Baadhi ya shule za kidato cha tano kukosa wanafunzi

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako akionyesha karatasi ya majibu ya mmoja wa watahiniwa wa mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2012, Dar es Salaam

KUNA kila dalili kwamba baadhi ya shule za sekondari zenye mikondo ya kidato cha tano zitakosa wanafunzi wa kujiunga nazo kwa masomo hayo mwaka huu kutokana na matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne.


Kadhalika, tatizo hilo litaviathiri vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu na kati, ambazo hutegemea wanafunzi hao kwa ajili ya kujiunga na kozi mbalimbali baada ya kuhitimu na kufaulu kidato cha sita.


Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne yalitangazwa mwanzoni mwa wiki hii na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa yakionyesha kuwa wanafunzi waliofaulu kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu ni 23,520, idadi ambayo kwa vyovyote haitakidhi mahitaji ya nafasi za kidato cha tano zinazokadiriwa kufikia 45,000 kwa sasa.


Mwaka jana wanafunzi 31,516 walichaguliwa kuingia kidato cha tano katika shule 201 za Serikali. Hivyo, hata kama wanafunzi wote waliopata madaraja ya I– III watachaguliwa kwenda katika shule hizo hawatatosheleza kwani kutakuwa na upungufu wa wanafunzi wapatao 8,000.


Hao ni mbali ya wale waliojiunga na masomo hayo katika shule binafsi za sekondari zinazokadiriwa kufikia 300 na ambazo tayari zimeanza kutafuta wanafunzi wa kidato cha tano kwa kutoa matangazo kwenye vyombo mbalimbali vya habari.


Takwimu za Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), zinaonyesha kuwa watahiniwa wa shule (school candidates) wanaoendelea na mitihani ya kidato cha sita kwa sasa ni 43,309, lakini kutokana na shule nyingi kuanzishwa, mahitaji yanatarajiwa kufikia 45,000.


Hiyo inamaanisha kwamba wanahitajika wanafunzi wa ziada 21,480 kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano kwa shule za Serikali na binafsi, idadi ambayo kama ni lazima ipatikane, hata waliopata daraja la nne (division four) watachukuliwa kuziba pengo hilo.


Hata hivyo, wanafunzi wanaochaguliwa kuingia kidato cha tano na baadaye kuruhusiwa kufanya mitihani ya kidato cha sita lazima wawe ni wale waliofaulu kwa kiwango cha kupata alama ‘C’ katika masomo matatu ya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne.


Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya shule zinahitaji idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha tano. Mkoani Mbeya Shule ya Sekondari Sangu ina uwezo wa kupokea wanafunzi 600 kwa mwaka, Southern Highlands 100, Meta 600, Mbalizi 250 na Loleza 450.
Mkoani Kilimanjaro, utafiti unaonyesha kuwa Bendel Memorial inahitaji wanafunzi 30, Majengo 600, Mariagoreti 150, Kibosho Girls 140, Visitation 30 na Kiraeni 40.


Hali kama hiyo pia inaonekana mkoani Arusha ambako shule zina mahitaji makubwa zikiwamo Arusha Sekondari 150, Enaboishu 150, Arusha Meru 140 na Arusha Mordern 150.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, watahiniwa waliopata daraja la kwanza ni 1,641, daraja la pili ni 6,453, daraja la tatu 15,426, daraja la nne 103,327, wakati waliopata sifuri ni 240,903 ambayo ni zaidi ya asilimia 60 ya watahiniwa.


Viongozi na wahadhiri katika baadhi ya vyuo vikuu nchini wamesema matokeo hayo yana athari kubwa ya upatikanaji wa wanafunzi wa kujiunga na vyuo hivyo miaka miwili ijayo.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Taaluma), Profesa Makenya Maboko alisema kama idadi ya wanafunzi waliofaulu ni hiyo, vyuo vitapata wanafunzi pungufu kuliko ilivyozoeleka.


Shirika la HakiElimu katika taarifa iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Elizabeth Missokia lilisema: “Wanafunzi watakaochaguliwa kuingia kidato cha tano wawe ni wale waliofaulu tu na siyo kuwapeleka hata wenye daraja la nne kwa lengo la kujaza nafasi kama ilivyofanywa kwa waliojiunga kidato cha kwanza mwaka 2013.”

 Hata hivyo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema wanafunzi watakaochaguliwa kwenda kidato cha tano ni wale watakaokidhi vigezo vya kitaaluma na kwamba nafasi nyingine zitabaki wazi kutokana na wanafunzi kufeli.

Watakaochaguliwa
Naibu Waziri Mulugo alikiri kwamba idadi ya wanafunzi watakaochaguliwa kuingia kidato cha tano lazima iwe ndogo kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne.
“Kimsingi hatuwezi kuwa drived (kuongozwa) na nafasi nyingi zilizopo kwenye shule zetu, maana lazima tuzingatie sheria katika kuchagua wanafunzi wa kwenda elimu ya juu, kwa hiyo tutachagua kutoka miongoni mwa hao waliopata matokeo mazuri,” alisema Mulugo.


Naibu waziri huyo aliongeza kuwa hata wale waliopata daraja la tatu si wote watakaochaguliwa kwenda kidato cha tano kwani uchaguzi huo utazingatia kuwiana kwa masomo husika (combination) pamoja na vigezo vingine vya kitaaluma.


“Kwa hiyo, hata hao 23,000 waliopata daraja la kwanza hadi la tatu, si wote watakaokwenda form five (kidato cha tano) katika shule za Serikali, wapo wengine pia watajiunga na shule binafsi na wengine watakwenda vyuo vya ufundi,” alisema na kuongeza:


“Sisi serikalini tutaangalia wale waliopo na wanaotimiza vigezo vya kitaaluma ndiyo tutakaowachagua, maana hatuna jinsi, kazi yetu sasa ni kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto zilizosababisha wanafunzi wetu kufanya vibaya.”
Mulugo pia alikiri kwamba athari hizo pia zitaathiri vyuo vikuu baada ya miaka miwili kwani wanafunzi watakaohitimu kidato cha sita, idadi yao itakuwa ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya vyuo hivyo.

Vyuo vikuu
Profesa Maboko alisema: “Vijana watakaomaliza kidato cha sita kwa matokeo hayo ni wachache hivyo itapunguza idadi ya wanafunzi watakaoingia vyuo vikuu miaka miwili ijayo.”
Alisema hivi sasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na vyuo vyake vishiriki vina uwezo wa kuchukua wanafunzi 7,000 hivyo kusema ni dhahiri kwamba wanafunzi watakaoingia miaka miwili ijayo watakuwa pungufu.


Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (Muccobs), Profesa Faustine Bee alisema matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa juzi yatakuwa na athari kubwa nchini.


“Matokeo hayo siyo mazuri. Wanafunzi wamefanya vibaya sana kwa hiyo athari yake ni kubwa hasa katika kupata wanafunzi wenye sifa ya kujiunga na elimu ya juu. Mbali na vyuo vikuu kujikuta vikikosa wanafunzi wenye sifa, lakini taifa litakuwa limetengeneza Watanzania wenye uwezo mdogo wa kupambanua mambo jambo ambalo ni hatari.”


“Kama hakuna msingi mzuri wa elimu ni tatizo maana kama wanafunzi wengi wanafeli kidato cha nne kutakuwa na athari kubwa sana katika kutengeneza taifa lenye watu waelewa.”


Mhadhiri katika wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Profesa Faustine Lekule alisema kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne kutakuwa na madhara makubwa katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu kukosa idadi ya kutosha ya wanafunzi.
Profesa Lekule alisema athari hizo zitavikumba pia vyuo vya ufundi na kwamba Serikali itakosa nguvu kazi yenye ujuzi.

No comments:

Post a Comment