Mafuriko yaibua wanyama hatari, Nigeria
Wanyama hatari kama vile Mamba, Nyoka na Viboko wameanza kuingia
kwenye makaazi ya watu katika eneo la kati nchini Nigeria.
Mafuriko makubwa yaliyokumba Nigeria yamepelekea mito iliyofurika kusomba wanyama hao hadi kwenye nyumba za wenyeji.
"kuna
kiboko ndani ya nyumba yangu," Mkaazi wa Jimbo la Benue Wuese Jirake
akaiambia BBC. "natarajia kiboko huyo ataondoka atakapochoka kujificha
nyumbani kwangu."
Mamia ya watu wamefariki na wengine kuachwa bila
makao huku mashamba yakiharibiwa na mafuriko hayo makubwa zaidi kuwahi
kukumba Nigeria kwa miongo mingi.
'tunatumai yatakwisha' Jirake akaiambia BBC
akiongezea kwamba kwa hivi sasa maji yamejaa nyumbani kwake kufikia kina
cha kiunoni.
"iwapo kuna njia ya kumuondoa kiboko huyu basi maafisa wa Serikali wanafaa kunisaidia."
Kulingana na Mwandishi wa BBC Is'haq Khalid, hali kama hiyo pia imeripotiwa katika Miji ya Makurdi, Agatu, Logo na Adoka.
Shirika la taifa la kushughulikia hali za
dharura limesema linashirikiana na Wakuu wa Jimbo la Benue na wahusika
wengine kuhakikisha walioathirika na mafuriko wamerudi kwenye nyumba
zao.
Mshirikishi wa Shirika hilo katika eneo la
kaskazini ya kati nchini Nigeria, Abdussalam Muhammad, ameiambia BBC
kwamba sio salama kwa wenyeji kurudi majumbani mwao baada ya wanyama
hatari kuingia humo.
"kwa hivi sasa kuna Mamba, Nyoka na wanyama
wengine hatari waliosombwa na mafuriko kwenye nyumba hizo, na huenda
wakawadhuru watu na kuhatarisha maisha yao," akasema.
Muhammad amewataka wakaazi kusubiri maagizo kutoka kwa Shirika hilo pale mafuriko yatakapopungua.
No comments:
Post a Comment