63 wafariki katika ajali ya treni DRC

Treni hiyo ilikuwa imebeba idadi kubwa ya watu baadhi wakiwa wamekaa juu ya treni

Takriban watu 63 wamefariki baada ya treni iliyokuwa imebeba abiria kupoteza mwelekeo Kusini Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Msemaji wa serikali Lambert Mende alisema kuwa polisi wanahofia kuwa idadi ya watu waliofariki huenda ikaongezeka. Pia alisema kuwa polisi watafanya uchunguzi kubaini chanzo cha ajali.

Ajali hiyo ilitokea karibu na eneo la Kamina katika mkoa wenye utajiri wa madini wa Katanga.

Treni hiyo ilikuwa imebeba idadi kubwa ya watu kupindukia wengine wakiwa wameketi juu ya treni yenyewe.

Waziri wa mambo ya ndani katika mkoa huo Jean Marie Dikanga Kazadi, aliambia BBC kuwadereva wa treni hiyo alikuwa anaiendesha kwa kasi .

Watu 80 walijeruhiwa vibaya huku wengine saba wakiwa bado wamekwama ndani ya treni vifusi.

Treni ilianguka Jumanne asubuhi lakini waokozi waliweza tu kuwasili nyakati za jioni.

Sehemu kubwa ya njia ya reli ya DRC, imesalia katika hali yake tangu enzi za ukoloni na ni nadra kufanyiwa ukarabati.

Treni hiyo ilianguka wakati dereva alipokuwa anajaribu kupunguza kasi.

Marekani yasikitishwa na umoja Palestina

Waziri wa Masahuri ya Kigeni wa Marekani, John Kerry, (kushoto) akiwa na wajumbe wa amani wa Israel na Palestina siku zilizopita.

Marekani inasema imesikitishwa na makubaliano kati ya makundi makuu Palestina ya kuiunda serikali ya Umoja.

Imeoya huenda hatua hiyo ikatatiza zaidi jitihada za amani. Uamuzi huo unalijumuisha kundi lenye msimamo kali za kidini, Hamas, unaliotawala eneo la Gaza na limetajwa na Marekani na Israeli kama kundi la kigaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Marekani Jen Psaki amesema wakati wa kutangaza uamuzi hduo ndio unaotia wasiwasi.

Tangazo hilo limefanywa wakati ambapo Marekani ilikuwa ikijitahidi kushawishi Israil na Wapalestina kukubali kuendelea kufanya mashauriano ya amani ambayo hadi kufikia sasa hayajazaa matunda yo yote.

Bi Psaki amesema mapatano kati ya Wapalestina yatavuruga vibaya sana juhudi hizo na akatangaza kuwa itakuwa vigumu kwa Israil kufanya mashauriano nakundi ambalo haliamini kuwa Israili ina haki ya kuwepo kama taifa; jinsi wanavyoamini wanachama wa Hamas.

Alisema Serikali ya Marekani itaendelea kuchunguza kwa makili hatua zinazochukuliwa kuhusiana na uamuzi huo na Wapalestina siku na hata masaa yanayokuja.

Wamarekani na mataifa washirika wake wamesisistiza kuwa muda mrefu kuwa taifa lo lote la Wapalastina inapaswa kuwa lile linaloshutumua vita, litambue Israil na kukubalia mapatano yote yanayohusisha taifa hilo la Wayahudi.

Wapalestina wanasisitiza kuwa umoja wao utampa uhalali zaidi Rais Mahmoud Abbas, kufanya mashauriano kwa niaba yao kwa sababu atakuwa akiwakilisha Wapalestina wote na wala sio baadhi yao tu.

Wazanzibari waishio Tanganyika wapinga kugawanywa

Rais Jakaya Kikwete

Jumuiya ya Wazanzibari Waishio Tanganyika imekuja juu ikipinga vikali mikakati ya kuwabagua inayolenga kuwatisha ili kuwarudisha nyuma wasiendelee kudai mamlaka kamili ya Zanzibar pamoja na Muungano wa haki na wenye maslahi kwa pande zote mbili.

Mikakati hiyo inadaiwa kufanywa na watu wa kubuni wanaojiita Umoja wa Wapemba Waishio Tanzania Bara (Neppelta) kwa kutumia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, aliyoitoa wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba, Machi 21, mwaka huu.

Tamko la jumuiya hiyo lilitolewa na Mwenyekiti wake, Abdallah Mohammed Kassim, marufu kama “Dullah”, jijini Dar es Salaam juzi.

Alisema kauli ya watu hao, ambayo ilinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni, imeonyesha ubaguzi wa dhahiri dhidi ya Wazanzibari, ambao kiasili ni wamoja licha ya kutenganishwa na bahari.

Abdallah alisema hawakubaliani na kauli ya watu hao iliyosisitiza kuwa wao ni “Wapemba” kwa kuwa Zanzibar ni moja na maslahi yake ni ya wote.

“Kitendo cha kusisitiza kuwa Muungano ukivunjika watakaopata hasara ni Wapemba ni ubaguzi kwani Wapemba ni Wazanzibar hivyo kuwabagua ni kujenga chuki miongoni mwa raia wa visiwa hivyo viwili ambao ni wananchi wa nchi moja,” alisema Abdallah.

Alisema Muungano uliopo ni wa nchi mbili, ambazo ni Tanganyika na Zanzibar na kwamba, Zanzibar ni visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo kuendelea kuwabagua Wapemba kwa maneno na vitendo ni kutowatendea haki.

Abdallah alisema uamuzi wa Wazanzibari kuishi na kufanya kazi Tanganyika ni haki yao ya msingi, hivyo kuwajengea hofu ni kuwanyima haki hiyo na kuwafanya waishi kwa mashaka makubwa, kitu ambacho alisema siyo kizuri kwa raia.

“Jumuiya ya Wazanzibari tunaoishi Tanganyika tunauliza kauli iliyotolewa na bwana Shehe Haji Faki ambaye alijitambulisha kama Mwenyekiti wa Wapemba waishio Bara kwa kusema idadi ya Wapemba waishio Bara imeongezeka hadi kufikia zaidi ya watu 800,000 mwaka 2012 na mtaji wa trilioni 1.2, takwimu hizi amezipata wapi?” alihoji Abdallah.

Alisema uhusiano na mwingiliano baina ya Wazanzibari na Watanganyika vilikuwapo kabla ya Muungano wa mwaka 1964.

Hivyo, akasema kuishi katika nchi yoyote duniani hakutegemei Muungano, kwani wapo Watanzania wanaishi nchi mbalimbali duniani bila ubaguzi na hata Tanzania wapo raia wengi wa kigeni wanaoishi licha ya kuwa nchi hizo hawajaungana nazo.

“Wazanzibari waliopo Tanganyika na kumiliki ardhi na mali isiwe sababu ya kuwatisha na kuwajengea hofu ya kudai maslahi ya nchi yao, kwani utaifa wa mtu hauwezi kutupwa kwa sababu ya kumiliki ardhi, mali, kuoa au kuolewa,” alisema Abdallah.

Alisema umoja uliopo miongoni mwa Watanzania unakumbusha kuwa wanaofaidika na Muungano siyo Wazanzibari pekee, kwani faida hizo zipo kwa raia wa pande zote mbili za Muungano.

CHANZO: NIPASHE

Dk. Slaa: Upinzani hatuna lengo la kuvunja Muungano

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia (Chadema),Dk. Willibroad Slaa.

Katibu  Mkuu wa Chama cha Demokrasia (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, amewataka Watanzania kutambua kuwa hakuna chama cha upinzani ambacho kina lengo la kuvunja Muungano bali yanayoelezwa ni njama ya kudhoofisha msimamo wa kuwapo kwa serikali tatu.

Alitoa kauli hiyo jana katika viwanja vya Tangamano, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa jiji la Tanga, baada ya kuongoza timu ya viongozi wa juu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mjini hapa na kuwataka wakazi wa jiji hilo kukataa hadaa zinazofanywa kwa lengo la kukanyaga rasimu ya katiba, ambayo waliitolea maoni yao.

Alisema kilichofanywa na Rais Jakaya Kikwete, wakati akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba kuiponda rasimu ya katiba ni kumdhalilisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambaye ni kiongozi mwenye heshima Tanzania na nje ya nchi na kwamba, Ukawa itazunguka nchini kote kumtetea.

Dk. Slaa ambaye ni Mwenyekiti wa Ukawa nje ya Bunge hilo, alisema Rais Kikwete anawahadaa wananchi anaposema wanaotaka serikali tatu wana lengo la kuvunja Muungano na kusisitiza kuwa hakuna chama chochote cha upinzania, ambacho kinataka Muungano uvunjike.

“Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na wananchi wote wa Tanzania Bara na hata visiwani, hakuna anayetaka Muungano uvunjike, bali kinachofanywa na CCM ni kuwachonganisha kwa wananchi ili waonekane ni maadui wa Muungano,” alisema Dk. Slaa.

Alisema inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar ndani ya Bunge hilo wakidanganywa kuahidiwa kupewa fedha za kuwasomesha ili waunge mkono msimamo wa kupiga kura ya serikali mbili jambo ambalo ni kinyume cha malengo ya uwakilishi wao kwa Watanzania.

“Chini ya Umoja wao wa Ukawa wanachofanya ni kutetea maoni ya wananchi yaliyotolewa kwenye Tume ya Katiba kwa kuwa Tanzania ni nchi ya wote na hakuna, ambaye akifa atazikwa nje ya nchi hii. Hivyo, ni lazima kutetea maslahi ya wananchi,” alisema Dk. Slaa.

KAIMU KATIBU MKUU WA CUF ANENA
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Shaweji Mketo, alisema Tume ya Maridhiano ya Zanzibar inayoundwa na viongozi kutoka CCM na CUF ikiongozwa na Nassoro Moyo, imetoa tamko la kumtaka Rais asidhani Watanzania ni watu wa kuhadaiwa, bali watatetea serikali tatu kwa kuwa ina lengo  la  kuimarisha  Muungano  uliopo.

CHANZO: NIPASHE

Diwani mbaroni kwa kufunga ofisi za serikali

Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanya, Benson Mpesya akitoa maelekezo kwa fundi ili kufungua mlango unaodaiwa kufungwa na diwani na watu wengine watatu. Picha: Mohab Dominick.

Watu  watatu  akiwamo  Diwani wa Kata ya Mwendakulima ya Halmashauri ya Wilaya ya  Kahama mkoani Shinyanga,  Ntabo Majhabi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufunga ofisi za serikali za mtendaji wa kata hiyo.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo wiki iliyopita  asubuhi baada ya mtendaji wa kata hiyo,  Cecilia Clement kupigiwa simu na mlinzi wa ofisi hizo, Joseph Katambi na kumpa taarifa za tukio hilo liliofanywa na wananchi 15 walioambatana na diwani huyo.

Kwa mujibu mtendaji huyo, waliamua kuibadilisha kamati ya sungusungu ya kata hiyo hali ambayo ilianza kuleta malalamiko na minong’ono na kwamba huenda ni chanzo cha watuhumiwa hao kufunga ofisi hizo.

Aliwataja wengine walikamatwa kuwa ni fundi selemala,Hamisi Abbas  na Makaka Benedictor,  wakazi wa kata hiyo.

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kahama,  Benson Mpesya akiongozana na kamati ya ulinzi ya kata na askari polisi, walifika katika ofisi hiyo  kushuhudia mlango huo ulivyofungwa kwa kuwekewa kipande cha bati na kupigiliwa misumari  na mawe.

Mpesya  alitoa amri ya kuvunjwa kwa bati hilo chini ya ulinzi wa polisi na kuamuru waliohusika akiwamo diwani huyo kukamatwa na kutiwa mbaroni.

Akizungumzia kitendo hicho Mpesya, alisema ni fedheha na kisichoweza kuvumilika .

CHANZO: NIPASHE

Msekwa: Sitta ana lake jambo

Aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa 


Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta kukiri kuchezewa kwa saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msekwa amesema, ‘mzungumzaji huyo ana lake jambo’.

Sitta akizungumza na gazeti hili juzi mjini Dodoma alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya 1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.

Alifafanua kuwa saini ya Nyerere imeongezwa herufi ‘us’ kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno ‘Msekwa’ kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini walifanya makosa.

Msekwa akizungumza na gazeti hili jana alisema: “Saini iliyo katika hati original (halisi) ni ya kwangu mimi, lakini huyo anayesema zimechezewa muulizeni atakuwa na lake jambo. Kama kompyuta imekosea ni leo kwa kuwa kipindi hicho kompyuta hazikuwapo.”

Aliongeza: “Ana lengo gani la kutilia shaka, ana lengo gani la kusema imechakachuliwa, kinachotakiwa ni hati original ambayo iko ofisi ya Katibu wa Bunge itolewe, kwanini tuendelee kuandikia mate wakati wino upo?”

Maoni mengine

Mjumbe wa Bodi ya Kituo cha Taarifa kwa Wananchi Umma (TCIB), Hebron Mwakagenda alisema yote hayo yanatokea ni kuvuruga hoja iliyopo mezani.

Alisema kitendo cha kupoteza muda kuzungumzia suala la kuchezewa kwa saini halitakiwi kwani kama maudhui yake hayakuchezewa basi hoja ya muundo wa Muungano uamuliwe na wananchi wenyewe.

“Tusianze kupoteza muda kwa mambo ambayo hayapo cha msingi wananchi wenyewe waulizwe wanaupenda Muungano au la lakini tusianze kumtafuta mchawi kuwa saini zimechezewa wananchi waamue wenyewe kuhusu Muungano,” alisema Mwakagenda.

Sakata lilivyoanza

Utata huo ulianza wiki hii baada ya kamati za Bunge Maalumu la Katiba kuanza vikao vyake vya kujadili sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba, zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wake.

Hali hiyo ilitokana na kutopatikana kwa hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ile ya Sheria ya Baraza la Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa Muungano.

Aprili 2 mwaka huu, Kamati namba 2 ilimwalika, Spika Mstaafu wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, lakini uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa aliitwa kutokana na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha, alithibitisha kutokea utata huo na kwamba walilazimika kumuita Msekwa ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa na Msekwa alisema saini zilizopo katika hati hiyo ni ya kwake.

Nahodha alisema kwa maelezo ya Msekwa, inaonekana hati ya Muungano ipo Umoja wa Mataifa (UN), kwani kabla ya Muungano, Tanganyika ilikuwa na kiti chake UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hali kadhalika.

Aliongeza kuwa baada ya UN kuomba uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi kurejeshwa.

Kwa upande wake Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo siyo rahisi kuipeleka bungeni Dodoma.

Kamati kumi zaitesa CCM

 
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba 


Dodoma. Kura za awali katika Kamati 10 kati ya 12 za Bunge Maalumu la Katiba, zinakipa wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi,(CCM) kutekeleza azma yake inayotajwa kuwa ni kufumua Rasimu ya Katiba, ili kuondoa mapendekezo ya Muundo wa serikali tatu, baada ya wajumbe wa Zanzibar kukwamisha upatikanaji theluthi mbili.

Kwa mujibu wa taarifa za kamati, ambazo tangu juzi zimeanza kutolewa katika sura ya kwanza na sita zinazungumzia Muundo wa Muungano, wajumbe kutoka Zanzibar kwa sasa ndiyo kikwazo kikubwa kwa CCM.

Hata hivyo, uamuzi ya mwisho kuhusu Muundo wa Serikali, kati ya mbili au tatu, unatarajiwa kujulikana Alhamisi wiki ijayo, wakati kamati zote zitakapowasilisha taarifa zao na kupigwa tena kura kwa wajumbe Tanzania Bara peke yao na Zanzibar peke yao.

Iwapo wajumbe wa Zanzibar wakiitetea kwa theluthi mbili kama sasa, mapendekezo ya muundo wa serikali tatu ndiyo yatakayopelekwa kwa wananchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, baadhi ya wenyeviti wa kamati hizo, Stephen Wassira, Ummy Mwalimu, Anna Abdalah na Paul Kimili, walitaja moja ya vifungu ambavyo vimeshindwa kupata theluthi mbili kuwa ni ibara ya kwanza kifungu cha kwanza.

Akizungumza jana Wassira ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Namba Sita alisema kwamba katika kamati yake ibara hiyo imeshindwa kupata theluthi mbili, ili kuweza kufanyiwa marekebisho.

“Lakini huu siyo mwisho kama nilivyosema awali, tukirudi bungeni tutapiga kura kwa wajumbe wote na ndiyo itakuwa na uamuzi wa mwisho kama muundo wa Muungano utakuwa na Serikali tatu ama mbili, ambao utapelekwa kwa wananchi,” alisema Wassira.

Jussa, Lissu- tumeibana CCM

Jussa alisema: “Kwa taarifa za matokeo tulizonazo katika Kamati Namba 1, 2, 3, 4, 6, 10, 11 na 12 mapendekezo ya kubadilisha Rasimu katika ibara hizo mbili yamekwama. Kama CCM wakichakachua sura ya kwanza na sita, maana yake ni kwamba hapa hakuna Katiba, hakuna kura ya maoni na hakuna mwafaka.”

Vifungu hivi pia kwa mujibu wa wenyeviti wa kamati nyingine, isipokuwa kamati ya Tano, ambayo inaongozwa na Hamad Rashid, havikupata kura theluthi mbili na hivyo kubaki kama vilivyo kwenye rasimu.

Naye Lissu alisema kwa sasa CCM ndiyo inaweza kuanza mkakati wa kuvuruga Bunge kwani tayari wamejua hawana theluthi mbili ya Zanzibar ili kubadili Rasimu kama wanavyotaka.

Matumaini ya kupatikana MH370 yakolea

Operesheni ya kuitafuta MH 370 inaendelea.

Kiongozi wa operesheni ya kuitafuta ndege ya Malaysia ya MH370 iliyotoweka mwezi mmoja uliopita, Angus Houston wa Australia, amesema kuwa ametambua mawimbi ya sauti inayoaminika kutoka kwa kinasa sauti cha ndege hiyo maarufu kama 'black box' ya ndege hiyo.

Houston alisema kuwa kifaa maalumu kinachokokotwa na meli moja ya kijeshi ya Australia, Ocean Shield, kilipata mawimbi kamili kwa muda wa kati ya dakika tano u nusu na saba.

Mawimbi sawa na hayo yaliopatikana mwishoni mwa wiki na hii ina maana kuwa wataweza kulenga eneo ambalo inaaminika zaidi kuwa ndege hiyo ilianguka na kwa hivyo kuimarisha utafutaji wake.