HALMASHAURI
ya wilaya ya Morogoro kwa kushirikiana na idara ya afya inatarajia
kuwafanyia upasuaji wa mabusha watu 80 wakati wowote kuanzia sasa katika
vituo vyake vya afya kwa lengo la kukabiliana na tatizo hilo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mratibu msaidizi wa kudhibiti
magonjwa yasiyopewa kipaumbele wilayani humo Elias Lugata alisema kwa
sasa dawa zimeshafika na kwamba taratibu za wataalam watahaohusika na
kufanya upasuaji huo linaendelea.
Lugata alisema kuwa katika zoezi hilo halmashauri imetenga vituo vya
afya vya Ngerengere,Mkono wa Mara,Dutumi na Tawa kwa lengo la
kuwawezesha walengwa kufika kwenye vituo hivyo walivyo jirani navyo
kupatiwa huduma hiyo.
Alisema fedha hizo zimetolewa na halmashauri kupitia mfuko wake(Basket
fund) kwa lengo la kuwasaidia watu wenye tatizo hilo ili kudhibiti
ongezeko na ugonjwa huo.
"unajua kuna watu wamekuwa wakifika kwenye vituo vyetu vya afya na
kutaka kufanyiwa upasuaji kutokana na kutokuwa na uwezo wa kumudu ghrama
za kufanyiwa upasuaji huo hivyo kutokana na hali hiyo halmashauri
ikaona ni vyema ikatenga fedha kwa ajili ya kusaidia watu hao"alisema
Lugata.
Alisema watu waliobainika ni wengi lakini tutaanza na watu hao na kwamba
zoezi hilo litaendelea kulingana na uwezo utakavyoruhusu kwa lengo la
kusaidia wananchi wa wilaya hiyo kukabiliana na tatizo hilo ambalo
linakuwa kero kubwa kwa mhusika kutokana na kuharibu maumbile.
No comments:
Post a Comment