NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba jana
alikutana na madudu katika uwanja mdogo wa ndege wa Moshi baada ya
kukuta sehemu ya kiwanja hicho imemegwa na kujengwa makazi ya watu huku
timu ya wawekezaji utoka Ufaransa ikiwa njiani kuja kukagua uwanja huo
kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Marubani.
Dk Chizeba alishindwa kuvumilia na kusema Tanzania
huenda ikapatwa na aibu wiki ijayo wakati timu ya wawekezaji hao
itakapowasili wakiwa na ramani inayotofautiana na ile ya sasa.
Ujio wa Dk Tizeba, unatokana na ombi la Mbunge wa
Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo aliyetaka aende mkoani humo kujionea
namna uwanja huo ulivyo katika hali mbaya.
Akiwa uwanjani hapo, Meneja wa uwanja huo, Francis
Massawe alimweleza naibu waziri huyo namna Halmashauri ya Manispaa ya
Moshi ilivyomega eneo la uwanja huo na kugawa viwanja vya makazi.
Naibu waziri huyo alishtushwa pia kukuta mnara wa
kampuni moja ya simu ukiwa umejengwa karibu na eneo la uwanja na kuhoji
ilikuwaje mnara huo ukajengwa hapo. Kutokana na utata huo, Dk Tizeba
aliagiza kuitwa kwa Mkuu wa Idara ya Mipango Miji wa Halmashauri ya
Manispaa ya Moshi, Alex Poteka na Ofisa Ardhi wake, Aloyce Msule ili
wajieleza.
Akijieleza katika kikao hicho, Poteka alisema eneo
la uwanja huo halijamegwa bali ni watu wamevamia eneo la dharura
(Buffer zone) na kwamba ukubwa wa eneo hilo uko kwenye ramani ya mwaka
1996/97. Kauli hiyo ilionekana kumchefua Dk Tizeba aliyehoji ilikuwaje
ramani mpya ya 1996/1997 wakati uwanja huo uko katika ramani kuu halisi
tangu 1954, ikiwa ni miaka 43 nyuma.
Dk Tizeba alimwagiza Katibu Tawala Mkoa
Kilimanjaro, Dk Feisal Issa, meneja wa uwanja, watendaji wa halmashauri
na wale wa wizara yake kukutana na kumpa ramani halisi.
Naibu Waziri huyo alimtaka Ndesamburo kuwaelimisha
wananchi wake ili wasipotoshwe baadaye kuwa yeye (waziri) amekwenda
Moshi kuchafua hali ya hewa wakati suala hilo linaungwa mkono pia na
mbunge wao.
Ndesamburo, alisema yeye yuko mstari wa mbele
katika kupigania kurejeshwa kwa eneo hilo la uwanja na ni mmoja wa
waliopaza sauti miaka ya 1990 uwanja ulipomegwa.
Alimsihi Dk Tizeba asiwaeleze watalaamu hao kuwa kuna tatizo la ardhi kiwanjani hapo kwani yatapatiwa ufumbuzi.
Ndesamburo alisema kujengwa kwa chuo hicho
kutaboresha uwanja huo na kutatoa fursa za kiuchumi kwa vile watalii
wanaokuja kupanda Mlima Kilimanjaro wangependa kushukia Moshi.
No comments:
Post a Comment