Mauaji ya albino,ukataji viungo vyazidi kutikisa nchi (3)

Ofisa mmoja wa polisi alipendekeza nimwulize Kulwa kama mabaki ya Maganga bado yapo kaburini kwa kuwa halikujengewa kwa nondo na zege.

Nilimshauri awasilishe wazo lake kwa viongozi wake ili waiombe Mahakama ruhusa ya kulifukua kaburi la Maganga na kupata uhakika kama viungo vyake bado vipo au vimeondolewa.
Niliwaacha polisi wakiendelea na uchunguzi wao na mimi nikaanza safari ya kurejea Dar es Salaam.

Nilipokea taarifa za jaribio la kumdhuru mtoto wa miezi saba ambaye ana ulemavu wa ngozi, Makunga Baraka Februari 5, mwaka huu katika Kijiji cha Nyaruhande, Kitongoji cha Nyasubi, Kata ya Nyaruhande, Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu. Nilizungumza na mama mzazi wa mtoto huyo, Jane Daudi ambaye aliniambia kuwa alikuwa amehifadhiwa kwa muda katika kituo cha polisi kwa usalama wa mwanae.

“Nilipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni George wa eneo la Ndiko. Akaniambia, “Dada nakuhurumia sana kwa kuwa una mtoto mwenye ulemavu wa ngozi.  Niliwasikia watu hotelini wakipanga njama za kuja kumuua.”  Niliogopa sana na nikamweleza mama yangu. Tukaenda hadi kwa mwenyekiti wa mtaa hatukumkuta. Baadaye tukatoa taarifa kwa wanakijiji.

Hawakutuamini. Hawakutaka kuja kutulinda. Kabla ya saa tatu usiku watu watatu walikuja nyumbani kwetu na kuanza kuturushia mawe dirishani na mlangoni. Wanakijiji wakawaona na wakawafukuza lakini hawakuwakamata. Usiku ule wanakijiji walipeana zamu kutulinda.”

“Kesho yake asubuhi Mwenyekiti wa Mtaa akaniandikia barua kwenda polisi na wanakijiji wakatusindikiza. Polisi wanafuatilia taarifa nilizowapa. Naogopa sana. Nahofia maisha ya mwanangu Makunga. Sitaondoka polisi hadi hapo nitakapopata ulinzi mkali,” anasema Jane.

Maria Chambanenge (39)
Nilipokea taarifa nyingine za kushambuliwa kwa Maria Chamanenge (39) katika Kijiji cha Mkowe, Miangalua, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Mkoa wa Rukwa.

Nilikwenda kumwona Maria katika Hospitali ya Mkoa ya Sumbawanga. Kulikuwa na ulinzi mkali na tulielezwa kwamba tunapaswa kupata kibali cha polisi ili kumtembelea wodini.
Kamanda wa Mkoa wa Polisi alikuwa safarini kikazi.  Maofisa tuliowakuta walituelekeza kuwa kibali kinapatikana kwa Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO).

Tulirejea tena hospitali na baadaye tulionana na Kaimu Mganga Mkuu, alitupa idhini ya kuzungumza na Maria lakini chini ya usimamizi.

Maria alikuwa bado ana maumivu makali, baada ya kukatwa mkono wa kushoto. Madaktari walituhakikishia kwamba hali yake inaendelea vizuri kwa upande wa matibabu. Swali lilikuwa je, kwa upande wa kisaikolojia?

Maria ni albino na haoni vizuri. Sasa ameongezewa ulemavu wa viungo. Huyu ni mama wa watoto wanne: Shukuru (8), Edron (6), Rahab (3) na Emma (miezi mitano). Mama huyu ni mke wa tatu wa Gabriel Yohana. Atawaleaje watoto wake akiwa na mkono mmoja sasa? Atafanyaje kazi za nyumbani na za kilimo bila mkono wa pili?

Baada ya kumjulia hali, nilimwomba anielezee jinsi alivyoshambuliwa na kukatwa mkono wa kushoto usiku wa Februari 11, mwaka huu, chumbani akiwa amelala na wanae.
“Usiku wa manane, kati ya saa saba na saa nane hivi, Nilisikia vishindo vya nyayo vikitokea sebuleni ambako mwanangu Shukuru na Edron walikuwa wamelala. Ghafla nikamwona mume wangu ameshika upanga ananishambulia kichwani. Nikawa nashangaa na kuwaangalia usoni bila kujua kwa nini alikuwa ananishambulia. Akasema, “Nyamaza!” Mimi nikawa nalia. Akasema, Pole!  Nyamaza!”

Hospitalini hapo, Mama mdogo wa Maria, Everada Palachi (42) alikuwa amesimama kando ya kitanda cha Maria akiwa amembeba Emma.

Amekuwa akimlea mtoto huyo wa Maria na huku akimuuguza Maria. Baada ya kukatwa mkono anahitaji kusaidiwa kwa mambo mengi tu sasa.  

Everada akaingilia kati, “Wewe unajua unasema nini?”  akanigeukia, “Maria amechanganyikiwa!”
Maria akajibu kuwa hajachanganyikiwa bali mume wake, ndiye aliyempiga panga kichwani mara tatu na alishirikiana na wengine watatu (majina nayahifadhi kwa sababu wanachunguzwa na polisi – wapo rumande) na kumkata mkono wake wa kushoto na kukimbia nao.

Everada alisisitiza kuwa Maria amechanganyikiwa. Akaanza kuzungumza naye Kinyiha (kabila la watu wa eneo hilo).

No comments:

Post a Comment