Pikipiki.
WAENDESHA pikipiki (bodaboda) wachache
wamejitokeza kuchukua leseni maalumu za kusafirisha abiria katika
halmashauri za manispaa zao katika Jiji la Dar es Salaam kama
ilivyoamriwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchikavu na Majini
(Sumatra).
Kwa maneno mengine ni kwamba madereva wengi wa pikipiki wanaosafirisha abiria katika jiji hilo ni feki.
Licha ya wito huo kutolewa na Sumatra tangu mwisho
wa mwezi uliopita, ni watu wachache waliojitokeza kuchukua leseni hizo
ukilinganisha na mwitikio mzuri ulioonyeshwa na madereva wa magari ya
magurudumu matatu (Bajaji).
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Mfawidhi wa
Sumatra, Kanda ya Mashariki, Conrad Shio alisema kuwa wamesambaza
matangazo maeneo mbalimbali ambayo yanatumika kama vituo vya kuendesha
biashara yao ya kuchukua abiria.
Shio alisema kuwa idadi ya leseni zilizotolewa
katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam ni kama ifuatavyo; Kinondoni
wamesajili bodaboda mbili na bajaji 250, Ilala wamesajili bodaboda tatu
na bajaji 17 na Temeke wamesajili bodaboda 18 na bajaji 149 tu.
“Wamejitokeza wamiliki wachache waliokuja kusajili
vyombo vyao vya usafiri hasa bodaboda, hivyo wiki ijayo tutafanya
operesheni maalumu ya kukamata bodaboda na bajaji ambazo zitakuwa
hazijapata leseni za kusafirisha abiria katika Jiji la Dar es Salaam,”
alisema Shio.
Ofisa huyo aliongeza kuwa lengo la zoezi hilo ni
kuweka udhibiti katika vyombo vya usafiri ili kuwalinda zaidi abiria
dhidi ya ajali.
No comments:
Post a Comment