‘Watoto wa viongozi wasisome nje’
Baadhi
ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wameitaka katiba mpya itamke kuwa
watoto wa viongozi wote wa nchi kusoma katika shule za serikali kuanzia
ngazi ya msingi hadi elimu ya juu.
Walisema hayo jana, wakati wakitoa maoni ya katiba mpya mbele ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba katika viwanja vya Shule ya Msingi Magomeni,
jijini Dar es Salaam.
Joshua Mutale, alisema kwa kufanya hivyo itahamasisha umakini wa
viongozi kuweka msisitizo katika suala la elimu hasa katika shule za
kata kuliko ilivyo sasa.
“Kama kiongozi akisomesha mtoto wake katika shule za serikali kwa ngazi
zote ni rahisi kuyatambua mapungufu yaliyopo katika shule hizo na
kuyatatua kwa haraka,” alisema Mutale.
Christian Kauzeni, alisema endapo jambo hilo litawekwa katika katiba
mpya na kufuatwa kama sheria litapunguza matabaka yaliopo kati ya shule
za serikali na zile za binafsi.
Aidha, baadhi ya wachangiaji walipendekeza katiba ipige marufuku
sviongozi wa serikali kutibiwa nje ya nchi na endapo ikitokea atapelekwa
huko avuliwe uongozi kwa muda na atibiwe kama raia wa kawaida.
Suleimani Juma, alisema hatua hiyo itaepusha mikataba ya ubinafsishaji
wa rasilimali za nchi kinyemela inayoweza kufanyika kupitia matibabu
hayo.
Mutale alisema baadhi ya viongozi hutumia mwanya wa matibabu kusaini mikataba ya uwekezaji wa rasilimali muhimu zilizopo nchini.
No comments:
Post a Comment