Dk Mvungi afariki dunia


Dk Sengondo Mvungi


Dar es Salaam.Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi (61) amefariki dunia katika Hospitali ya Millpark Netcare, Johanesburg, Afrika Kusini.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana kutoka Afrika Kusini na kuthibitishwa na Msemaji wa Hospitali ya Millpark, Tebogo Nyembezi zinasema Dk Mvungi alifariki dunia jana mchana. “Ni kweli tulimpokea mgonjwa huyo kutoka Tanzania na alifariki 6:00 mchana (saa 7:00 kwa saa za Afrika Mashariki),”alisema Nyembezi.

Nyembezi alisema kwamba walimpokea mgonjwa huyo akiwa na majeraha ya kichwa, lakini aliahidi kueleza sababu ya kifo chake leo baada ya kuzungumza na madaktari waliokuwa wakimtibu.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba pia alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kwamba walikuwa wakiendelea kuandaa taratibu za kuleta mwili wake nchini.

“Ni pigo kubwa kwetu, tunaangalia namna ya kuusafirisha kuja nchini na baadaye tutatoa taarifa rasmi,”alisema Jaji Warioba na kuongeza:

“Kwa kweli ni pigo kubwa siyo kwetu tu, lakini pigo kubwa kwa nchi yetu, tumepoteza mtu muhimu na kiungo muhimu sana. Dk Mvungi, wengine tulimfahamu tangu alipokuwa mwanafunzi, alikuwa mtu aliyesema kile alichokiamini, akikwambia kitu kilikuwa ni kile kilichopo moyoni mwake”.

Jaji Warioba alisema Dk Mvungi alikuwa msomi aliyebobea katika masuala ya sheria na kwamba alikuwa na mchango mkubwa katika tume. Pia alisema marehemu atakumbukwa kwa ushiriki wake wa dhati katika kupigania haki za binadamu, kazi aliyoifanya kwa moyo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani alisema: “Dk Mvungi alikuwa mfanyakazi hodari, alikuwa hachoki na hata ulipotokea ubishi mkubwa katika majadiliano kiasi cha watu wengine ku-loose temper (kupandwa na jazba), yeye alibaki vilevile na alizungumza vilevile bila kubadilika. Kweli tumempoteza mtu muhimu sana maana alikuwa akifahamu vizuri sana sheria, hatuna jinsi maana tumempoteza, kwahiyo itabidi tuendelee na kazi hii. Hatuna namna nyingine ya kufanya,”alisema Jaji Ramadhani.

Jaji Ramadhani alisema taratibu nyingine zitatangazwa baadaye kwani lazima washirikiane na chama chake, NCCR- Mageuzi alikokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji, familia yake na Chuo Kikuu cha Bagamoyo ambako alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliliambia gazeti hili kwamba walipokea taarifa ya kifo cha Dk Mvungi saa 9.30 alasiri jana. “Tumepokea taarifa hizo alasiri kwamba amefariki. Ni kweli na sasa ninaelekea nyumbani kwake ili kuitaarifu familia,”alisema Mbatia.

Taarifa ya Tume

Jana jioni, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa rasmi kuhusu kifo cha Dk Mvungi ikisema: “Kwa masikitiko makubwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dk Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Millpark iliyopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini amefariki dunia.”

Taarifa iliyotolewa Katibu wa tume hiyo, Assaa Rashid ilisema Dk Mvungi alifariki dunia saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini.

Iliendelea kusema taarifa hiyo kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka Afrika Kusini kuja nchini kwa maziko zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa baadaye.

Dk Mvungi, alikuwa akitibiwa Afrika Kusini baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana walipovamiwa nyumbani kwake Kibamba, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Novemba 3 mwaka huu.

Alipelekwa nchini Afrika Kusini, Novemba 7, 2013 kwa matibabu zaidi baada ya kulazwa kwa siku tano kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) jijini Dar es Salaam.

Dk Mvungi, ambaye aligombea urais mwaka 2010 kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi, alijeruhiwa vibaya kichwani na sehemu nyingine za mwili wake baada ya kukatwa mapanga na wavamizi hao.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Profesa Costa Mahalu alisema chuo hicho kimepoteza mtu muhimu sana, kwani ni mmoja wa waanzilishi waliokuwa wakifahamu vyema malengo na dira yake.

“Tumepata pigo kubwa sana kwani tumempoteza mtu ambaye tulishirikiana naye katika kuanzisha chuo hiki na aliyafahamu vyema malengo na dira yake, alikuwa ni mwalimu mzuri aliyebobea katika constitutional laws (sheria za Katiba) na wanafunzi walimpenda sana,”alisema Profesa Mahalu.

Profesa Mahalu alisema Dk Mvungi ambaye alikuwa naibu wake kabla ya kujiunga na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, walifahamiana naye siku nyingi na kwamba wakati marehemu alipokwenda kusoma Shahada ya Uzamivu nchini Ujerumani alifikia nyumbani kwake (kwa Mahalu).

“Wakati huo nilikuwa nikifundisha Ujerumani, alikuja kusoma PhD yake ya masuala ya sheria na alifikia nyumbani kwangu, tutamkumbuka kwa uhodari wake katika kuchapa kazi, kweli tumempoteza mtu mahiri sana,”alisema.

Chadema, CCM wamlilia

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema amesikitishwa na taarifa za kifo cha Dk Mvungi na kwamba taifa limempoteza mwanzilishi wa mageuzi ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kudai Katiba Mpya.

“Tumepokea taarifa za kifo hiki kwa mshtuko mkubwa, tunamwomba Mwenyezi Mungu aipe nguvu familia ya Dk Mvungi, tunatoa pole kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na uongozi wa NCCR-Mageuzi,” alisema Mbowe.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa (CCM), Mwigulu Nchemba alisema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na kutoa pole kwa Watanzania wote kwa sababu Dk Mvungi alikuwa anafanya kazi muhimu ya kuwezesha kupatikana kwa Katiba Mpya.

Alisema amekufa wakati mchango na mawazo yake yakiwa yanahitajika kwa kiasi kikubwa katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba CCM kinaendelea kuisisitizia Serikali iwasake wahalifu hao ili wafikishwe kwenye vyombo vya dola.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema ameshtushwa na taarifa za kifo hicho ambacho kimetokea wakati Dk Mvungi akifanya kazi muhimu ya kuitafuta Katiba Mpya. “Naomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi, amina,” alisema.

Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila alisema taifa limepoteza mtu muhimu na kwamba hali ya ulinzi ni suala linalohitaji mjadala wa kitaifa.“Tunahitaji kuangalia kiini cha uhalifu hapa nchini, watu wanateswa na kujeruhiwa ovyo ni lazima tuchukue hatua,” alisema.

Mitandao ya kijamii

Muda mfupi baada ya taarifa za kifo chake, mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Jamii Forum ilikuwa ilitawaliwa na salamu za pole kutoka kwa watu mbalimbali.

Hussein Bashe kwenye ukurasa wake wa Facebook aliandika kuwa, “Dr Sengondo Mvungi Is No More (hatunaye tena), taarifa zilizonifikia kutoka Hospitali ya Millpark, ndugu yetu Mvungi amefariki, mnamo saa tisa na nusu.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Wahalifu wamekatisha uhai wake wakati akifanya jukumu zito kwa ajili ya taifa letu. Jambo hili linaumiza sana Mungu atalipia uhalifu huu, poleni Tume ya Katiba, Poleni Familia, poleni NCCR-Mageuzi.”

Mtu mwingine aliyechangia suala hilo kwenye mtandao wa Jamiiforum ni yule aliyejitambulisha kwa jina la Ta Muganyizi aliyeandika kuwa, RIP Dr. Mvungi... Mungu akulaze mahala pema peponi. Japo umeondoka kivuli chako kitaishi... Naipa pole familia yako, maisha yetu kwa sasa nchini ni kudra za Mwenyezi Mungu. Ni kwamba tupigwe... wengine wamepona lakini wewe umeondoka.”

No comments:

Post a Comment