Watu watano wameuawa na
wengine 23 kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na waasi katika
jimbo la Kordofan Kusini, kwa mujibu wa taarifa za redio ya taifa.
Mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, alisema kuwa
makombora matano yalirushwa ndani na nje ya mji mkuu wa Kordofan Kusini,
Kadugli,hali iliyosababisha wafanyakazi wa kutoa misaada kukimbilia
usalama wao katika maeneo ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa
Mataifa.
Waasi hao wamekiri kufanya mashambulizi hayo ingawa walikana kama raia walijeruhiwa.
Waasi wamekuwa wakipigana katika jimbo la
Kordofan Kusini, karibu na mpaka wa Sudan Kusini , tangu mwaka jana
lakini mji wa Kadugli umekuwa tulivu kwa miezi kadhaa kabla ya kuanza
tena kwa vurugu hizo.
Sudan Kusini ambayo ilijitenga na Sudan mwaka jana, imekana madai ya kuunga mkono waasi hao.
Redio ya taifa, Radio Omdurman, haikusema ikiwa majeruhi walikuwa raia au wanajeshi.
Awali, jeshi la Sudan, lililaumu waasi wa SPLM-North, kwa mashambulizi hayo.
Msemaji wa jeshi la Sudan, alielezea kuwa waasi
wa SPLM-North walijaribu kuingia ndani ya mji wa Kadugli na kushambulia
eneo lenye umbali wa kilomita sita, Mashariki mwa Kadugli.
Umoja wa mataifa ulisema kuwa wafanyakazi wake
wa misaada waliondolewa katika eneo hilo na kupelekewa katika kambi ya
jeshi kama hatua ya tahadhari.
Mfanyakazi mwingine wa umoja huo alidokeza kuwa
mashambulizi yalianza nyakati za asubuhi, akiongeza kuwa makombora
mawili yalianguka katika makao ya shirika la UNICEF ingawa hayakulipuka.
Mapigano katika jimbo la Kordofan Kusini,
yamekuwa mojawapo ya maswala nyeti ambayo yamekuwa yakichochea hali ya
taharuki kati ya Sudan na Sudan Kusini katika mwaka mmoja uliopita.
No comments:
Post a Comment