Mamilioni yatolewa kwa dijitali

 
Star Times. 


KATIKA mkakati wa kusambaza mawasiliano ya mfumo mpya  wa dijitali katika mikoa 14 nchini, jumla ya Sh50 milioni zimetolewa na Kampuni ya StarTimes ili kuwezesha kazi hiyo.

Meneja Habari wa StarTime, Erick David aliitaja mikoa ambayo kampuni hiyo imewekeza kuwa ni pamoja na Shinyanga, Iringa, Tabara,  Ruvuma, Mara, Kigoma  na Manyara.

David aliyasema hayo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, alisema hatua hiyo ni kuunga mkono Serikali kuhusu dhamira ya kusambaza mfumo  huo nchi nzima, ambapo inakwenda sambamba na kutoa huduma mpya ya kukodisha ving’amuzi kwa wateja.

Mikoa mingine ni Singida,  Kusini Pemba, Kaskazini Pemba na Rukwa, Mtwara na Lindi  na kwamba mikoa 23 inatarajia kupatiwa huduma hiyo kufikia mwisho wa mwaka huu.

“Huduma hii ya kukodisha ving’amuzi ni mpya  kutoka Startimes, kutatua changamoto zinazoikabili dijitali na kwamba mteja anatakiwa kutoa Sh39,000 kama dhamana ya kuchukua king’amuzi na pia mteja anatakiwa kulipa  Sh6,000 kama malipo ya kila mwezi  na itakuwa na chaneli 15 za nyumbani na nyinginezo,” alisema David.

Alisema mteja anaweza kurudisha  na akarudishiwa Sh39,000 aliyotoa kama dhamana baada ya matumizi yake na huduma hiyo inayolenga kuwanufaisha watu wa kipato cha chini kwani licha ya kukodishwa  utapata  channel zaidi ya 15 saa 24 kwa mwezi mzima.

Alisema katika kuifanya jamii kuwa karibu na ulimwengu huu wa dijitali na kuepuka  gharama kubwa za ununuzi wa ving’amuzi na malipo ya vifurushi kwa kila mwezi kampuni yao inarahisisha hilo.

No comments:

Post a Comment