Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai (DCI), Robert Manumba
HATIMAYE Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai (DCI), Robert Manumba amesafirishwa kupelekwa
nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Jaffer
Dharsee ambako Manumba alikuwa amelazwa katika Chumba cha Wagonjwa
Mahututi (ICU) tangu Januari 13, mwaka huu, amethibitisha kusafirishwa
kwa kiongozi huyo wa Polisi.
“Ni kweli amesafirishwa jana (juzi),kwenda Afrika
Kusini, akiwa katika hali ya kuridhisha, ila sijajua bado jina la
hospitali aliyopelekwa,”alisema Dk Dharsee.
Akizungumza na gazeti hili juzi mchana, kabla ya
kusafirishwa Manumba, Dk Dharsee alieleza kuwa hali ya kiongozi huyo
sasa inatia matumaini kwani ameweza kujitingisha baadhi ya viungo vya
mwili wake, tofauti na awali alipofikishwa hospitalini hapo.
“Anaendelea vizuri, licha ya kwamba yupo ICU,
lakini anatia matumaini kwa sababu kwa sasa naweza kusema amepata
ufahamu, kwani anaonyesha kuwa ana maumivu,hata uso wake sasa
umebadilika tofauti na awali alipokuwa hajitambui,” alisema Dk Dharsee.
Awali Dk Dharsee alithibitisha kuwa Manumba
anasumbuliwa na malaria kali baada ya kumfanyia uchunguzi na kukutwa na
wadudu 500 wa ugonjwa huo hatari, hali ambayo ilisababisha apoteze
fahamu na figo zake zote mbili kushindwa kufanya kazi.
Kwa upande wa Mganga Mkuu Mwelekezi wa Polisi, Dk
Ahmed Makata aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu jana kuwa,
kusafirishwa kwa Manumba kumefanikiwa baada ya afya yake kuimarika vyema
tofauti na ilivyokuwa awali.
“Mimi kwa sasa nipo Tanga, lakini imewezekana
kumsafirisha kwa kuwa afya yake imeimarika, yaani presha, mzunguko wake
wa damu kwa kifupi ni kwamba imewezekana kwa sababu yupo vyema sasa
tofauti na awali, ambapo ilishindikana kumsafirisha,”alisema Dk Makata.
Msemaji wa Polisi, Advera Senzo alipohojiwa kuhusu
kusafirishwa kwa Manumba, alithibitisha, lakini hakuwa tayari kueleza
amesafirishwa wakati gani, ndege iliyomsafirisha, wala hospitali
aliyopelekwa.
“Taarifa ninayokupa ni hii, amesafirishwa jana
(juzi) kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi basi hayo mengine mimi
sikwambii kwa sasa, lakini amefika salama,” alisema Senso.
Tangu alipolazwa katika Hospitali ya Aga Khan
chumba cha ICU, akiwa hajitambui huku akipumua kwa msaada wa mashine,
viongozi mbalimbali wakiwamo wa Serikali walimtembelea ili kumjulia
hali.
Miongoni mwa viongozi waliomtembelea ni pamoja na
Rais Jakaya Kikwete na mkewe mama Salma Kikwete, Makamu wa Rais Dk
Mohamed Gharib Bilali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na mke wake mama Tunu
Pinda.
Viongozi wengine ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein
Mwinyi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emanuel Nchimbi na Naibu
wake, Pereira Silima, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa na Mkuu wa
Polisi, Said Mwema na maofisa wengine wa Jeshi la Polisi.
No comments:
Post a Comment