Derick Cyprian akiangaliwa na baba yake katika Hospitali ya Mount Meru
jana baada ya kujeruhiwa na bomu.
Arusha.Mtu mmoja amefariki
dunia na wengine 59 kujeruhiwa akiwamo Balozi wa Vatican na Mwakilishi
wa Papa nchini Tanzania, Askofu Mkuu Francisco Montecillo Padilla jana
asubuhi baada ya mtu asiyejulikana kurusha bomu wakati wa sherehe ya
uzinduzi wa Jengo la Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi,
Olasiti, Arusha.
Miongoni mwa majeruhi, imeelezwa kuwa wanne ni mahututi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus
Sabas amelielezea kuwa tukio hilo kuwa ni la kigaidi hasa kutokana na
kumlenga Balozi wa Papa nchini na kwamba mtu mmoja anashikiliwa
akihusishwa nalo.
Wataalamu wa mabomu wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) wanachunguza aina ya bomu lililotupwa lakini uchunguzi wa awali
unaonyesha lilikuwa limetengenezwa kienyeji.
Ilivyokuwa
Watu walioshuhudia tukio hilo wanasimulia kuwa
bomu hilo lilirushwa yapata saa nne asubuhi wakati mgeni rasmi
akijiandaa kufungua jengo la kanisa baada ya ujenzi wake kukamilika.
Shambulio hilo lilitokea wakati balozi huyo akiwa
amesimama na mwenyeji wake, Askofu Mkuu, Josephat Lebulu, mapadri na
watawa kutoka mashirika mbalimbali ya Jimbo Kuu la Arusha kwa ajili ya
kukata utepe wa uzinduzi.
Kamanda Sabas alisema mtu aliyerusha bomu hilo
alitokea nyuma ya kanisa hilo la ghorofa na kurusha bomu hilo kwa mkono
wa kulia... “Alifanya jitihada za kupenya ili awafikie viongozi lakini
alishindwa kutokana na wingi wa waumini waliokuwapo kwenye eneo hilo.”
Padri Moses Mwaniki aliyemshikia Balozi Padilla
maji ya baraka yaliyotumika kubariki kanisa hilo, alisema kilichosaidia
bomu hilo kutomfikia mwakilishi huyo wa Papa ni kutua mgongoni mwa mmoja
wa waumini na kuanguka chini kabla ya kulipuka na kujeruhi watu.
“Ingawa hatuwezi kusema kwa uhakika, tunaamini
mlengwa mkuu alikuwa mgeni wetu, Balozi Askofu Mkuu Padilla. Tunatakiwa
kuliombea sana Taifa liondokane na matukio mabaya kama haya,” alisema
Padri Mwaniki.
Baada ya tukio hilo, Balozi Padilla, Askofu Lebulu
na viongozi wa kanisa hilo waliondolewa na kuhifadhiwa katika moja ya
vyumba vya kanisa hilo kabla ya kutolewa kwenye eneo hilo yapata saa
5.30 asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Msemaji wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha,
Padri Festus Mangwangi alisema aliyerusha bomu hilo alishuhudiwa na
mtoto mdogo aliyekuwapo kanisani hapo.
“Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto huyo, mtu huyo alikuwa amevaa
kanzu nyeupe pamoja na koti la mvua lenye rangi ya kahawia na alikimbia
mara baada ya kulirusha katikati ya watu. Ametusimulia kuwa mtu huyo
baada ya kurusha bomu lile alikimbia na kuwahadaa watu kwa kuita ‘mwizi
mwizi mwizi…’ akionyesha mbele kama kuna mtu anayemfukuza jambo
lililowazubaisha watu lakini mtoto aliyemwona akirusha bomu aliwaeleza
kuwa ndiye mhusika.”
“Waliomshuhudia mhusika akikimbia wanasema
walishindwa kumwona mwizi aliyekuwa akimfukuza na hivyo kubaki
wakimkodolea macho, hali iliyomfanya atokomee katikati ya nyumba za
watu,” alisema Padri Mangwangi, ambaye aliongeza kuwa katika kipindi
hicho kulikuwa kuna mkanganyiko mkubwa kutokana na bomu kulipuka na mtu
huyo kudai kuna mwizi.
Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi, Julius Mbaga ambaye mkewe, Concesa (42), ni mmoja wa
majeruhi, alisema ni kudra za Mwenyezi Mungu pekee ndizo zimeepusha
madhara na maafa makubwa.
Kifo na majeruhi
Aliyefariki ametambuliwa kuwa ni Regina Losioki
(46), ambaye alikuwa anaimba kwaya katika kanisa hilo. Alifariki baada
ya kufikishwa katika Hospitali ya St. Elizabeth, Arusha.
Mamia ya watu jana walifurika katika Hospitali ya
Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kushuhudia watu waliokuwa wakifikishwa hapo
kutoka katika eneo la tukio.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa, Dk Frida Mokiti
alisema majeruhi 41 walikuwa wamelazwa Mount Meru, 16 walikuwa Hospitali
ya St Elizabeth huku mmoja akiwa katika Hospitali ya Selian na mwingine
Hospitali ya Kaloleni... “Kuna mgonjwa mmoja, ambaye amepelekwa
Hospitali ya Rufaa ya KCMC (Moshi) kwa matibabu zaidi.”
Waliojeruhiwa ambao majina yao yalibandikwa katika
ukuta wa Hospitali ya Mount Meru ni Christopher Raymond (10), Consensia
Mbaga (53), Deborah Joachim (24), Elizabeth Isdori (24), Bertha
Cosinery (49), Anna Didas (52), Edda Ndowo(77), Derick Cyprian (8),
Faustine Andrea (35), Mary Okech na Neema Daud (13).
Alex Arnold, Agripina Alex (9), James Gabriel
(16), Loveness Nelson (17), Amalone Pius (25), Frank Donatus (10),
Alphonce Nyaland (26), Athanasia Reginald (14), Phillemon Ceressa (49),
Neema Daud (13) Sophia Kanda (72), Theofrida Innocent (21), Regina
Darnes (17).
Mesoit Siriri (33), Clenes Pius (22), Joyce Yohana
(15), Restuta Alex (50), Mathias Riha (74), Magreth Andrew (45), James
Gabriel (16), Regina James (17), Elizabeth Masawe (15), Elizabeth Sauli
(18), Njau (35), Yasinta Msafiri (160) na Doreen Pancras (28).
Waliokuwa katika Hospitali ya St. Elizabeth kwa
mujibu wa Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Samwel Mlay ni Fatuma
Tarimo, Glory Tesha, Rose Pius, Isabela Michael, Jenipher Joachim,
Samwel Laswai, John James, Joan Temba, Joram Kisera, Novat John, Neema
Kilusu, Regina Shirima, Inocent Charles, Lightness na Anna Edward.
Majeruhi wazungumza
Akizungumzia tukio hilo, Ndowe ambaye amelazwa Mount Metu,
alisema aliona kitu kikidondoka kanisani na kutoa kishindo kikubwa na
watu kuanza kukimbia ovyo. Alipoteza fahamu kutokana na kutokwa na damu
nyingi.
Debora ambaye ni Polisi alisema alipoona kitu
kikidondoka alibaini mara moja kuwa ni bomu. Alijeruhiwa mguu na mkono.
Elizabeth alisema aliona kitu kama kibuyu kikianguka chini na kupasuka
na baada ya hapo hakujua kilichoendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo alisema:
“Hili ni jambo la kusikitisha, kukera na
kufadhaisha sana kutokea mkoani mwetu. Nawaomba wananchi wote tuwe
watulivu wakati vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea na uchunguzi.”
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa
Arumeru Mashariki, Joshua Nassari waliongoza mamia ya watu kutoa damu
ili kuokoa maisha ya majeruhi.
Akizungumza kabla ya kutoa damu, Lema alisema
msiba huo ni wa wakazi wote wa Arusha na akaomba usichochee mpasuko wa
kidini kwani haijulikani nani waliohusika.
“Msiba huu ni wetu sote Wakristo na Waislamu,
kikubwa ni kuomboleza na kulaani waliohusika na unyama huu na sote
tuhakikishe tunasaidia kukamatwa kwa wote waliohusika,” alisema.
Bajeti ya Mambo ya Ndani leo
Tukio hilo limekuja siku moja kabla ya Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi kuwasilisha bungeni Dodoma leo, Hotuba ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi yake kwa mwaka 2013/14.
Tukio hilo pamoja na matukio kadhaa yenye
kuhatarisha umoja wa Watanzania yanayohusishwa na masuala ya dini
yanatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika mjadala wa bajeti hiyo.
Imeandikwa na Mussa Juma, Moses Mashalla Peter Saramba na Daniel Sabuni.
No comments:
Post a Comment