Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, amewata wakuu wa mikoa nchini kuondoa woga na kusimama
kidete, ili kukomesha vurugu zinazoendelea nchini yakiwemo mauaji
yanayotokana na imani za kidini.
Sitta ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki
alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Chama
Cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) katika ukumbi wa Chuo cha Mipango
mjini Dodoma.
Alisema kama wakuu wa mikoa hawatatimiza wajibu
wao, migogoro na visingizio vya imani za kidini vitaendelea kukithiri
siku hadi siku.
Waziri huyo alisema amekuwa akishangazwa na hatua
ya viongozi wa mikoa kushindwa kuzima maasi hayo mapema licha ya kuwa na
vyombo muhimu vinavyowapa taarifa za haraka.
“Wakati mwingine ni uoga wa viongozi wetu, ama kwa
kutokujiamini maana jambo linaaza kwao na wao wanakuwa na mamlaka zote
lakini wanashindwa kuchukua hatua mapema hadi Waziri Mkuu au Rais
aingilie kati, hii ni aibu kweli,” alisema Sitta. Waziri huyo aliwataka
viongozi wa mikoa kujenga ujasiri na kuwa wepesi wa kukabili matatizo
yanapotokea katika maeneo yao ili yasilete madhara makubwa katika jamii.
Kuhusu wanasheria, alisema licha ya Tanzania kuwa na chuo kikongwe cha
kisheria, lakini bado ina upungufu mkubwa wa wanasheria ikilinganishwa
na nchi kama Kenya ambayo wanasheria wake walianzia kusoma Tanzania.
Alisema kwa sasa watu waliosajiliwa kama wanasheria nchini Tanzania ni 3500 wakati nchi kama Kenya imesajili wanasheria 11,000.
“Chuo cha Lumumba ndicho Chuo kikongwe katika
Afrika Mashariki chenye kutoa taaluma ya sheria, lakini hadi sasa sisi
tunawasheria wachache ikilinganishwa na nchi za wenzetu na hasa Kenya,”
alisema.
Hata hivyo alisema kuwa mkatati wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki kwa sasa ni kufungua soko la pamoja kwa wanasheria, ili
waweze kufanya kazi katika nchi zote ndani ya shirikisho.
Kwa upande mwingine alisema changamoto kubwa
itakuwa ni katika masuala la lugha kwani bado Kiingereza kinaonekana
kuwa na nafasi kubwa lakini pia nchi kama Burundi wanatumia lugha ya
Kifaransa.
Kwa upande wake, Rais wa TLS Francis Stolla,
alikiri kuwa gharama za kisheria bado ziko juu ikilinganishwa na watu
wanaohitaji kuhudumiwa.
Wakati Sitta akieleza hayo, Shirika la Under The
Same Sun (UTSS) limeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kukomesha
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Limesema matukio hayo ya kikatili yanahusishwa na imani za kishirikina kwani mpaka sasa watu 72 wenye ulemavu wa ngozi wameuawa.
No comments:
Post a Comment