Watu wapatao 60 wanahofiwa kufa baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka katika jimbo la Darfur nchini Sudan.
Waokoaji walikuwa wakitumia zana za asili
kujaribu kuwafikia wachimbaji hao huku kukiwa na hofu kwamba visima
zaidi huenda vikafunikwa.
Makundi hasimu Kaskazini mwa Darfur, yalikuwa yakipigana kugombea udhibiti wa mgodi huo mwazi Februari mwaka huu.
Dhahabu imekua bidhaa muhimu kwa Sudan tangu Sudan Kusini yenye utajiri mkubwa wa mafuta ijitenge miaka miwili iliyopita.
Kujitenga kwa Sudan Kusini kulisababisha Sudan kupoteza asilimia sabini na tano ya uzalishaji wa mafuta.
Serikali ya Sudan inatarajia kuzalisha takriban
tani 50 za dhahabu mwaka 2013, ambayo huenda ikaifanya Sudan kuwa nchi
ya tatu Barani Afrika kwa uchimbaji wa dhahabu na kuifikisha katika
nafasi ya 15 ya wazalishaji wakubwa duniani.
Ukosefu wa vifaa vya uokozi
Uchimbaji wa madini ya dhahabu
Kwa mujibu wa afisa wa serikali, Haroun al
Hassan kisima hicho chenye urefu wa mita 40, kwenye mgodi wa Jebel Amer
Darfur Kaskazini kilifunikwa siku ya Jumatatu.
Kaimu Gavana wa Kaskazini Darfur, Al Fatieh
Abdeaziz, ameiambia BBC kwamba watu 60 hawajulikani walipo, lakini
hakuthibitisha kama wamekufa.
Bw. Hassan amesema juhudi za uokoaji
zinakwamishwa na hofu kwamba visima zaidi huenda vikafunikwa. Amedai
kuwa, waokoaji hawawezi kutumia mashine kwa sababu endapo zitafika
karibu, ardhi itafunikwa.
Ameongeza kuwa, watu wanatumia zana za asili na kwa sababu hiyo, shughuli ya uokoaji inakwenda taratibu.
Umoja wa Mataifa umesema, watu wapatao 100,000
walikimbia mapigano baada ya makundi hasimu ya Kiarabu kupigana
wakigombea udhibiti wa mgodi huo Februari mwaka huu.
Zaidi ya watu milioni moja wamekuwa wakiishi katika kambi za watu wasiokuwa na makazi Darfur, baada ya muongo mmoja wa mapigano.
Machafuko ya Darfur yamepungua baada ya kuzuka
kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2003 lakini bado kuna mapigano
kati ya vikosi vya serikali, waasi, wahalifu na makundi hasimu.
No comments:
Post a Comment