Dar wafurahia ‘treni la Waziri Mwakyembe’



WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaamu, wameeleza jinsi wanavyoendelea kunufaika na kupata faraja kupitia usafiri wa treni zinazofanya safari zake katikati ya jiji.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema kuwa wanafurahia na wanakuwa na matumaini makubwa kwa kiongozi wao aliyekaa kuwafikiria juu ya adha ya usafiri wanayoipata na kuamua kufufua usafiri huo.


“Imani yetu sasa ni kwamba wapo viongozi wanaoweza kuweka mbele masilahi ya taifa na hata kama angetaka michango kuhusu suala jingine inakuwa rahisi kuchangia kwa sababu tuna imani naye,” walisema wananchi hao.


Farida Jamal mkazi wa Ubungo alisema kuwa usafiri wa treni umemrahisishia kazi zake nyingi ambazo anazifanya kwa wakati unaotakiwa.


“Mimi kama mfanyabiashara ambaye nategemea sana usafiri ili kuwafikia wateja wangu kwa urahisi treni imekuwa mkombozi wangu kibiashara,” alisema Jamali.
“Naweza kufanya kazi zangu za kibiashara hasa katikati ya jiji kwa haraka zaidi bila kutumia muda mwingi pia foleni hainisumbui kama awali,” aliongeza.


Kwa upande wake Abubakari Mtoi alisema kuwa anaweza kuwahi majukumu yake ya kila siku bila kusumbuka na foleni za daladala ambazo huwafanya watu wengi kuchelewa katika shughuli zao.


Aidha, wananchi hao waliwaomba viongozi Tanzania kuiga mfano bora kutoka kwa Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe wa kufufua vitu vyenye manufaa kwa umma.


Mkazi wa eneo la Matumbi jijini hapa Athuman Idd alisema yeye anamshukuru Mungu kwa kumponya Mwakyembe ili awatumikie wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Idd alisema Mwakyembe ni kiongozi ambaye kwa vitendo ameonyesha kuuchukia ufisadi na kufanya kazi kwa manufaa ya Watanzania.


‘Fikiria alivyoweafumua viongozi wa Kampuni ya Ndege (ATCL), viongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na kusimamia vizuri TRL”, alisema na kusisitiza kwamba waziri yeyote kwa sasa lazima asiowaonee haya wakuu wa mashirika wanaokula fedha za umma.


Wakati huohuo habari kutoka Shinyanga na Mwanza zilisema wakazi wa huko walikesha wakiimba baada ya kuona treni likipita tena baada ya kuacha njia hiyo tangu 2009.

No comments:

Post a Comment