Jaji Warioba: Wananchi zaidi ya 900,000 watoa maoni Katiba Mpya
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba, amesema hakuna chombo chochote kilichowahi kuwafikia
watu wengi nchini zaidi ya tume yake, ambayo hadi awamu ya tatu ya kazi
yake ya kukusanya maoni inamalizika, imekwishafikiwa na wananchi zaidi
ya 900,000 kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya katika mikoa 24 ya Tanzania
Bara na Zanzibar.
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana, kwa lengo la kutoa tathmini baada ya
tume yake kumaliza awamu ya tatu na kuendelea na awamu ya nne, ambayo ni
ya mwisho ya kazi yake ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba
Mpya.
Alisema katika awamu zote hizo, tume
imefanya jitihada kubwa kuhakikisha inakutana na kila kundi katika
jamii, wakiwamo makundi tisa ya watu wenye ulemavu, ambao alisema wote
wamepata maoni yao.
“Hakuna chombo kilichowahi kupata watu
wengi kama tume hii. (Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus
Kibamba) Aniambie ni chombo gani katika nchi hii kilichowahi kuwafikia
watu wengi? Anataka tume ifanye kazi kulingana na mawazo yake na siyo
kwa kufuata sheria,” alisema Jaji Warioba.
Alisema awamu ya tatu ya kazi ya tume yake
ilifanyika kuanzia Oktoba 8 hadi Novemba 6, mwaka huu katika mikoa ya
Rukwa, Njombe, Iringa, Singida, Tabora, Mtwara, Kilimanjaro, Kaskazini
Unguja na Kaskazini Pemba.
Jaji Warioba alisema awamu ya kwanza
ilifanyika kati ya Julai 2-30, mwaka huu na kwamba, ilihusisha mikoa ya
Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga
na Tanga.
Alisema katika awamu ya pili, iliyofanyika
kuanzia Agosti 27 hadi Septemba 28, mwaka huu, tume ilitembelea mikoa
ya Kigoma, Lindi, Mwanza, Morogoro, Mbeya, Katavi na Ruvuma.
Jaji Warioba alisema katika awamu ya tatu
iliyomalizika Novemba 6, tume ilifanya mikutano 522 katika mikoa yote
tisa ingawa ilipanga kufanya mikutano 496.
Alisema hali hiyo ilitokana na mahitaji
mapya katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo na kuifanya tume kuitisha
mikutano ya ziada ili kuwapa fursa wananchi wengi zaidi.
Jaji Warioba alisema katika awamu ya pili, tume ilifanya mikutano 449 wakati awamu ya kwanza ilifanya mikutano 388.
Alisema katika awamu ya tatu, wananchi
392,385 walihudhuria mikutano na kwamba, wananchi 21,512 walitoa maoni
yao kwa kuzungumza katika mikutano hiyo na wananchi 84,939 walitoa maoni
ya kwa maandishi.
Aidha, alisema katika awamu hiyo, wananchi 1,639 walitoa maoni yao kwa kuzungumza na pia kwa maandishi katika mikutano hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alisema tume
inaridhika na kazi inavyoendelea na namna wananchi wanavyojitokeza kutoa
maoni kwa njia mbalimbali zilizotolewa na tume.
Alisema tume yake haitaingilia misimamo ya
vyama vya siasa vinavyominya uhuru wa wafuasi wao kutoa maoni na kusema
kazi ya tume ni kuchukua maoni na kwamba, yeyote anayetoa maoni popote
aliko watayachukua.
No comments:
Post a Comment