Wanne wahukumiwa kunyongwa kwa kuua albino Tanzania

 

Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya mlemavu wa ngozi, Zawadi Magimbu (32) wakiwa ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Geita baada ya kuhukumiwa kunyongwa. Kutoka kushoto ni Nasoro Charles, Singu Siantemi, Masaru Kahindi na Ndahanya Lumola. Picha na Jackline Masinde.      


Geita/Dar. Watu wanne wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na kosa la kumuua Zawadi Magindu (32) mwenye ulemavu wa ngozi, mkazi wa Kijiji cha Nyamaruru, Wilaya ya Geita mkoani hapa.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Joacquine De-Mello wa Mahakama Kuu, ambaye alisema alisema Mahakama imeridhika pasi na shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kwamba walihusika moja kwa moja na kifo hicho.

Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Nassoro Charles mkazi wa Kijiji cha Beda mkoani Kagera, Masaru Kahindi mkazi wa Kijiji cha Nyamaruru, Ndahanya Lumola na Singu Nsiantemi wakazi wa Kijiji cha Kakoyoyo, Wilaya ya Bukombe.

Jaji De-Mello alisema washtakiwa walifanya kosa hilo Machi 11, 2008 saa 1:00 usiku nyumbani kwa akina Zawadi wakati wakipata chakula cha usiku, walimkata kwa shoka na panga miguu yote na mkono wa kulia.

Alisema Masaru Kahindi aliyekuwa jirani na Zawadi, Nassoro Charles aliyekuwa mume wa marehemu walivamia nyumbani kwao wakati wanapata chakula cha usiku, huku wakiwa na panga na shoka kisha kumkata miguu na mkono wa kulia .

“Watu hao walikwenda na shoka na panga, walitumia shoka kumkata Zawadi huku mama yake Magdalena Mashimba na mjukuu wake, Semen Hamisi wakipigwa na kutupwa nje na wauaji hao,” alisema Jaji De-Mello.

Aliendelea kusema kuwa, wakati wanamkata Zawadi, mtoto wake Semeni alijibanza mlangoni na kuwatambua wauaji hao kuwa mmojawapo alikuwa mume wa mama yake na mwingine jirani yao.

“Walionwa na shahidi Magdalena na Semeni waliwatambua kwa sauti na mwonekano, kwani wakati wanafanya hivyo kulikuwa na mwanga wa mbalamwezi,” alisema.

Pia, Jaji De-Mello alisema washtakiwa Ndahanya na Nsiantemi walikuwa wafanyabiashara wa viungo vya albino, walikamatwa na polisi baada ya kutegewa mtego.

“Polisi walikuwa kwenye operesheni ya kuwatafuta watu wanaojihusisha na vitendo vya kuua albino, walipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna watu wanataka viungo vya albino ndipo walipotafuta albino wawili, mmoja akiwa mtoto na mwingine mtu mzima,” alisema.

Alisema baada ya kutegwa mtego huo walikamatwa washtakiwa wawili; Ndahanya na Nsiantemi ambao walikiri kuhusika na mauaji ya Zawadi na kuchukua viungo hivyo, kisha kuvipeleka kwa mganga wa jadi, Mussa Ally mkazi wa Katoro ambaye alihusika kuvipima ili kujua iwapo vina ubora.

“Wakati watu hawa wanahojiwa na polisi waliwataja wenzao wengi ambao hapa mahakamani hawapo sijui ni kwa nini… wakiongozwa na Robert Kagoma ambaye ndiye alikuwa wakala wa kulangua viungo hivyo na kuvipeleka kwa mganga wa jadi aliyetajwa kwa jina la Gerald Mazuri ambaye pia huviuza kwa ‘wazungu’ Geita,” alisema Jaji De-Mello.

Jaji De-Mello alisema Ndahanya alipohojiwa alikiri kuhusika na rafiki yake Robert kutafuta walipo albino, waligundua kuwa kuna albino Kijiji cha Nyamaruru na walipopanga mbinu na kutafuta watu wa kukata mapanga ambao walifanikiwa kumkata Zawadi.

“Baada ya kukata walichukua viungo hivyo na kuvipeleka kwa mganga Ally kwa ajili ya vipimo, ili kujua kama vina kidhi mahitaji kusudiwa, walipima viungo hivyo kwa kutumia redio, shilingi moja ya zamani na wembe lakini vipimo hivyo vilionyesha viungo hivyo havikuwa na ubora,”alisema.

Alisema kutokana na ushahidi wa mama yake Zawadi na mtoto wa miaka 11, unaonyesha Kahindi na Nassoro walionwa wakiua, mwonekano wa wao ulionyeshwa mahakamni na mashahidi hao.

“Sina budi kusema watu hawa wanahusika,” alisema Jaji De-Mello.

Kuhusu Ndahanya na Nsiantemi, alisema ushahidi unaonyesha walikiri kufanya biashara hiyo baada ya kunaswa kwenye mtego wa polisi kwa maandishi.

“Nitamke kuwa kutokana na matatizo ya mauaji ya walemavu wa ngozi kuongezeka kila kukicha, mauaji haya ni ukatili, hivyo nimewatia hatiani kwa kuhusika na kifo hiki kwa mujibu wa sheria kifungu cha 199 na 197 cha kanuni ya adhabu, kifungu namba 16 mnahukumiwa kunyongwa hadi kufa,” alisema Jaji De-Mello.

Tangu mwaka 2007 hadi 2015, Wilaya ya Geita zaidi ya albino sita wameuawa huku wengine wanne wakijeruhiwa kwa kukatwa viungo vyao.

Hukumu hiyo ni ya 16 kitaifa kutolewa kuhusiana na mauaji ya albino na kwa Mkoa wa Geita ni ya kwanza.

Wadau wapongeza

Mbunge wa Lindi Mjini Salum Barwany ambaye ni mlemavu wa ngozi, amemuomba Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha anatia saini hukumu hiyo ili utekelezaji ufanyike haraka iwezekavyo.

Alisema imekuwa ni jambo la kawaida kwa adhabu hizo kutolewa lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu hali inayosababisha wahusika kuendelea kuwepo.

“Ningemuomba Rais kabla hajamaliza muda wake achukue hatua hiyo ninayoweza kusema muhimu kwetu na itamfanya akumbukwe siku zote, hususani katika suala kubwa kama hili,” alisema Barwany

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu anayewawakilisha watu wenye ulemavu wa ngozi bungeni Al-Shaymaa Kwegyir alisema adhabu hiyo ni sahihi kwa kuwa wahusika walionyesha kukusudia kuua.

“Nimefarijika kuona hatimaye Serikali imesikia kilio chao na kuanza kutoa adhabu ambayo itakuwa fundisho kwa watu wengine wenye tabia hizo.”

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHR,C Dk Helen-Kijo Bisimba alisema licha ya kuwa adhabu hiyo inalenga kukomesha vitendo hivyo vya kinyama, lakini inakiuka haki za binadamu.

Alifafanua kuwa kuna haja ya kuangaliwa upya kifungu cha adhabu ya kifo na kuondolewa kwenye sheria, huku wanaofanya makosa ya mauaji wakihukumiwa kifungo cha maisha.

“Kwa kosa walilofanya wanastahili adhabu kubwa ambayo binafsi naona kifungo cha maisha kingewafaa zaidi, ili wakiwa huko waweze kujifunza na kujutia makosa yao lakini siyo kuwaua,”alisema.

No comments:

Post a Comment