Daktari bandia aliwaambukiza Ukimwi watu 100


Mwanaume mmoja aliyejidai kuwa daktari na kuwaambukiza watu zaidi ya mia moja virusi amefikishwa mahakamani nchini Cambodia.

Yamkini daktari huyo bandia alikuwa akiwadunga wagonjwa wake kwa sindano aliyokuwa ameitumia kwa mgonjwa aliyekuwa na virusi vya Ukimwi.

Yem Chhrin anakabiliwa na kosa la kuua na kuambukiza watu ugonjwa huo kwa kukusudia.

Aidha Bw Yem anashtakiwa kwa kuwalaghai watu kuwa ni daktari ilhali hana vyeti halali vya kuhudumia umma.

Iwapo atapatikana na hatia mahakama ya nchi hiyo huenda ikamhukumu kifungo cha maisha jela.

Waathiriwa walioambukizwa maradhi ya Ukimwi wanatokea katika kijiji cha Roka kilichoko Kaskazini Magharibi.

Mmoja wao ni kiongozi wa kidini wa madhehebu ya Buddha na mtoto wa miaka mitatu.

Takriban 10 kati ya waathiriwa hao wanakisiwa kuwa wameshakata roho.

Kwa mujibu wa ripoti za mahakama daktari huyo bandia amekiri kuhudumu bila vyeti maalum ila anakana kukusudia kuwaambukiza watu hao 100 virusi vinavyosababisha maradhi ya Ukimwi.

No comments:

Post a Comment