Serikali yaondoa fao la kujitoa kwenye Muswada
Waziri
wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, ameondoa rasmi sehemu inayohusu
‘fao la kujitoa’ kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali ili
kupata muda wa kutosha wa kuandaa na kuleta Muswada wa Sheria
utakaokidhi matakwa ya Azimio la Bunge na mahitaji ya kuwa na mfumo
endelevu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Alisema wakati serikali inalifanyia kazi Azimio la Bunge kabla ya
kuandaa Muswada wa Sheria kusudiwa, itafanya majadiliano na wadau wote
wakiwemo wabunge, vyama vya wafanyakazi, waajiri na wananchi.
Pia alisema watatoa elimu kwa umma kuhusiana na suala la fao la kujitoa
na maudhui ya hoja binafsi ya Mbunge wa Kisarawe (CCM), Seleman Jafo,
kwa ujumla wake kama yalivyoridhiwa na bunge.
Waziri Kabaka alisema hayo bungeni jana, wakati akisoma kauli ya serikali kuhusu sehemu hiyo.
“Hakuna ubishi kwamba hoja iliyoletwa na kuridhiwa na Bunge ina
umuhimu. Serikali inatambua umuhimu wa Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii na kwa kuzingatia uzito wa suala la fao la kujitoa pamoja na
mapendekezo yaliyojitokeza kwenye hoja ya Jafo,” alisema.
Alisema bunge liliunda kikosi kazi ambacho kimefanya utafiti na kuandaa
mapendekezo ili kuona kama kuna manufaa ya kuendelea na mfumo uliopo au
kama kunahitajika mfumo mpya kama ilivyokusudiwa.
Alisema baada ya serikali kupitia taarifa ya kikosi kazi imebaini kwamba
yapo mambo ya msingi kadhaa ambayo sharti yawe yameshughulikiwa kwanza
kwa kina kabla ya kuandaliwa kwa Muswada utakaokidhi matakwa ya hoja ya
Jafo kama ilivyoridhiwa na Bunge Agosti, mwaka huu.
“Serikali baada ya kutafakari kwa kina imejiridhisha kuwa kurejesha tu
fao la kujitoa kama ilivyokuwa katika Muswada wa Marekebisho wa Sheria
za Hifadhi za Jamii, 2012 wakati huu, bado hakutakidhi kiu ya mabadiliko
yanayohitajika ya Mfumo wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini kutoa
mapendekezo ya marekebisho ya sheria kuhakikisha kwamba mifuko iliyoko
kwenye sekta hiyo inalinda haki za wanachama kwa namna inayojitosheleza.
No comments:
Post a Comment