CCM chakipongeza Chadema kwa kukitua 'mzigo'


Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rufiji kimepongeza hatua ya Chama cha Chadema kumchukua aliyekuwa kada wake Seleman Ndumbugani na kueleza kuhama kwake sawa na kuutua mzigo ulioshindikana.

Akizungumza na NIPASHE Jumamosi, Katibu wa Uenezi na Uhamasishaji wa Wilaya hiyo, Hemed Mnyeresa alisema CCM kamwe haisikitiki kuondoka kwa mwanachama wake huyo wa siku nyingi kutokana na kuwepo kwake kulikuwa na migogoro isiyokwisha na kusababisha chama hicho kuyumba.

Alisema kauli ya Ndubugai ambaye alikuwa Katibu wa Uenezi na Uhamasishaji wa Wilaya hiyo, kwamba ameondoka ndani ya Chama hicho kwa sababu kinaendeshwa kiukoo, hazina msingi na badala yake alimtaka aseme ukweli kilichomfanya aondoke.

Ndubugai alikihama chama hicho na kuhamia Chadema Desemba 13, mwaka huu, ambapo alinukuliwa na vyombo vya habari akisema aliondoka CCM kutokana na chama hicho Wilaya ya Rufiji kutawaliwa kiukoo.

Mnyeresa alisema chama hicho kinaendelea kuwabaini na kuwaondoa wanachama wote wanaodhani uongozi ni mali yao na kuwepo kwao humo ni moja ya maisha yao.

"Hatutaki watu wanaodhani wao hawawezi kushindwa kwenye uongozi na kuona ni mali yao milele, tunaendelea kuwasaka watu wa aina hiyo na kuwapa mkono wa kwaheri wakishindwa kufuata kanuni na maadili ya chama," aliongeza kusema katibu huyo.

Alisema Ndubugai aliingia nyongo na kuchukua hatua hiyo baada ya kushindwa nafasi hiyo katika uchaguzi uliopita, ambapo alianza kufanya mambo mbalimbali yanayokwenda kinyume na chama hicho na alipoona kuna dalili ya kumuondoa aliamua kujiondoa mwenyewe.

Hata hivyo, katibu huyo alieleza kwa sasa CCM imejikita katika kuhakikisha kinaondoa kero zinazowakabili wananchi wa chama hicho ikiwemo kuishinikiza serikali kutafuta soko la korosho pamoja na kusimamia usambazaji wa zana za kilimo katika msimu huu wa kilimo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment