Ripoti ya Tume ya MV Skagit yabaini kasoro kibao

Tume ya kuchunguza ajali ya boti ya MV Skagit, imekamilisha uchunguzi wake na kubainisha kuwa Nahodha aliyekuwa akiendesha boti hiyo hakuwa na sifa wala ujuzi na kupendekeza viongozi kadhaa wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Kutokana na kutokuwa na ujuzi, Nahodha huyo alishindwa kuwaandaa abiria wake kujiokoa wala kutoa taarifa ya dharura kwa vyombo vinavyohusika na mambo ya usalama, licha ya kuona boti yake ipo katika hatari za kuzama.

Katibu Mkuu Kiongozi wa SMZ, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alisema serikali imeyakubali mapendekezo yote na kuyafanyia kazi kwa kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu waliohusika na uzembe na kusababisha vifo vya watu wasio na hatia.

Dk. Abdulhamid ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, alisema Nahodha Makame Mussa Makame alikuwa akiendesha boti ya MV Skagit bila kuwa na cheti cha umahiri.

Alisema kitendo hicho ni kinyume na sheria kifungu 167(1), cha sheria ya usafiri wa baharini Zanzibar namba 5 ya mwaka 2006.

Aidha alisema ripoti hiyo imebaini Nahodha alikuwa akiendesha meli hiyo, huku akijua meli hiyo haipo salama kwa kutokuwepo Mhandisi Mkuu wakati wa safari zake, na badala yake alikuwepo Mhandisi Msaidizi asiye na sifa kitu ambacho ni kinyume na kifungu cha sheria ya usafiri wa baharini 321(1) namba 5 ya mwaka 2006.

Aliongeza kuwa uzembe umebainika baada ya meli hiyo kupakia abiria 431 badala ya uwezo wake wa abiria 250 kitu ambacho ni kinyume na kanuni ya 4 na 5 za kanuni ya hesabu na usajili wa abiria ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 2011.

Alisema ripoti hiyo imebaini maiti 81 zilipatikana na kutambuliwa majina yao, na watu 212 wamepotea kusikojulikana, na 154 waliokolewa katika ajali hiyo wakiwemo raia wa kigeni 18, na watatu walikufa.

Alisema tume imependekeza mmiliki na nahodha wa boti hiyo washitakiwe kwa kosa la kusababisha vifo kutokana na uzembe.

Jaji Abdlhakim Ameir Issa, ambaye alikuwa akiongoza tume hiyo alisema tume imependekeza aliyekuwa Kaimu Mkaguzi wa meli, Juma Seif Juma, achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuisajili boti ya MV Skagit na kuipatia cheti cha usajili wa muda pamoja na cheti cha usajili wa kudumu bila ya kufuata masharti ya usajili yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria katika kifungu cha 31 namba 5 ya mwaka 2006.

Tume hiyo pia imependekeza Mkaguzi wa kujitegemea, Captain Saad Shafi Adam, kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufutwa uteuzi wake wa kuwa mkaguzi wa meli anayetumiwa na ZMA, kwa kutoa mapendekezo ya kusajiliwa MV Skagit, baada ya kuifanyia ukaguzi ambao haukufuata masharti ya vifungu vya 192 na 194 vya sheria ya usafiri wa baharini, namba 5/2006.

Wengine waliopendekezwa na tume hiyo kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni Maafisa Usalama wa Bandari ya Dar es salaam, Johari Mikidadi, Ndumbati na Peter Ndimbwa Mwasi, kwa kushindwa kudhibiti uingiaji wa abiria kinyume na majukumu yao ya kazi.

“Tume inapendekeza Mmiliki wa meli hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Seagull Sea Transport Said Abdulrahman Mbuzi achukuliwe hatua za kisheria kwa kufanya biashara ya usafiri wa baharini kwa kutumia chombo ambacho hakikusajiliwa kwa mujibu wa sheria ya usafiri wa baharini Zanzibar namba 5/2006,” alisema Dk. Abdulhamid Mzee.

Aidha, tume hiyo imependekeza fidia za aina tatu za kuwalipa waathirika sawa na kima cha chini cha mshahara kwa muda wa miezi 80. Kima cha chini cha Zanzibar Sh. 150,000 kitakipwa kwa waliofariki, wakati walionusurika na kupata ulemavu walipwe asilimia 75 ya kiwango hicho, na asilimia 50 ya kiwango hicho walipwe walionusurika bila ya kupata ulemavu.

No comments:

Post a Comment