Bunge likiendelea katika Kikao cha tisa cha mkutano wa 11wa Bunge mjini Dodoma jana.
Picha na Edwin Mjwahuzi
Na Sharon Sauwa
Dodoma. Baadhi ya wabunge
wamesema kukosekana bungeni kwa wenzao wanaofikia 200 hata kuhesabiwa ni
watoro, kumetokana na wengi wao kutokamilisha ahadi kwa wapigakura wao
walizotoa mwaka 2010, hivyo kulazimika kukimbilia majimboni ili kujaribu
kuzikamilisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti bungeni hivi
karibuni, walisema wengi wao bado hawajakamilisha ahadi walizoahidi
walipoomba kura na sasa umefika mwaka wa uchaguzi.
“Wengine wamesafiri nje ya nchi kikazi. Si unajua
hiki ni kipindi kigumu kwa sababu tunaingia kwenye uchaguzi. Wamekwenda
majimboni kufanya maandalizi ya uchaguzi,” alisema Mbunge wa Mufindi
Kusini (CCM), Mendard Kigora.
Alisema yeye yupo bungeni tangu Mkutano wa 19 ulipoanza kwa sababu ameshakamilisha ahadi zake kwa asilimia 90.
“Sina wasiwasi, nimekuja bungeni kuhakikisha
nashiriki kutunga sheria zote, ili ‘next year’ (mwaka ujao) tuzisimamie
vizuri. Sitaki muswada hata mmoja unipite,” alisema Kigora.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Christowaja
Mtinda alisema wabunge wengi wako majimboni kwa sababu huu ni wakati wa
lala salama na hawajakamilisha ahadi walizoahidi.
“Wapo majimboni kuwaweka sawa wananchi wao kabla
ya uchaguzi hasa kwa upande CCM, wengine wako huko kwa ajili ya
kuhakikisha wananchi wanapigia kura ya ndiyo Katiba Inayopendekezwa,”
alisema.
Alisema wabunge walio chini ya Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), wana ratiba kila wanapokamilisha mikutano ya Bunge
hurudi majimboni kwao kwa ajili ya kutekeleza ahadi zao.
“Sisi hatuko kama upande wa pili (CCM), hatusubiri
hadi uchaguzi ukaribie. Tuna ratiba, tukitoka hapa tunakwenda moja kwa
moja majimboni kukamilisha ahadi zetu,” alisema.
Mbunge wa Karagwe (CCM), Godbless Blandes alisema
kuwa wabunge wengine wako katika kamati mbalimbali za Bunge wakijadili
miswada itakayowasilishwa katika vikao vinavyoendelea.
“Miswada ni mingi inayoingia katika Bunge hili,
kwa hiyo wakati mwingine unakuta wabunge wako katika kamati zao
wakijadili miswada yao,” alisema.
Alisema wabunge wengine wana dharura za kuugua au
majimboni mwao kuna kero hali inayowalazimu kwenda huko kuzitatua kabla
ya kurejea tena kwenye vikao vya Bunge.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR Mageuzi), Moses Machali alisema
wabunge wengi wana wasiwasi na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika
Oktoba mwaka huu, hivyo wako majimboni.
“Presha imepanda, wako majimboni wanajitahidi kuweka mambo sawa kabla ya uchaguzi,” alisema.
Hata hivyo, alisema yeye hana wasiwasi kwani anajua wenye haki ya kumpa kura katika uchaguzi ni wananchi.
“Hakimu wa ubunge wangu ni mwananchi. Kama wanaona
nilifanya vyema basi watanichagua tena, wao ndiyo wenye ‘kisu’ bwana
wanaamua, nipite, nisipite ni sawa tu kwa kuwa mimi sina uamuzi wa
mwisho,” alisema Machali.
Kukithiri kwa utoro kwenye vikao vya Bunge la
Jamhuri ya Muungano vinavyoendelea ilibainika hivi karibuni baada ya
ofisi ya chombo hicho cha kutunga sheria kusema kuwa kina taarifa za
wabunge 15 pekee walioomba ruhusa kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Bunge hilo, linalotakiwa kuwa na wabunge 357,
lilishindwa kupitisha miswada mitatu iliyohitaji theluthi mbili ya
wabunge wa kila upande wa Muungano.
Wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya
Usimamizi wa Maafa uliowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), Jenister Mhagama wiki iliyopita
kulikuwa na wabunge 81 ndani ya Ukumbi wa Bunge, jambo linalomaanisha
kuwa takriban wabunge 250 hawakuwamo.
Hali ilikuwa mbaya zaidi wakati kikao cha Bunge
hilo kilipoanza kujadili Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa
Silaha na Risasi kwani kulikuwa na wabunge 29 tu ukumbini.
Hali hiyo ilimaanisha kwamba zaidi ya wabunge 320 hawakuwamo ndani kujadili suala hilo nyeti kwa mustakabali wa Taifa.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Shughuli za
Bunge, John Joel alisema : “Wabunge 15 tu ndiyo wenye ruhusa, wengine
wapo lakini wanaingia na kutoka bungeni. Kutokuwapo kwao kunaathiri sana
wakati wa kupitisha miswada kutokana na kutotimia kwa akidi.”
Idadi ya wabunge walio na ruhusa ni ndogo
ikilinganishwa na viti vingi vinavyokuwa vitupu wakati wa mijadala
mbalimbali kwenye vikao vya Mkutano wa 19 vinavyoendelea mjini Dodoma.
Ofisi ya Bunge imeeleza kuwa jambo hilo linathiri shughuli mbalimbali za Bunge zinazotakiwa kufanyika.
Kaimu kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu
anasema utoro wa wabunge unakwamisha mambo mengi ya msingi bungeni, huku
akibainisha kuwa miswada haiwezi kupitishwa huku kukiwa na idadi ndogo
ya wabunge na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka kanuni.
“Ukiingia bungeni unakuta ukumbi mtupu kabisa,
lakini ukitoka nje unakutana na wabunge wengi wakizurura. Kanuni
zinasema kuwa ili muswada upitishwe inatakiwa kuwe na wabunge walau
nusu,” alisema Lissu.
Lissu alisema huenda kukosekana kwa wabunge hao kukawa kunachangiwa na Uchaguzi Mkuu, kwani wengi wamejikita majimboni.
“Pia wapo ambao wamekwenda safari za kibunge, lakini si wengi kufanya Bunge liwe tupu.”
Wabunge wengi hawaonekani bungeni, lakini wamekuwa
vinara wa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii katika majimbo yao
hasa kipindi hiki, kitu kinachoonekana kuwa ni kujiweka karibu na
wananchi.
Wengi wanajishughulisha na kuchangia masuala ya
maendeleo pia kuendesha au kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira wa
miguu katika majimbo yao.
Mbali na kutoonekana bungeni kutokana na kujikita
kuweka mikakati ya ushindi majimboni, baadhi ya wabunge pia wamekuwa
watoro wa kuhudhuria vikao vya Bunge, kama wakionekana asubuhi, jioni ni
nadra kuwaona.
Baada ya kujadili muswada wa Uhamiaji wiki
iliyopita, Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohamed Habib Mnyaa aliomba
mwongozo wa Spika kuhusu idadi ya wabunge kuwa ndogo.
Mbunge huyo alisema kwa idadi hiyo itakuwa kinyume
na kanuni kama Bunge litapitisha muswada. “Ninavyofahamu ili tuweze
kupitisha muswada huu wabunge tunaotakiwa kuwemo humu ndani ni kuanzia
176, lakini nikitizama idadi yetu hata 100 hatufiki, kutokana na suala
hili naomba mwongozo wako,” alisema Mnyaa.
Akijibu suala hilo, Spika Makinda alisema: “Naona kuna watu wapo kwa ajili ya kukwamisha vitu tu. Haya tuendelee.”
Baada ya majibu ya Spika, idadi ya wabunge iliongezeka kidogo na kufikia 139.
Akizungumzia muswada huo, Lissu alisema itakuwa
vigumu kupitishwa kwa sababu unatakiwa kupigiwa kura na theluthi mbili
ya wabunge wa Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar.
“Sijui kama muswada huu utaweza kupita maana ukitizama idadi ya
wabunge si rahisi kupata theluthi mbili kutoka Zanzibar na Tanzania
Bara,” alisema Lissu. Licha ya idadi kuwa ndogo, mjadala uliendelea na
hatimaye muswada huo ukapitishwa.
Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan alisema utoro
huo hautoi picha nzuri kwa wananchi kwani wabunge ni wawakilishi wa
wananchi na wanatakiwa kuhudhuria vikao vya Bunge.
Mbunge wa Songwe (CCM), Philipo Mulugo alisema:
“Kukosekana kwa mbunge kuna sababu nyingi, wapo walioomba ruhusa
kutokana na kuwa na sababu maalumu na pia wapo waliopo majimboni. Ila
binafsi naona ushiriki wetu bungeni ni jambo muhimu.”
Tangu kuanza kwa vikao vya Mkutano wa 19 wa Bunge
Machi 17 mwaka huu, idadi ya wabunge imekuwa ndogo ikilinganishwa na
hali ilivyokuwa katika Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge uliokuwa na
mahudhurio makubwa kutokana na kujadili sakata la Akaunti ya Tegeta
Escrow.
Katika mkutano wa 18 ulioisha Februari mwaka huu,
wabunge wengi waliokuwa wakichangia hoja, walijikita katika kuzungumzia
matatizo ya majimbo yao na kuacha mjadala uliokuwa mezani.
Jambo hilo lilimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwataka wajikite kwenye hoja za msingi na si kuzungumzia masuala ya majimbo
No comments:
Post a Comment