Marekani yakerwa na ziara ya Assad Moscow
Marekani imeshutumu Urusi kwa kumpa mapokezi ya taadhima Rais wa Syria Bashar al-Assad mjini Moscow.
"Tunatazama
mapokezi ya zulia jekundu aliyopewa Assad, aliyetumia silaha za
kemikali dhidi ya watu wake, kuwa kinyume na lengo lililoelezwa wazi na
Urusi la kutaka kuwepo na shughuli wa mpito kisiasa Syria,” msemaji wa
ikulu ya White House Eric Schultz amewaambia wanahabari.
Afisa wa
wizara ya masuala ya ndani ya Marekani alisema taifa hilo
halijashangazwa na ziara hiyo, lakini wasiwasi mkubwa kwa Marekani ni
Urusi kuendelea kumsaidia kivita Assad.
Alisema hilo litaipa nguvu zaidi serikali ya Assad na hivyo kuendeleza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Ziara
hiyo ya kiongozi huyo wa Syria Jumanne ilifanyika wiki tatu baada ya
Urusi kuanza kushambulia kwa ndege ngome za wapiganaji wa Islamic State
na makundi mengine yanayopinga utawala wa Assad.
Ilikuwa ziara ya
kwanza kabisa kwa Assad nje ya nchi baada ya mapigano kuzuka Syria 2011.
Mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe yameua watu 250,000.
Akiwa jijini Moscow, Assad alitoa shukrani zake kwa Urusi kuingilia kati kijeshi nchini mwake.
Alisema operesheni hiyo ya Urusi ilikuwa imezuia ugadi kueneza zaidi na kuwa madhara makubwa Syria.
Kwa
upande wake, Bw Putin alisema matumaini ya Moscow ni kwamba suluhu ya
muda mrefu itapatikana kupitia mchakato wa kisiasa na kwa kushirikisha
makundi yote ya kisiasa, kikabila na kidini.
Mwandishi wa BBC
aliyeko Moscow Steve Rosenberg anasema kuwa kwa kumkaribisha kiongozi
huyo wa Syria mjini Moscow, Putin alikuwa akituma ujumbe mkali kwa
mataifa ya Magharibi kwamba Moscow ni mhusika mkuu katika mzozo huo
Mashariki ya Kati na kwamba suluhu haiwezi kupatikana bila kuhusisha
Urusi.
No comments:
Post a Comment