MAWAZIRI na watendaji wa wizara mbalimbali
watakaokuwa wazembe, watachekechwa na kubaki wale ambao utendaji kazi
wao ni bora, baada ya kuzinduliwa kwa mpango maalumu wa kupima utendaji
wa kazi wa viongozi.
Mpango huo ulizinduliwa jana jijini Dar es Salaam
na Rais Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Katika nchi za Rwanda na Malaysia, ambako mpango
huo unatekelezwa, waziri anaposhindwa kufikia malengo yaliyowekwa katika
wizara yake, anahesabika kuwa ameshindwa kazi na hujiuzulu.
Kwa kuanzia, wizara zitakazoanza kutekeleza mpango
huo ni Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo na Chakula, Wizara ya
Uchukuzi, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi na Wizara ya Maji.
Akizungumzia mpango huo, Rais Kikwete alisema kuwa
ni busara kwa nchi kujifunza kutoka katika nchi zilizofanikiwa
kimaendeleo kama Uingereza, Vietnam na Malaysia, ambazo zinatekeleza
mpango huo.
Alisema Uingereza chini ya Waziri Mkuu wa zamani,
Goldon Brown, ilianzisha mpango kama huo na ulifanikiwa kwa kiasi
kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Nchini Malaysia, mpango huu unafanya vizuri
zaidi, waziri akishindwa kutekeleza miradi aliyopangiwa, akaitwa kwa
waziri mkuu, ina maana ameshindwa kazi na hawezi kuendelea tena kuwa
waziri,” alisema Kikwete.
Alisema kuwa mpango huo mpya una lengo la kutoa
majukumu kwa kiongozi mmoja, mmoja ili aweze kutoa matokeo mazuri ya
kazi zake na kwamba hilo ndilo litakalomfanya aendelee na wadhifa wake.
Katika tukio hilo, mawaziri wa wizara zilizo
katika mpango huo walisimama na kuahidi kutekeleza majukumu yao chini ya
mpango huo na kwamba hivi sasa watendaji mbalimbali wa wizara hizo wako
kwenye mafunzo maalumu kuhusu mpango huo.
Akizungumza, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe alisema kuwa mpango huo ukianza kutekelezwa utakuwa kiama kwa
viongozi wapenda vyeo, wasiotekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Utafika wakati watu watazikataa teuzi za uwaziri
kutokana na kazi zitakazokuwa mbele yao. Uongozi utakuwa mzigo mkubwa
badala ya sasa watu wanatuambia tumeula tunapoteuliwa kuongoza wizara,”
alisema Dk Mwakyembe.
Alisema: “Nchi ambazo mpango huo unatekelezwa,
Rais anaweza kuwaomba watu kadhaa wamsaidie kuongoza wizara na wakakataa
kwa sababu ya kufahamu kazi ngumu iliyo mbele yao.”
No comments:
Post a Comment