NINAJIBU tahariri ya gazeti hili, toleo la
Jumanne, Januari 15, 2013 iliyokuwa na kichwa cha habari, ‘Kiingereza
sasa ndiyo lugha ya dunia’
Tahariri hiyo ililenga kupinga hoja zilizotolewa
na Mamlaka za Elimu Tanzania ambazo zote kwa pamoja zilipendekeza hivi
karibuni kuwa Kiswahili iwe ndiyo lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya
msingi hadi chuo kikuu.
Mamlaka hizo ni Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),
Baraza la Mitihani (NECTA), Tume ya Taifa ya Sayansi (COSTECH), Baraza
la Taifa la Ufundi (NACTE), Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA).
Kwa hakika mamlaka hizi zinastahili pongezi kwa kutoa maoni hayo kwani yamegusa panapotakiwa.
Katika tahariri yenu mlitoa hoja mbalimbali
kuhusiana na mapendekezo hayo ya mamlaka za elimu mkionyesha kuwa
kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia kutaiondoa Tanzania katika
ramani ya dunia jamani!
Wahenga husema mkataa kwao ni mtumwa! Labda kwa
nafasi hii ndogo nijibu hoja zenu na niwaongezee hoja zaidi ili muweze
kuwa wazalendo na kuelewa kwa nini wadau wa Kiswahili tunadai haya.
Mamlaka hizi zimezingatia mahitaji ya wateja wao,
ambao ni watahiniwa, wanafunzi Watanzania wa ngazi mbalimbali za elimu
ambao mamlaka zimegundua kuwa kuendelea kutumia Kiingereza ni kushusha
kiwango cha elimu nchini, huo ni ukweli usiopingika.
Mimi kama mwalimu wa sekondari na hata vyuo
naamini kuwa mwanafunzi katika somo la Uraia (Civics) anaulizwa kwa
Kiingereza kutaja rangi zilizopo kwenye bendera ya taifa lake aelezee
zina maana gani, haieleweki.
Wanafunzi wetu wanashindwa kueleza hayo kwa
Kiingereza. Je, vipi swali kama hilo mwanafunzi angetahiniwa kwa
Kiswahili, angeshindwa? Kujua elimu hii ya uraia ni suala la dunia au
ni letu?
Ni vyema mkatambua kuwa maarifa na lugha ni vitu
viwili tofauti. Mtu anaposomeshwa Jiografia, Historia, Fizikia n.k.
lengo ni kupata maarifa hayo, ili yaweze kumnufaisha yeye na jamii yake,
kama ilivyo kwa waandishi wa habari wenye taaluma ya habari, mnatupatia
elimu na kutuhabarisha Watanzania kwa Kiswahili, ingawa huenda
mlisomeshwa kwa Kiingereza.
Lakini, mkitumia Kiingereza ni Watanzania wangapi
wangejua mnachotuhabarisha? je, nyie waandishi ni wangapi wanaoweza
kuandika Kiingereza fasaha na sanifu? Je, mauzo ya gazeti lenu la
Kiingereza na ya Kiswahili yapo sawa?
‘Kiingereza ni cha dunia, Kiswahili ni cha kwetu’,
mlisomeshwa kwa Kiingereza mnatuhabarisha kwa Kiswahili kwa faida ipi?
Ni bora mkasomeshwa kwa Kiswahili na pengine maarifa yenu yangekuwa
makubwa mno, mngetunufaisha na elimu yenu.
Hakuna mgonjwa atakayekwenda hospitali akatibiwa
kwa Kiingereza. Hakika atatibiwa kwa lugha anayoielewa na maarifa ya
daktari wake hata kama kayapata kwa lugha ya Kirusi, Kijapani ai
Kiarabu, lakini akimhudumia Mswahili atapona. Barabara nzuri na majengo
mengine yanajengwa na Wachina, Wakorea ni maarifa waliyonayo na si
lugha?
Mlitoa hoja ya uongozi wa awamu mbalimbali kutokufanya uamuzi wa
kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia mkimtaja Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, pia Ali Hassan Mwinyi.
Hii ni hoja
nyepesi, kwani yapo mambo mengi ambayo viongozi wetu waliopita
hawakuyatimiza katika vipindi vilivyopita, lakini awamu nyingine za
uongozi yametimizwa na kuendelea kufanyiwa kazi.
Pia, umezipa fursa hata mamlaka za elimu za Tanzania kueleza kile kilichokuwa kinawakera na kuwatesa wateja wao kwa muda mrefu.
Madai hayo pia yanatakiwa yatambue kuwa maendeleo ya Kiswahili wakati wa Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi si kama yalivyo hivi leo.
Hivi leo, Kiswahili kimekua na kinazungumzwa na watu zaidi ya milioni 120 duniani.
Pia, kinafundishwa katika vyuo vikuu mbalimbali duniani kama vile, Ufaransa, Marekani, Japan, Urusi, China n.k.
Hali kadhalika, vyombo vya habari vya kitaifa na
kimataifa vinavyotumia Kiswahili vimekuwa vingi, mfano: BBC (iliyompa
sifa na umaarufu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi
Communications, Tido Mhando ambaye ni kipenzi chetu katika kukuza
Kiswahili kupitia vyombo anavyosimamia pia katika gazeti la Mwananspoti.
Leo
pia tunashuhudia BBC wakirusha matangazo ya Kiswahili kupitia kwenye
runinga huku watangazaji wao, Salim Kikee, Charles Hillary na wengineo
wakitamba kwa Kiswahili.
Pia, kuna Redio Deutsche Welle ya Ujerumani, Idhaa
ya Kiswahili ya Iran kuna wahariri wenu, Hawra Shamte ambaye
anatangaza huko kwa Kiswahili fasaha. Pia, Redio ya Kimataifa ya
Ufaransa, Sauti ya Amerika na nyinginezo
Nchini mwetu Kiswahili kimekuwa na mafanikio
makubwa. Hivi juzi Bunge liliridhia kuanzishwa kwa Kamisheni ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki ambayo makao makuu yake yapo Zanzibar,
tumeshuhudia kozi za Kiswahili katika vyuo mbalimbali nchini. Vilevile,
vitabu vya fani za sayansi na kompyuta kwa Kiswahili.
Kwa hiyo, ni wakati sasa Kiswahili kitumike
kufundishia kwani huwezi kulinganisha na kipindi cha nyuma na wakati huu
wa utandawazi.
Madai yenu kuwa hoja zetu ni za matege kwa kuwa
zinatolewa kiharakati na kiitikadi kwani tunadhani kuwa tukitumia
Kiswahili huo utakuwa mwisho wa wanafunzi kufeli.
Napenda mfahamu kuwa, Wataalamu wanasisitiza
kwamba lugha inayofaa kufundishia ni ile ya kwanza, lugha hiyo
huwasaidia wanafunzi siyo tu kujenga moyo wa kujiamini, bali pia katika
kuelewa upesi, kufikiri kwa haraka na kujieleza kwa urahisi kwa kutumia
lugha ya Kiswahili ni dhahiri wanafunzi wetu watakuza stadi zao katika
kusikiliza, kuzungumza kusoma na kuandika.
Hapa msisitizo ni kuwa mwanafunzi huhitaji kupata
maarifa zaidi siyo tu kutoka kwa mwalimu, bali pia hupata maarifa kutoka
katika vitabu, redio, luninga na watu mbalimbali.
Napenda mtambue
kuwa mfumo wa teknolojia, soko la ajira, kazi, biashara na siasa, siyo
kweli kwamba tutavikosa kwa kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia.
Hayo ni mawazo mgando ni ukweli ulio dhahiri kuwa
zipo nchi nyingi ambazo zinatumia lugha zao za asili na zimepiga hatua
kubwa katika maendeleo. Mfano, China, Norway, Ufilipino n.k.
Licha
ya hayo, ifahamike kuwa wadau wa Kiswahili hatusemi kwamba Kiingereza
kisifundishwe, hapana, tunachopendekeza ni Kiswahili kitumike kama lugha
ya kufundishia na Kiingereza kifundishwe kama somo linalojitegemea na
kwa ustadi na weledi mkubwa, ili wanafunzi wetu waweze kukimudu vizuri
na kuwakutanisha na jamii za kimataifa, tofauti na sasa ambapo
mwanafunzi hupewa maarifa kwa Kiingereza na yanatolewa kwa Kiswahili,
yaani ni vurugu tupu.
Mamlaka zimenena nasi wadau tunataka lugha yetu adhimu ya Kiswahili ndiyo iwe lugha ya kufundishia.
Napenda kutumia fursa hii kuwaeleza Mwananchi na
watendaji wake kwamba mmenufaika na Kiswahili msikipinge bali ni vyema
mkaendelea kutuunga mkono tunaotaka kukiendeleza.
No comments:
Post a Comment