Kutoka kushoto ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam
John Guninita na aliyekuwa mwenyekiti Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja
ambao leo wamehamia Chadema.
By Louis Kolumbia, Mwananchi Digital
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na aliyekuwa mwenyekiti mkoa wa
Dar es Salaam John Guninita wametangaza leo kuachana na CCM na kujiunga
Chadema.
Makada hao wa CCM wametangaza kujiunga
na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam leo.
Wakizungumza
katika mkutano huo, makada hao wamesema wamechukua uamuzi huo baada ya
kubaini CCM imepoteza mwelekeo na kwamba kinaendeshwa kibabe tofauti na
misingi ya kuasisiwa kwake.
Wametolea mfano wa kukiukwa
kwa demokrasia kulikofanywa wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea
urais wa chama hicho ambapo Dr John Magufuli aliteuliwa kupeperusha
bendera ya CCM.
Hatua ya makada hao imekuja ikiwa ni
siku moja tu tangu aliyekuwa mbunge wa chama hicho jimbo la Sikonge,
Said Nkumba atangaze kuachana na chama hicho na kujiunga na Chadema.
Huo
ni mwendelezo wa matukio ya makada na wabunge chama hicho kuhamia
upinzani hasa Chadema kwani awali aliyekuwa waziri mkuu wa zamani Edward
Lowassa aliachana na CCM baada ya jina lake kukatwa na kamati ya
maadili ya chama hicho.
Wengine waliohama CCM ni
aliyekuwa mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, aliyekuwa
mbunge wa Segerea, Makongoro Mahanga ambaye pia ni naibu waziri Kazi na
Ajira, aliyekuwa mbunge wa Kahama, James Lembeli, aliyekuwa mwenyekiti
wa wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai na mbunge wa viti maalumu anayemaliza
muda wake Esther Bulaya.
No comments:
Post a Comment