Sh Milioni saba ‘zafichwa’ akaunti binafsi
Mratibu Elimu kata wilayani Nzega mkoa wa Tabora amekiri kuchukua pesa za ujenzi wa shule na kuweka kwenye akaunti yake.
Mratibu huyo, Richard Nkwabi wa Kata ya Puge wilayani Nzega alikiri
kuweka fedha hizo baada ya malalamiko ya wananchi wa kata hiyo
kumshutumu yeye pamoja na diwani Alex Nyasani kujichukulia maamuzi ya
kuweka pesa za maendeleo ya ujenzi wa majengo mawili ya shule ya kidato
cha tano na sita ya shule ya sekondari Puge kwenye akaunti binafsi.
Shutuma nyingine zilizotolewa na wananchi hao kwa viongozi wao ni
kutekeleza mradi wa madarasa hayo na kuuhamishia sehemu nyingine kwa
lengo la kujitafutia njia ya ‘kutafuna’ pesa hizo za serikali.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu toka wilayani Nzega,
Nkwabi alikiri na kusema kiasi cha Sh.milioni 7.4, zimewekwa katika
akaunti yake Novemba 30, mwaka huu katika benki ya NMB tawi la Nzega
kutokana na kutekeleza maamuzi ya Kamati ya Maendeleo ya Kata (OBC).
"Kweli kiasi hicho kimewekwa katika akaunti yangu ya NMB tawi la Nzega,
lakini nimetekeleza maagizo ya OBC yaliyonitaka nifanye hivyo...hizo ni
kati ya Sh.milioni 13 zilizotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa
ajili ya ujenzi wa shule," alisema Nkwabi.
Nkwabi alisema Sh.milioni sita kati ya 13, zilitumika kununulia vifaa
vya ujenzi yakiwemo mabati, lakini kiasi kilichobaki kamati iliamua
ziwekwe kwenye akaunti binafsi hadi hapo watakapofungua ya kamati ya
ujenzi.
“Kweli pesa ziliingia tangu Juni mwaka huu, lakini kutokana na kuhofia
kurejeshwa zilikotoka, ikaamuriwa nyingine zitumike kwa kununulia vifaa
na nyingine ziwekwe kwenye akaunti yangu,” alisema.
“Tunaamini lengo la viongozi hao na kamati yao, walikuwa na mpango wa
kutafuta njia ya kuudhoofisha mradi huo ikiwa ni pamoja na kuhamisha
ujenzi ambao tayari ulikuwa umeanza sehemu iliyopendekezwa na wananchi
na kupeleka kwingine, lakini mbaya ni pesa za mradi kuwekwa akaunti
binafsi,” alisema mmoja wa wananchi walalamikaji.
Aidha, walielekeza shutuma kwa Diwani wao, Alex Nyasani kwa kuruhusu
ujenzi kufanyika wa shule kufanyika sehemu nyingine bila kuhusisha vikao
vya wananchi wenye kutoa maamuzi.
Lakini wananchi hao wanasema, mvutano uliopo sasa na viongozi wao ni
kushindwa kuwaeleza kuiendeleza shule hiyo ambayo ilipewa baraka na
viongozi wa serikali na pesa zake kupewa halmashauri ili izigawe kwa
ajili ya muendelezo wa shule hiyo ambayo mpaka sasa madarasa yake mawili
yamesimama hatua ya madirishani.
Pia, wananchi hao walisema madarasa ya shule hiyo yamejengwa sehemu
yenye nafasi na pia ni jirani na ilipo hosteli ya wanawake wa shule ya
Puge, jengo la utawala na maabara, hivyo kuanzishwa kwa ujenzi mwingine
kunaashiria ‘utafunaji’ wa pesa hizo.
Hata hivyo, diwani wa kata hiyo, Nyasani akizungumzia shutuma hizo za
wananchi wa kata yake, alisema hayana msingi kutokana na kinachofanyika
ndicho kinachotakiwa kwa ajili ya maendeleo ya kata ya Puge.
Wakati Nkwabi akikiri kuweka pesa za ujenzi wa shule katika akaunti
yake, diwani Nyasani alimtetea na kusema hakuna kitu kama hicho, na
kuirushia mpira kamati ya maendeleo ya kata.
No comments:
Post a Comment