Mafao ya viongozi wastaafu yashtua

Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye 

WAKATI Watanzania kwa mamilioni wakiendelea kukosa huduma mbalimbali muhimu ikiwamo afya na njaa kutawala katika maeneo mengi nchini, imebainika kuwa viongozi wastaafu wanarundikiwa mafao.

Ukubwa wa mafao hayo na posho kwa marais, makamu wa rais na mawaziri wakuu wastaafu unatajwa kuwa huenda ndiyo chanzo cha uongozi kupiganiwa kwa udi na uvumba na kwa gharama yoyote, kutokana na kuwa vyeo hivyo huwanufaisha katika maisha yao yote na baada ya wao kufariki wategemezi wao huendelea kunufaika.

Sheria ya Mafao ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1999, ambayo ilirekebishwa mwaka 2005, inaeleza kuwa Rais Mstaafu anapomaliza kipindi chake cha uongozi, hupata mafao ya mkupuo.

Ingawa kiwango cha mshahara wa Rais wa Tanzania ni siri, sheria hiyo inaeleza kuwa mafao yao hukokotolewa kwa kuzingatia mshahara wa juu aliowahi kupata miezi aliyofanya kazi.

Kiwango cha mafao hayo hukokotolewa kwa kutumia kanuni za kiwango cha asilimia itakayopangwa na mamlaka husika.

Mbali ya mafao yake ya kazi, Rais Mstaafu hulipwa posho ya kila mwezi kiasi cha asilimia 80 ya mshahara wa rais aliyeko madarakani. Kiasi hicho ni sawa na Sh80 kwa kila Sh100 anayopata Rais aliye madarakani.

Licha ya posho hiyo, Rais hupewa ulinzi, msaidizi, katibu muhtasi, mhudumu wa ofisi, mpishi, dobi, mtumishi wa ndani, mtunza bustani, madereva wawili na gharama za mazishi atakapofariki.

Mafao mengine

Pamoja na malipo ya mkupuo anayopata Rais Mstaafu, pia anapewa pasi ya kusafiria ya hadhi ya kidiplomasia, yeye pamoja na mke au mume wake.

Rais pamoja na mke wake, pia hulipwa gharama za matibabu ndani au nje ya nchi.

Baada ya kustaafu rais pia hulipiwa matengenezo ya magari mawili yenye uzito usiopungua tani tatu, ambayo hutolewa na Serikali, ambayo pia hubadilishwa kila baada ya miaka mitano.

Kama hiyo haitoshi, Rais pia hujengewa nyumba mpya, ambayo ni lazima iwe na vyumba angalau vinne, viwili kati ya hivyo ni lazima viwe na huduma zote ndani (self-contained).

 

Aidha, nyumba hiyo ni lazima iwe na ofisi iliyokamilika na nyumba kwa ajili ya mfanyakazi wake.

Rais huyo mstaafu vilevile atagharimiwa gharama za mazishi pindi atakapofariki

Makamu wa rais na mawaziri

Mafao hayo ya viongozi wa umma yanampa nafasi Waziri Mkuu mstaafu na makamu wa rais fursa kama anazopata Rais, isipokuwa wao hawajengewi nyumba, pia wanapata gari moja tu.

Makamu wa rais na waziri mkuu wastaafu wanapewa fedha za kulipa mishahara ya watumishi, mpishi, dobi, mfanyakazi wa ndani, mtunza bustani na dereva.

Sheria hiyo inawakinga pia wategemezi wa viongozi wastaafu, hasa viongozi hao wanapofariki.

Kinga ya wategemezi wa viongozi hao iliundwa katika marekebisho ya Sheria ya Mafao ya Viongozi wa Siasa ya Mwaka 1999, ambayo ilitiwa saini na Rais mstaafu Benjamin Mkapa Juni 2005. Marekebisho yaliyotiwa saini na Rais Mkapa ni pamoja na kuwalipa mafao wajane na wagane wa viongozi wa juu wa kitaifa akiwamo rais, makamu wa rais na waziri mkuu.

Rais mstaafu akifariki dunia, mke au mume wake hupewa nyumba, posho kiasi cha asilimia 40 ya mshahara wa rais aliye madarakani.

Aidha, mjane au mgane huyo hutengewa fedha za matibabu ndani ya nchi na matengenezo ya gari analopewa na Serikali.

Pia hulipiwa mshahara wa kima cha chini kwa dereva na mtumishi wa ndani pamoja na hupewa usafiri wa kwenda mahali atakapoishi maisha yake yaliyosalia.

Mabadiliko hayo yalilenga pia kuhakikisha kuwa iwapo kiongozi husika alikuwa analipwa pensheni kwa ajira ya awali, malipo yake yataendelea kutumiwa na mjane.

Aidha katika kikao cha Bunge la Bajeti mwaka uliopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alisema kuwa Serikali imetenga Sh9 bilioni kwa ajili ya matibabu ya wastaafu wanaopaswa kutunzwa na Serikali.

 

Mawaziri wakuu waliostaafu na kunufaika na mafao hayo ni sita akiwamo, Joseph Warioba, Samuel Malecela, Cleopa Msuya, Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.

Marais wastaafu, wanaonufaika na mafao hayo kwa sasa ni Benjamin Mkapa aliyeiongoza Tanzania kwa miaka kumi, kati ya mwaka 1995 na 2005 na Ali Hassan Mwinyi aliyeongoza kati ya mwaka 1986 hadi 1995.

Akizungumzia unono wa mafao hayo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy alisema: “Huo ni mzigo, kwa Serikali” Alisema ni vyema kama hilo jambo likapelekwa bungeni ili lijadiliwe kwa kina.

Mbunge wa Viti Maalumu Chadema, Rose Kamili, alisema kuwa ni wakati wa wabunge kujenga hoja ili sheria hiyo ibadilishwe, kwani wapo wastaafu, ambao hawalipwi na wana madai ya muda mrefu.

“Mbona marais wakiwa madarakani tayari wanakuwa na fedha za kutosha, wanakuwa na mali na wameshawekeza kwa kiasi kikubwa, iweje wapate mafao makubwa kiasi hiki?” alisema akihoji.

Alisema kwamba mafao hayo pamoja na yale ya wanajeshi, Jaji Mkuu na IGP ni makubwa yakilinganishwa na uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment