anachokifanya ni suna kwa hiyo hataki kelele, akisikia atanikaba nife.”

“Niliumia sana na asubuhi mama alirudi nikajitahidi kweli asijue na hata shule sikwenda, jioni mama aliondoka tena baba hakuniita siku hiyo lakini baada ya siku tatu aliniita tena ikawa vilevile navumilia. Siku zilivyozidi unaweza kukuta kwa wiki naitwa hata mara nne siku ambazo mama hayupo nyumbani,” alisema.

Watoto hao walieleza kuwa baadaye baba huyo alihamia kwa binti mdogo kwa staili ileile na kila mmoja alikuwa akiitwa kwa zamu na kwa vile kila mmoja alijua ni siri yake na baba. Kutonaka na woga wa kuuawa, hakuna aliyemweleza mwenzake hadi katikati ya mwaka jana mmoja wao alipomweleza mwenzake na baadaye kumweleza mama yao.

“Baba alikuwa anasema atatuua bila hata mtu kujua na tutaozea shambani, hata nikiwa katika siku zangu baba ananiingilia hivyohivyo, naugua kila mara UTI, mdogo wangu naye kila mara UTI, tukaamua liwalo na liwe kama kufa basi ila mama ajue,” alisema mtoto huyo huku akibubujikwa na machozi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembe Saba, Hamis Shomari alisema kabla ya kupelekwa kituo cha polisi Kongowe Jumamosi iliyopita, watoto hao waliitwa shuleni hapo na kuhojiwa kila mmoja peke yake na wote walikiri kuanza kubakwa mwaka 2013 na baba yao na kwamba tabia hiyo iliendelea hadi Machi 19 usiku alipobakwa binti mdogo kwa mara ya mwisho na Machi 20 walipoamua kumweleza mama yao.

 Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema wanamshikilia mtuhumiwa huyo na kwamba wasichana hao wamefanyiwa vipimo mbalimbali na majibu ya daktari yamethibitisha kuwa wamebakwa na sehemu zao za siri  zimeharibiwa, hivyo wanaendelea na matibabu.

JK kuzindua studio za Azam

 

Studio za Azam Tv 



Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete leo anazindua studio za kituo cha televisheni cha Azam zilizopo Tabata jijini hapa.

Naibu Ofisa Mtendaji wa Azam, Tido Mhando alisema jana kuwa mwitikio wa Rais kwa ajili ya shughuli hiyo ni faraja kubwa.

Mhando alisema viongozi mbalimbali wa dini na Serikali pia wanatahudhuria kwenye uzinduzi huo kuanzia saa tatu asubuhi.

Mhando ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication, alisema kuzinduliwa kwa studio hiyo ya kisasa kutaleta chachu ya mabadiliko katika tasnia ya habari.

“Hapo nyuma tulikuwa tukilega lega kwa kiasi fulani, lakini tunaamini uzinduzi huu utaamsha ari ya ushindani katika tasnia ya habari,” alisema huku akimwagia sifa studio hiyo kuwa inaweza kuwa bora kuliko zote Afrika Mashariki.

Alisema studio hiyo ambayo ujenzi wake umegharimu Dola 31 milioni za Marekani, (sawa na Sh55 bilioni), itapanua wigo wa kurusha matangazo na vipindi bora vitakavyohabarisha umma.

“Baada ya uzinduzi huu tunatarajia kuongeza studio nyingine mbili zitakazokuwa ndani ya hii kubwa,” alisema Mhando.

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa kampuni hiyo, Yahaya Mohamed alisema ubora wa studio hiyo utaendana na ubora waandishi wao.

Mohamed ambaye aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya Sahara Media Group alisema uwekezaji huo utafungua milango kwa waandishi.

“Tutakuwa tunapokea kazi za waandishi wengine, lakini jambo la kuzingatia ni ubora wa kazi yako,” alisema Mohamed.

Upinzani, Tume watofautiana uandikishaji Zanzibar


Zanzibar. Wakati Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), ikitangaza siku mbili kwa kila kituo kuanza uandikishaji wa wapiga kura wapya baada ya Kura ya Maoni, vyama vya siasa vimedai muda huo hautoshi kulinganisha na mahitaji makubwa ya wananchi kujiandikisha kupiga kura.

Mkuu wa Divisheni wa Zec, Idrisa Haji Jecha alisema mjini Unguja juzi kuwa kila kituo kimepangiwa kutumia muda huo kuandikisha wapiga kura, hasa wale waliofikia miaka 18 na ambao hawakupata nafasi kwa sababu mbalimbali.

Jecha alisema matayarisho ya kazi hiyo yamekamilika, ikiwa ni pamoja na Zec kuagiza vifaa vya kisasa kufanikisha kazi hiyo.

“Kila kituo kitaandikisha wapiga kura wapya kwa siku mbili, tunategemea kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa na uchaguzi utakuwa wa kisayansi,” alisema Jecha.

Alisema ratiba ya Uchaguzi Mkuu imekamilika na kwamba utafanyika Oktoba 25, uteuzi wa wagombea nafasi za urais, ubunge, uwakilishi na udiwani utakuwa Agosti 17 na kampeni zitaanza Septemba 7 hadi Oktoba 24.

Kiasi cha Sh7.1 bilioni zitatumika kufanikisha uchaguzi Zanzibar, mbali na michango ya mashirika ya maendeleo ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa Chama cha Wananchi (CUF), Omar Ali Shehe alisema muda uliowekwa na Zec hautoshi na ameshauri tume kuuongeza.

“Kuna idadi kubwa ya watu hadi sasa hawajapewa vyeti vya kuzaliwa na wengine hawana vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, nadhani muda hautatosha,” alisema Shehe.

Alisema kimsingi, idadi ya wapiga kura wapya ni wengi Unguja na Pemba, hivyo kuna kila dalili wapiga kura wapya watakosa fursa hiyo.

“Tungependa kuona wananchi wanapata muda wa kutosha kujiandikisha kutokana na hamasa kubwa waliyonayo kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu,” alisema Shehe.

Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatib alisema ili kuondoa malalamiko na mivutano, kuna haja kwa Zec kuongeza muda wa uandikishaji.

Khatib alisema kutokana na mwamko uliopo sasa, siku zilizotangazwa ni chache na wengi wanaweza kubaki bila kuandikishwa kama muda hautaongezwa.

Kuhusiana na suala la baadhi ya watu kukosa vyeti vya kuzaliwa au vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, alisema linaweza kuleta migongano.

“Kwanza muda uliotolewa na Zec hautoshi, lakini pia unawanyima wananchi wengi kupata fursa ya kujiandikisha. Ni vizuri suala la vitambulisho likamalizwa kwanza, ndipo kazi ya uandikishaji wapiga kura ifanyike,” alisema Khatib.

Wanne wahukumiwa kunyongwa kwa kuua albino Tanzania

 

Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mlemavu wa ngozi, Zawadi Magimbu (32) wakiwa ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita baada ya kuhukumiwa kunyongwa. Kutoka kushoto ni Nasoro Charles, Singu Siantemi, Masaru Kahindi na Ndahanya Lumola. Picha na Jackline Masinde.      


Geita/Dar. Watu wanne wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na kosa la kumuua Zawadi Magindu (32) mwenye ulemavu wa ngozi, mkazi wa Kijiji cha Nyamaruru, Wilaya ya Geita mkoani hapa.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Joacquine De-Mello wa Mahakama Kuu, ambaye alisema alisema Mahakama imeridhika pasi na shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kwamba walihusika moja kwa moja na kifo hicho.

Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Nassoro Charles mkazi wa Kijiji cha Beda mkoani Kagera, Masaru Kahindi mkazi wa Kijiji cha Nyamaruru, Ndahanya Lumola na Singu Nsiantemi wakazi wa Kijiji cha Kakoyoyo, Wilaya ya Bukombe.

Jaji De-Mello alisema washtakiwa walifanya kosa hilo Machi 11, 2008 saa 1:00 usiku nyumbani kwa akina Zawadi wakati wakipata chakula cha usiku, walimkata kwa shoka na panga miguu yote na mkono wa kulia.

Alisema Masaru Kahindi aliyekuwa jirani na Zawadi, Nassoro Charles aliyekuwa mume wa marehemu walivamia nyumbani kwao wakati wanapata chakula cha usiku, huku wakiwa na panga na shoka kisha kumkata miguu na mkono wa kulia .

“Watu hao walikwenda na shoka na panga, walitumia shoka kumkata Zawadi huku mama yake Magdalena Mashimba na mjukuu wake, Semen Hamisi wakipigwa na kutupwa nje na wauaji hao,” alisema Jaji De-Mello.

Aliendelea kusema kuwa, wakati wanamkata Zawadi, mtoto wake Semeni alijibanza mlangoni na kuwatambua wauaji hao kuwa mmojawapo alikuwa mume wa mama yake na mwingine jirani yao.

“Walionwa na shahidi Magdalena na Semeni waliwatambua kwa sauti na mwonekano, kwani wakati wanafanya hivyo kulikuwa na mwanga wa mbalamwezi,” alisema.

Pia, Jaji De-Mello alisema washtakiwa Ndahanya na Nsiantemi walikuwa wafanyabiashara wa viungo vya albino, walikamatwa na polisi baada ya kutegewa mtego.

“Polisi walikuwa kwenye operesheni ya kuwatafuta watu wanaojihusisha na vitendo vya kuua albino, walipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna watu wanataka viungo vya albino ndipo walipotafuta albino wawili, mmoja akiwa mtoto na mwingine mtu mzima,” alisema.

Alisema baada ya kutegwa mtego huo walikamatwa washtakiwa wawili; Ndahanya na Nsiantemi ambao walikiri kuhusika na mauaji ya Zawadi na kuchukua viungo hivyo, kisha kuvipeleka kwa mganga wa jadi, Mussa Ally mkazi wa Katoro ambaye alihusika kuvipima ili kujua iwapo vina ubora.

“Wakati watu hawa wanahojiwa na polisi waliwataja wenzao wengi ambao hapa mahakamani hawapo sijui ni kwa nini… wakiongozwa na Robert Kagoma ambaye ndiye alikuwa wakala wa kulangua viungo hivyo na kuvipeleka kwa mganga wa jadi aliyetajwa kwa jina la Gerald Mazuri ambaye pia huviuza kwa ‘wazungu’ Geita,” alisema Jaji De-Mello.

Jaji De-Mello alisema Ndahanya alipohojiwa alikiri kuhusika na rafiki yake Robert kutafuta walipo albino, waligundua kuwa kuna albino Kijiji cha Nyamaruru na walipopanga mbinu na kutafuta watu wa kukata mapanga ambao walifanikiwa kumkata Zawadi.

“Baada ya kukata walichukua viungo hivyo na kuvipeleka kwa mganga Ally kwa ajili ya vipimo, ili kujua kama vina kidhi mahitaji kusudiwa, walipima viungo hivyo kwa kutumia redio, shilingi moja ya zamani na wembe lakini vipimo hivyo vilionyesha viungo hivyo havikuwa na ubora,”alisema.

Alisema kutokana na ushahidi wa mama yake Zawadi na mtoto wa miaka 11, unaonyesha Kahindi na Nassoro walionwa wakiua, mwonekano wa wao ulionyeshwa mahakamni na mashahidi hao.

“Sina budi kusema watu hawa wanahusika,” alisema Jaji De-Mello.

Kuhusu Ndahanya na Nsiantemi, alisema ushahidi unaonyesha walikiri kufanya biashara hiyo baada ya kunaswa kwenye mtego wa polisi kwa maandishi.

“Nitamke kuwa kutokana na matatizo ya mauaji ya walemavu wa ngozi kuongezeka kila kukicha, mauaji haya ni ukatili, hivyo nimewatia hatiani kwa kuhusika na kifo hiki kwa mujibu wa sheria kifungu cha 199 na 197 cha kanuni ya adhabu, kifungu namba 16 mnahukumiwa kunyongwa hadi kufa,” alisema Jaji De-Mello.

Tangu mwaka 2007 hadi 2015, Wilaya ya Geita zaidi ya albino sita wameuawa huku wengine wanne wakijeruhiwa kwa kukatwa viungo vyao.

Hukumu hiyo ni ya 16 kitaifa kutolewa kuhusiana na mauaji ya albino na kwa Mkoa wa Geita ni ya kwanza.

Wadau wapongeza

Mbunge wa Lindi Mjini Salum Barwany ambaye ni mlemavu wa ngozi, amemuomba Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha anatia saini hukumu hiyo ili utekelezaji ufanyike haraka iwezekavyo.

Alisema imekuwa ni jambo la kawaida kwa adhabu hizo kutolewa lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu hali inayosababisha wahusika kuendelea kuwepo.

“Ningemuomba Rais kabla hajamaliza muda wake achukue hatua hiyo ninayoweza kusema muhimu kwetu na itamfanya akumbukwe siku zote, hususani katika suala kubwa kama hili,” alisema Barwany

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu anayewawakilisha watu wenye ulemavu wa ngozi bungeni Al-Shaymaa Kwegyir alisema adhabu hiyo ni sahihi kwa kuwa wahusika walionyesha kukusudia kuua.

“Nimefarijika kuona hatimaye Serikali imesikia kilio chao na kuanza kutoa adhabu ambayo itakuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia hizo.”

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHR,C Dk Helen-Kijo Bisimba alisema licha ya kuwa adhabu hiyo inalenga kukomesha vitendo hivyo vya kinyama, lakini inakiuka haki za binadamu.

Alifafanua kuwa kuna haja ya kuangaliwa upya kifungu cha adhabu ya kifo na kuondolewa kwenye sheria, huku wanaofanya makosa ya mauaji wakihukumiwa kifungo cha maisha.

“Kwa kosa walilofanya wanastahili adhabu kubwa ambayo binafsi naona kifungo cha maisha kingewafaa zaidi, ili wakiwa huko waweze kujifunza na kujutia makosa yao lakini siyo kuwaua,”alisema.