Baadhi
ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamependekeza muundo wa Katiba utoe
mamlaka kwa Mahakama kutangaza matokeo ya uchaguzi na kuwapa nguvu
wananchi kuhoji matokeo hayo ikiwa imebainika kuwapo na matatizo,
badala ya kuiachia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Wakazi hao walisema hayo wakati wakitoa maoni yao kwa tume ya mabadiliko
ya katiba jana jijini Dar es Salaam, katika mchakato unaoendelea ikiwa
ni awamu ya nne tangu uanze.
Walisema katiba iliyopo haitoi fursa kwa wananchi kuhoji matokeo ya
uchaguzi hata kama kunaonekana kuwapo na matatizo hususani upande wa
Rais.
“Nafasi ya Rais imepewa kinga kubwa sana katika uchaguzi, hata pale
matokeo yanaponekana kuwa na utata, wananchi wanashindwa kuhoji kwa kuwa
Katiba haijaruhuru kufanya hivyo,” alisema Jackson Makala.
Kwa mujibu wa katiba ya sasa, baada ya Nec kutangaza matokeo ya uchaguzi
wa Rais, hakuna chombo chochote kinachoweza kuhoji, ikiwemo Mahakama.
Kwa upande wake Ntogwa Manamba, aliomba katiba mpya imuondolee Rais
nafasi 10 za kuteua wabunge, badala yake nafasi hizo waongezewe wanawake
wa viti maalum.
Aliongeza kwamba nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya wasiteuliwe na Rais,
bali zitangazwe nafasi za ajira kama zinavyotangazwa nafasi nyingine
za kawaida.
Kuhusiana na suala la Muungano, wananchi hao wameiomba tume ya
mabadiliko ya katiba kuwaunganisha Watanzania kutoka Zanzibar na Bara
ili wapige kura ya maoni juu ya muungano huo.
“Katika suala la Muungano ni lazima maamuzi magumu yafanyike, Watanzania
wa pande zote mbili wapige kura waamue kuuvunja au kuendelea nao,”
Julius Agensi.
Aliongeza: “Hakuna haja ya kuendelea kulumbana la suala moja la muungano, tunaomba maamuzi yafanyike suluhu ipatikane kwa kura.”
Suala jingine lilionekana kutolewa maoni sana na wananchi hao, ni kutaka
katiba mpya iainishe nafasi ya vyombo vya habari kuwa mhimili wa nne.
No comments:
Post a Comment