Ripoti yabaini mwandishi mmoja huuawa duniani kila baada ya siku 5

Askaro Polisi wakiwa katika eneo alipouawa Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi kwa kulipuliwa na bomu la machozi mwaka jana.

Dar es Salaam. Mwishoni mwa  wiki tasnia ya habari ilifanya kumbukumbu ya Siku ya Uhuru wa Habari  huku taarifa zikionyesha kuwa kwa miaka kumi iliyopita, wastani wa mwandishi mmoja kuuawa kila baada ya siku tano katika maeneo mbalimbali duniani.             

Ripoti iliyoandaliwa na jumuiya ya kulinda usalama wa waandishi wa habari duniani (CPJ)  inaeleza kuwa tangu mwaka 1992  mpaka 2013, waandishi 982 wameuawa.

Sababu za mauaji hayo zinatajwa  kuwa ni mazingira ya utekelezaji wa kazi zao.

Ripoti ya CPJ inaonyesha nchi za Afrika na Uarabuni zinaongoza katika utekelezaji wa mauaji hayo huku Somalia ikiripotiwa kuuawa waandishi 50 katika kipindi hicho.
Nchi kubwa zenye idadi ndogo ya mauaji hayo ni Uingereza(1), Ufaransa(1), China (2), Japan (1)na  Hispania(1). Tanzania ni moja kati ya nchi zilizotajwa na kuingia katika ripoti ya kumbukumbu hiyo duniani kutokana na kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi.

Pia, mwanahabari Issa Ngumba wa Radio Kwizera aliuawa kule Kakonko, Mkoani Kigoma.

Kutokana na matokeo hayo, wadau mbalimbali wa masuala ya habari nchini wametoa maoni yao  juu ya mwenendo wa uhuru wa vyombo vya habari nchini wakisema uhuru huo sasa umetiwa kitanzini.

MCT
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga amesema katika kipindi cha hivi karibuni usalama kwa waandishi wa habari umepungua kutokana na kuwapo kwa matukio ya vitisho visivyotarajiwa miongoni mwao.

Mukajanga alisema mbali na mauaji ya Mwangosi, kuna baadhi ya vitisho vimetolewa kwao wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Matukio ya utekaji nyara japokuwa hatujapata uthibitisho lakini hali hiyo imeondoa taswira ya nchi na kushusha heshima yake kimataifa,” alisema Mukajanga.

Mukajanga alisema matukio hayo yamesababishwa na hali ya kuibuka kwa makundi ya kisiasa na kidini katika kipindi cha hivi karibuni hatua iliyochangia mwandishi kunyimwa uhuru na kujengewa dhana ya kuegemea upande mmoja katika uandishi wa habari zake hususan zinazogusa makundi hayo.

“Kwa mazingira hayo mwandishi wa habari lazima atakuwa na wakati mgumu sana, hata kama ataandika ukweli bado atakuwa amesababisha madhara au kuharibu masilahi ya upande mwingine,” anasema Mukajanga.

Hata hivyo, Mukajanga alitoa mapendekezo yake akiwataka waandishi wan habari kusimamia maadili ya kazi zao ili jamii itambue ukweli hata kama wataendelea kupigwa vita.

 

TMF  
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), Erenest Sungura alisema kutokana na usalama wa mwandishi wa habari kupungua hapa nchini, Serikali inatakiwa kuangalia changamoto za kimazingira zinazochangia madhara hayo.

Sungura alisema inawezekana moja ya sababu ni pamoja na sheria zinazonyima uhuru wa kuandika habari fulani hivyo mwandishi hujikuta akilazimisha kuandika ukweli katikati ya ukiukwaji wa sheria zinazombana.

“Kuna sheria zinazowanyima uhuru wa kuandika mambo mengine zifanyiwe mabadiliko,” alisema.

Hata hivyo, Sungura anatoa wito akiwataka wamiliki wa vyombo vya habari kutengeneza mazingira ya ulinzi wa kutosha kwa waandishi wao pale wanapokuwa wanafanya kazi za uchunguzi.

“Wahariri waangalie suala hilo kwa sababu mimi napokea simu karibu tano kwa mwezi za waandishi wakieleza kupewa vitisho,” anasema.
Mbali na hilo, Sungura anawataka pia waandishi wazingatie maadili ya kazi zao ili kujenga taswira ya ubora wa taaluma yao ili kujiweka huru na kupunguza uadui miongoni mwa jamii zenye makundi.   

Taswa
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa),  Juma Pinto anasema tofauti za makundi ya kisiasa ndiyo imekuwa chanzo cha mwandishi wa habari nchini kukumbwa na hatari ya usalama wake pale anapokuwa akitekeleza majukumu yake.

“Makundi ya kisiasa  ndiyo tatizo zaidi, kwa nini hatusikii kwenye michezo  au burudani,” alisema.

Pinto anasema kutokana na mazingira magumu yaliyopo kwa sasa, ameshauri waandishi kuwa na umoja na msimamo mkali pale inapotokea mwandishi ameingia kwenye matatizo ya vitisho, kutekwa au kuuawa.

“Mbali na msimamo wetu Serikali pia inatakiwa kuangalia sheria kandamizi kwa mwandishi wa habari, Katiba yenyewe inamtambua mmiliki wa chombo na sio mwandishi, yaani mwandishi wetu hapa nchini ni sawa na mtoto aliyetelekezwa, hana sehemu yoyote inayomtambua,” anasema Pinto.

Hali katika nchi nyingine
Mbali na taarifa hizo, hali si salama kwa nchi nyingine ambapo shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka duniani liliripoti kuwa mwaka 2012 ulikuwa ni mwaka wa maafa zaidi kwa waandishi wa habari kote duniani ukilinganisha na miaka iliyopita.

Somalia ambayo haina serikali thabiti iliripotiwa kufanya mauaji ya waandishi 18 na Pakstan waandishi 10.

Katika ripoti hiyo ya Desemba 19,  2012,  ofisa wa shirika hilo, Ulrike Gruska anasema  waandishi 88 waliuawa wakati wakiripoti kazi zao kutoka maeneo yenye vita na mashambulizi ya mabomu huku sababu zikielezwa kuwa ni pamoja na mazingira ya kutatanisha, makusudi na uhasama kutoka kwa baadhi ya wanasiasa.

 

Ripoti hiyo inasema mpaka sasa kuna jumla ya waandishi wa habari 65 wameuawa nchini Syria mwaka huu, wakati wanatekeleza majukumu yao, huku 21 wakiswekwa rumande na makundi ya watu ama wapiganaji nchini humo.

Nchini Mexico, waandishi wanaishi katika maisha ya hatari,hasa wanapokuwa wanaripoti kuhusu uhalifu, usafirishaji wa dawa za kulevya na uhusiano kati ya viongozi wa magenge ya wahalifu na wafanyakazi wa umma.

Taarifa nchini humo zinasema kuna idadi ya waandishi sita wameuawa tangu Januari mwaka huu.

Mbali na nchi hiyo, Brazil pia imetajwa kama mojawapo ya nchi hatari kwa waandishi wa habari kutokana na vita inayofanywa dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

Matukio ya unyanyasaji  
Katika hatua nyingine, hali imeonyesha wasiwasi baada ya kuongezeka kwa idadi ya waandishi duniani waliofungwa jela mwaka huu. Ripoti hiyo inasema zaidi ya waandishi na wana ‘blogi’ 1,000 walikamatwa mwaka huu huku zaidi ya 2,000 wakipewa vitisho.

No comments:

Post a Comment