Nimesikitishwa Na Kauli Ya Simba Mwenzangu Zacharia Hans-Pope

Ndugu zangu, 


Juzi usiku kwenye habari za michezo kwenye moja ya runinga zetu nilimsikia Mwenyekiti wa Friends Of Simba Zacharia Hans-Pope akitamka kuwa kuanzia sasa Simba haitasajili wachezazi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki akirejea tukio la mchezaji Mbuyi Twitte na utata wake katika usajili ambapo ameishia kwenda Yanga badala ya Simba licha ya Aden Rage kuonekana kwenye picha za magazetini kuwa ameshamaliza mambo na mchezaji huyo.


Hans- Pope anasema wachezaji wa ukanda huu wa Afrika Mashariki hawaaminiki na hivyo sasa Simba itaangalia zaidi wachezaji kutoka nchi nyingine ikiwemo nchi kama za Ghana na Nigeria.


Hans- Pope amepotoka. Kauli yake ni ya jumla mno. Binafsi imenisikitisha, maana ametoa hukumu ya jumla. Si kweli kuwa wachezaji wote wa Afria Mashariki hawaaminiki.  Tumewaona wachezaji kadhaa wa Afrika Mashariki wakiaminika hata kwenye soka ya Kimataifa; wachezaji kama vile Katerezi ( Rwanda) na Macdonald Mariga ( Kenya) kwa kuwataja wachache.


Mimi ni Simba kama Hans-Pope, tukubali kuwa watani zetu Yanga wametuzi maarifa, na haya yanatokea kwenye soka. Tuache sasa kucheza soka ya magazetini, redioni, runinga , viwanja vya Ikulu na  Bunge kama wanavyofanya watani zetu Yanga.


Ni kweli kuwa Yanga wametukera Simba kwa walichotufanyia. Lakini,  tunajua, na Yanga pia wanajua, kuwa  Simba ni ' Taifa Kubwa'.  Mbuyi Twitte ni  mchezaji kama wengine, kwa nini atusumbue kichwa kiasi cha kuwaweka wachezaji wote wa Afrika Mashariki kwenye fungu moja na Mbuyi Twitte?


Hans-Pope hajachelewa, kwa namna atakayoona inafaa, arekebishe kauli yake ile, na hivyo basi, kuwaomba radhi wachezaji wa Afrika Mashariki.


No comments:

Post a Comment