Chadema wambana Dk. Magufuli
Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimehoji sababu za Waziri wa Ujenzi,
Dk. John Magufuli, kumpigia debe mgombea urais wa Kenya, Raila Odinga,
kutaka awe Rais wa nchi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao nchini humo na
kutaka maelezo kama kitendo hicho ndiyo msimamo wa serikali au la.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chadema, Ezekia Wenje,
alisema wanataka maelezo hayo kutoka serikalini kwa kuwa kitendo hicho
cha Waziri Magufuli ni cha hatari.
Wenje, ambaye ni Mbunge wa Nyamagana (Chadema), alisema wanapinga
kitendo hicho cha Waziri Magufuli kwa kuwa kuna mikataba ya kimataifa
inayokataza nchi moja kujiingiza katika siasa za nchi nyingine na pia
kinaweza kuharibu uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Kenya.
Alisema kitendo hicho cha Waziri Magufuli kinathibitisha kuwa waziri
huyo alikuwa anafanya biashara ya mtu, hivyo akasema wanataka kujua mtu
huyo ni nani.
Wenje, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, alisema wanao uthibitisho kwamba, Chama cha Orange Democratic
Party (ODM) hakikukialika Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Mkutano Mkuu
wake uliotumiwa na Waziri Magufuli kumpigia debe Odinga na pia CCM siyo
chama rafiki wa ODM.
Alisema inawezekana Waziri Magufuli alihudhuria mkutano huo wa ODM kwa
nafasi yake ya waziri, lakini akaitumia vibaya nafasi hiyo au alikuwa
akiiwakilisha serikali.
“Kwa hiyo, tunaitaka serikali itoke hadharani iseme kama ndiyo msimamo
wa serikali ya Tanzania na Rais Jakaya Kikwete,” alisema Wenje.
Akizungumza katika mkutano huo wa ODM wiki iliyopita, Waziri Magufuli
alisema Odinga anastahili kuwa Rais wa Kenya kutokana na sifa zake za
uongozi na kwamba, hakuna sababu zozote zitakazowafanya Wakenya
wasimchague.
Waziri Magufuli alisema kati ya wagombea wote waliojitokeza kuwania kiti
cha urais nchini Kenya, hakuna anayemfikia Odinga na hiyo inaonyesha
kuwa wakimchagua atawasaidia bila ubaguzi.
Alisema na hata Odinga, ambaye ni Waziri Mkuu wa Kenya, akiamua kugombea ubunge katika Jimbo lake la Chato, hawezi kumshinda.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema jana kuwa hadi jana
jioni alikuwa akimtafuta msaidizi wa Waziri Magufuli ili kumpata waziri
huyo, lakini hadi tunakwenda mitamboni jitihada zake zilikuwa hazijazaa
matunda.
No comments:
Post a Comment