Mhando atemwa rasmi Tanesco

  *Ni uchaguzi wa CCM Wazazi
  *Wa UVCCM wapingwa kwa JK
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi William Mhando

Bodi  ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), imemwachisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Mhandisi William Mhando, baada ya kukutwa na hatia ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya  madaraka.

Hatua hiyo imechukuliwa na bodi hiyo baada ya Mhando na maofisa wengine watatu waandamizi wa shirika hilo kusimamishwa kazi Julai 16, mwaka huu, kupisha uchunguzi huru na wa haki ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo.

Maofisa hao waandamizi ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Huduma za Tanesco, Robert Shemhilu; Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi na Ununuzi, Harun Mattambo.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jenerali Mstaafu Robert Mboma, alisema katika taarifa kwa umma iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana kuwa, hatua hiyo imechukuliwa baada ya bodi kujiridhisha kuwa Mhando alifanya makosa yanayohusiana na kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi kinyume cha taratibu za shirika.

“Hivyo, basi kufuatia makosa hayo, Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco iliamua kumwachisha kazi Mhandisi William Geofrey Mhando kuanzia tarehe 29.10.2012,” alisema Jenerali Mboma kupitia taarifa hiyo.

Alisema baada ya Mhando na maofisa wengine waandamizi kusimamishwa kazi, ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Mashirika ya Umma ilifanya uchunguzi ili kubaini ukweli juu ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili Mhando.

Mboma alisema katika uchunguzi huo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Mashirika ya Umma, aligundua kuwapo kwa ushahidi dhahiri wa ukiukwaji wa taratibu za shirika na matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya Mhando.

Alisema baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Mashirika ya Umma, bodi iliteua jopo la watu watatu kusikiliza utetezi wa Mhando dhidi ya tuhuma mbalimbali zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu huyo wa Hesabu za Mashairika ya Umma.

“Baada ya kumsikiliza jopo hilo lilimkuta Mhandisi William Geofrey Mhando na hatia dhidi ya makosa yanayohusiana na ukiukwaji wa taratibu za shirika, ikiwamo mgongano wa kimaslahi,” alisema Mboma na kuongeza:

“Pamoja na yote yaliyoelekezwa hapo juu, tarehe 29.10.2012, Bodi ilikutana na kujiridhisha kuwa Mhandisi William Geofrey Mhando alifanya makosa yanayohusiana na kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi kinyume cha taratibu za shirika.”

Julai 27, mwaka huu, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Nishati na Madini, John Mnyika, aliweka bayana tuhuma zinazomkabili Mhando.

Mnyika, ambaye ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), alirejea tuhuma hizo kwa kuweka sawa uhusika wa Mhando katika uamuzi wa kupotea Sh. bilioni 6 kwa mwezi na jinsi alivyoipatia kampuni ya mkewe zabuni ya Sh. milioni 88.4.5.

Alisema kulitokea mahitaji ya umeme wa dharura kukahitajika ununuzi wa mafuta kwa ajili ya kuwasha mitambo ya IPTL ili kukidhi pengo hilo la umeme.

Kutokana na mahitaji hayo, Wakala wa Ufilisi, Vizazi na Vifo (Rita), ambayo ndiyo mufilisi wa IPTL aliweka wazi kuwa katika kampuni zenye uwezo wa kuuzia IPTL mafuta, kampuni ya Puma Energy ndiyo iliyokuwa ikiuza kwa bei rahisi.

Kwa mujibu wa Mnyika, Rita ilibainisha kuwa Oryx ilikuwa inauza mafuta hayo kwa Sh. milioni 1.6 kwa tani wakati Puma Energy iliyokuwa BP zamani ikiuza tani moja kwa Sh. milioni 1.40.

Kutokana na hesabu hizo, Mnyika alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alitoa kibali kwa Rita inunue mafuta kutoka Puma, inayouza kwa bei nafuu.

Mnyika alisema wakati Maswi aliagiza mafuta ya bei rahisi yanunuliwe tangu Julai jana, Septemba 27, Mhando alisaini mkataba kununua mafuta kutoka Oryx kwa Sh. milioni 1.5 kwa tani.

Pia alisema wiki moja kabla ya hapo, Mhando alishasaini mkataba mwingine na kampuni ya CamelOil kununua mafuta kwa Sh. milioni 1.44 kwa tani na kukatisha mkataba na Puma, ambayo ilikuwa inauza kwa bei nafuu.

Alisema cha kushangaza, wakati Oryx na CamelOil zikitoa bei tofauti, Tanesco ilianza kununua mafuta hayo kutoka kampuni hizo mbili kwa bei ya Sh. 1,850 kwa lita wakati bei ya Puma ilikuwa Sh. 1,460 kwa lita na hivyo kuipotezea serikali mapato ya Sh. bilioni 6.2, ambazo zingeokolewa kama Puma ingepewa kazi hiyo.

Alisema Mhando akijua ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, aliipa kampuni binafsi ya mkewe, Santa Clara Supplies Ltd zabuni ya ugavi wa vifaa vya ofisi vya Tanesco kwa gharama ya Sh. milioni 884.

Kwa mujibu wa Mnyika, Mhando alitoa zabuni hiyo akijua kuwa yeye ni Mkurugenzi na mwanahisa wa kampuni hiyo binafsi pamoja na mkewe, Eva Steven William, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na watoto.

Kutokana na tuhuma hizo, Mnyika aliomba iundwe Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi.

Pia aliomba Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aamuru hatua za uchunguzi za kijinai zichukuliwe dhidi ya Mhando kuhusu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

No comments:

Post a Comment