Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,Dk Marina Njelekela
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam juzi. Kulia ni
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa hospitali hiyo,Agnes Kuhenga.
HOSPITALI ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es
Salaam, imeanza mkakati wa kudhibiti mianya ya ufisadi chini ya
mpango utakaowawezesha wagonjwa, kulipia gharama za huduma kupitia
benki.
Pamoja na mkakati huo, menejimenti ya hospitali hiyo kubwa
nchini, imesema imebaini kuwa mrundikano wa wagonjwa, unachangiwa na
udhaifu katika utoaji tiba kwenye hospitali za mikoa na wilaya.
Akizungumzia mkakati wa kudhibiti mianya ya
ufisadi, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Marina Njelekela,
alisema uchunguzi umebaini hatua ya kutumia benki katika kukusanya
malipo ya gharama za huduma mbalimbali, itasaidia kuokoa zaidi ya
asilimia 20 ya fedha zinazopotea.
“Kufanikiwa kwa mkakati huu, kutaiwezesha
hospitali kuvuka lengo la kugharamia bajeti ya matuminzi ya kawaida, kwa
kutumia mapato ya ndani kwa asilimi 40 kama sera ya mabadiliko ya
taasisi za umma inavyoeleza,” alisema Dk Njelekela.
Alisema mabadiliko ya mfumo wa ukusanyaji wa
mapato kwa kutumia benki, yataongeza uwezo wa kifedha kwa matumizi ya
kawaida ya mapato ya ndani kutoka asilimia 58 hadi kufikia zaidi ya
asilimia 72 katika mwaka wa fedha wa 2013/14.
Mkurugenzi huyo alisema tayari hospitali
imeingia makubaliano na Benki ya NMB, ili kutekeleza mkakati wa
kukusanya mapatio yake na kwamba hatua hiyo itaanza rasmi Machi 11 mwaka
huu.
“Mfumo huo utamwezesha mgonjwa kupata hati ya
gharama ya malipo ya huduma itakayokuwa inatolewa na mfanyakazi wa
hospitali katika kituo cha karibu na huduma ,’”alisema
Kuhusu hospitali kuelemewa na idadi kubwa ya
wagonjwa, mkurugenzi alisema udhaifu katika utoaji wa huduma za tiba na
hasa hospitali za mikoa na wilaya, unachangia kwa kiasi kikubwa.
Alisema
kama Seriklai itaboresha huduma katika hospitali hizo kwa kuzipatia
madaktari wa kutosha na wataalam, tatizo hilo litapungua kama si
kumalizika kabisa .
Alisema Shirika la Afya la Dunia (WHO,) litaka
daktari mmoja kuwahudumia wagonjwa 10,000 lakini kwa Hospitali ya
Muhimbili madaktari wake wanatoa huduma kwa zaidi ya idadi hiyo.
Akizungumzia tatizo la wagonjwa kulala sakafuni,
mkurugenzi alisema tatizo si upungufu wa vitanda na kwamba tatizo ni
nafasi ya kuweka viwanda vya wagonjwa.
Alisema majengo ya hospitali yalijengwa kwa uwezo wa kuwekeza vitanda 35 tu.
No comments:
Post a Comment